in , ,

Hizi ndizo faida za Simba Super Cup

Simba Super Cup

Urafiki ambao utawapa nafasi nyingine Simba SC kuwaalika tena kwa ajili ya mashindano mengine endelevu

Jana Simba SC walizindua michuano mipya ambayo wao ndiyo waandaaji. Michuano hiyo itaitwa Simba Super Cup na itashirikisha timu tatu ambazo ni Simba SC ya Tanzania, Al Hilal ya Sudan na TP Mazembe ya, DR Congo.

Michuano hii itafanyika katika uwanja wa Mkapa. Mengi yamezungumzwa kuhusu michuano hii, kwa pamoja tutazame faida ya michuano hii kwa Simba SC.

Kuna faida kuu mbili ambazo mimi binafsi nimeziona kwenye michuano hii. Faida ya kwanza ni nje ya uwanja ambapo Simba SC itajenga mahusiano na faida ya pili ni ndani ya uwanja ambapo Simba SC itapata kutokana na kupata mechi za kimataifa za kirafiki.

Tuanze na faida ya kwanza ya nje ya uwanja. Nje ya uwanja Simba SC itabahatika kujenga mahusiano chanya ya kibiashara kwa njia mbili. Njia ya kwanza ni mahusiano ya kibiashara na timu ambazo zimealikwa na Simba SC kwenye michuano hii.

Simba SC kuwapa mwaliko TP Mazembe na AL Hilal kisha kuwapa nafasi ya kuwalipia kila kitu kuanzia tikiti ya ndege, malazi na chakula kitawapa nafasi kubwa kwa Simba SC kujenga urafiki mkubwa na hivi vilabu.

Urafiki ambao utawapa nafasi nyingine Simba SC kuwaalika tena kwa ajili ya mashindano mengine endelevu. Pia kitendo cha kuwadumia hawa wageni wakubwa barani Afrika kutawapa nafasi kubwa Simba kujenga imani kwa vilabu vingine.

Itakuwa rahisi kwa Simba SC kuwaalika vilabu vingine na kukubaliwa kwa sababu ya kufanikisha haya mashindano kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo hii itakuwa hatua ya kwanza ya kujijengea uaminifu kwa vilabu vingine.

Ukiachana na mahusiano ya Simba SC na vilabu pia Simba itajenga mahusiano makubwa na mashabiki wake. Kwa sasa inauwezo wa kuleta vilabu vikubwa hapa nchini.

Mashabiki watakuwa na nafasi kubwa ya kuviona vilabu vikubwa barani Afrika hivo mashabiki watakuwa na uwezo wa kuja kwenye viwanja. Kuja kwenye viwanja kunaongeza msisimko wa mashindano.

Msisimko ukiongezeka kutavutia wadhamini kuja kuwekeza kwenye michuano hiyo. Kutavutia pia vituo vya habari kununua haki ya matangazo ya michuano hiyo. Kwa hiyo mahusiano ya kibiashara yatajengwa vyema kupitia michuano hii.

Faida ya pili ni ndani ya uwanja. Simba kwa sasa haina kocha mkuu. Kocha mkuu atakuja kipindi ambacho michuano hii inaanza. Kuja kwake kwenye michuano hii itamsaidia sana kukijenga kikosi chake.

Pili , kwenye kundi la Simba SC kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika wapo na As Vita ya DR Congo pamoja na El Marreikh ya Sudan bila kusahau Al Ahly ya Misri. Simba SC imealika timu ambazo zinatoka ukanda mmoja na timu ambazo wako nazo kwenye kundi kwa hiyo hii itakuwa na faida kubwa sana kwao Simba.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
VAR

VAR ilivyobadilisha soka

Didier Gomes Da Rosa

SIMBA ni WCB ya mpira wa miguu ?