in , , ,

Ukimsifu Theo Walcott, mgeukie Arsene  Wenger

Alisajili vijana kutoka nchini kwake Ufaransa, akasajili vijana wa England, akawaakuza na kuwafanya kuwa nyota wakali..

KWA mara nyingine tena jina la Arsene Wenger linazidi kutawala katika mchezo wa mpira wa miguu. Moja ya vipaji vilivyoletwa na Arsene Wenger katika klabu ya Arsenal ni winga mwenye kasi Theo Walcott. Winga huyo ametangaza rasmi kustaafu kucheza mpira wa miguu akiwa na klabu ya Southampton. 

Nyota huyo ni miongoni mwa vipaji vilivyoaminiwa na kocha Arsene na kuwaaminisha maelfu ya mashabiki kuwa anaweza kucheza soka kwa kiwango cha juu. Ilikuwa kazi ngumu mashabiki kukubaliana na kile kilichoonwa na benchi la ufundi la Arsenal. Ilikuwa kazi ngumu kuamini kinda wa miaka 17 angeweza kupenya kwenye kikosi cha kwanza cha  Arsenal. 

Ulikuwa mradi mgumu kuaminiwa kwa mashabiki lakini Wenger alikusanya vijana wengi wenye vipaji na akawafanya wawe nyota wa mpira wa miguu. Walcott amekuwa miongoni mwa mawinga walioonesha uwezo mkubwa katika kikosi cha klabu yake pamoja na timu ya Taifa. Ukimweka Walcott kwenye ushindani na winga kama Jamie Penant, bila shaka ungeona kasi ya Walcott ikipenya kikosi cha kwanza. 

Tanzania Sports

Ni uwezo wa kukaa na mpira, kufunga mabao,kucheza kitimu,kusaidia ulinzi, pamoja na kuwa mchezaji aliyeweza kutumika kwenye mashambulizi ya kushtukiza. Theo Walcott anabaki kuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa muhimu kwenye mipango ya Arsene Wenger. Wakati dunia ilikuwa ikiamini mastaa wakubwa kwenye timu zao, Wenger alikuwa na mtazamo mwingine. 

Alisajili vijana kutoka nchini kwake Ufaransa, akasajili vijana wa England, akawaakuza na kuwafanya kuwa nyota wakali. Wakati akimsajili Theo Walcott kutoka Southampton wengi waliona kama anabahatisha tu. Hata ujio wa beki wa kushoto kama Kieran Gibbs, kiungo Denilson toka Brazil, Abou Diaby kutoka Ufaransa ilikuwa kama vile Arsene Wenger anafanya masihara katika kazi yake. 

Hata hivyo Wenger  aliwaaminisha vijana hao kuwa wana vipaji vya kutikisa ligi yoyote. Kati yao Walcott ndiye mchezaji mashuhuri zaidi. Hadi anaamua kutundika daruga ametoa mchango mkubwa kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya Taifa. Theo Walcott amefanikiwa kufunga mabao mengi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa kuliko wachezaji nyota na waliotwaa mataji kama vile Ronaldo De Lima (Brazil), David Villa (Hispania), Zinedine Zidane (Ufaransa), Carlos Tevez(Argentina) na Michael Owen (England). 

Mnamo mwaka 2019 Theo Walcott alitunukiwa tuzo ya kucheza mechi 300 za Ligi Kuu England. Mwaka 2017 alifunga bao la 100 la Arsenal kwenye robo fainali ya kombe la FA. Nyota huyo alijiunga na Arsenal Januari 20 mwaka 2006. Katika maisha yake ya soka amecheza na nyota kama vile Alexis Sanchez,Alex Chamberlane, Santi Carzola,Mathieeu Flamini,Cesc Fabregas,Alexandre Hleb,Mesut Ozil kwa kuwataja wachache. Amedumu katika EPL kwa miaka 18.

Theo James Walcott amecheza mechi 563 na kufunga mabao 129, pamoja na kuitumikia Timu ya Taifa kwa mechi 47 na kuifungia mabao 8 kwenye mashindano mbalimbali. maisha yake ya mpira wa miguu yalianzia kwenye akademi ya vijana wa Southampton. Alijiunga na Arsenal kwa pauni milioni 5. 

Wakati anajiunga Southampton alikuwa na umri wa miaka mtoto mdogo. Lakini alipofikisha miaka 16 alisajiliwa na Arsene Wenger na kumfanya aishi katika klabu hiyo kwa miaka 12. Lakini amestaafu soka akiwa katika klabu yake ya utotoni ya Southampton. 

Tanzania Sports

Huyu ni kati ya mawinga ambao wameadimika si tu kwenye EPL bali ligi nyingi duniani zinakabiliwa na changamoto ya mawinga kutokana na mabadiliko ya mifumo ya uchezaji inayosisitizwa na makocha. Mifumo ya sasa inawataka wachezaji ambao wanaweza kuitumikia timu na kupunguza matumizi ya vipaji binafsi. Theo anastaafu katika mazingira ambayo mawinga wanaadimika kila kukicha.  

Wakati maelfu ya washabiki wakimtakia kila lenye heri Theo Walcott wanatakiwa kumgeukia bingwa wa kuendeleza vipaji, yaani Arsene Wenger. Kocha ambaye aliweka imani yake kwa kinda mwenye umri wa miaka 16 na kumwaga noti ili amsajili toka Southampton. Ni dhahiri nyota huyu atakumbukwa kwa kasi yake, mabao,chenga na uwezo wa kucheza kitimu lakini sifa nyingine zimwendee Wenger kwa uvumilivu na kulea kipaji hicho.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Wadhamini Ligi Kuu nunueni haki za sura za wachezaji

Tanzania Sports

Kwanini Liverpool wamemsajili Wataru Endo?