Upo ukweli mchungu na mbaya kwamba vyombo vya michezo vya Uingereza vimeshindwa kukabiliana na kashfa ya ubaguzi wa rangi.
England Netball ni moja ya vyombo 80 vinavyosimamia michezo nchini hapa na vilivyotoa tamko la pamoja wakisema kwamba hawajafanya jitihada za kutosha katika kukabiliana na ubaguzi wa rangi, ambapo watu weusi au wenye asili ya Afrika ndio waathirika wakubwa zaidi.
Vyama hivyo – ikiwa ni pamoja na British Athletics, British Cycling na England Netball – vimechapisha taarifa ambayo aina yake haikupata kutolewa kabla; kwamba hawajajielekeza ipasavyo katika ngazi zote kuanzia ile ya chini kabisa hadi juu kwenye bodi za uongozi.
Tamko lililochapishwa na Sport and Recreation Alliance, linasema kwamba michezo haiwezi tena kuendelea katika hali hiyo kutegemea weusi walio katika uandamizi kwenye michezo kutoa matamko dhidi ya ubaguzi, hivyo kuna haja ya mfumo kubadilishwa ili michezo iwe shirikishi zaidi, ikitafakari na kuona uzuri wa watu wa aina mbalimbali kwenye jamii na michango yao bila kujali rangi zao.
“Haiwezekani kupata suluhu rahisi na hivyo mabadiliko yatategemea juhudi za pamoja kutoka ndani na nje ya sekta. Ni wakati mwafaka sasa kukabiliana na maswali mabaya, kujiingiza na kujihusisha na kuleta mabadiliko hata kama ni kwa majadiliano yasiyopendeza, nasi tunatakiwa kujiwajibisha,” ikasema taarifa hiyo.
Ripoti iliyochapishwa juma lililpopita inaonesha kwamba vyama vya soka, umoja wa rugby na soka, Bodi ya Kriketi ya England na Wales, Chama cha Baiskeli, tenisi, golf, riadha na kadhalika vilikuwa na mjumbe mmoja tu mweusi kwenye bodi zao.
Waziri wa Michezo, Nigel Huddleston, naye amesema kwamba atapitia upya Kanuni za Maadili ya Uongozi wa Michezo ili kuona ikiwa kuna haja ya kila bodi kulazimishwa kuwa na idadi fulani ya watu weusi na wale wanaotoka kwenye makundi mdogo ya jamii tofauti na Wazungu weupe.
“Kifo cha kutisha cha George Floyd, malalamiko ya makundi ya watu dhidi ya ubaguzi na ukatli yaliyotolewa kutoka pande mbalimbali duniani yakifuatiwa na ujumbe mzito wa ‘Black Lives Matter’ kutoka kwa wanaharakati yamefanya kila sehemu ya jamii kuona hilo na kuukabili ukweli mchungu,” wakasema.
Wakaongeza kwamba michezo na burudani vina wajibu wenye ushawishi mkubwa juu ya kuweza kuleta mabadiliko ya maana na wakati huu umepelekea sekta husika kujifikiria upya, kusikiliza, kuhoji, kujifunza na kwa uwazi kabisa kujadili jinsi ya kuchukua hatua chanya dhidi ya ubaguzi na kuhakikisha kuna usawa miongoni mwa watu wote bila kujali rangi zao.
“Inafikiriwa kwamba hadi hatua hii, hatujafanya inavyotakiwa wala kutosha. Ni wakati wa kukabiliana na ubaguzi na ukosefu wa usawa ulio katika michezo yote, kuanzia ngazi za chini hadi kwenye bodi ambapo weusi wanakosa ushirikishwaji unaotakiwa,” wakasema.
Vyombo hivyo vya michezo pia vimeitaka serikali kujielekeza na kuahidi kutoa nyongeza katika rasilimali na kugharamia uletwaji wa usawa wa watu, kama ambavyo imejitolea kuhakkisha inaondoa ubaguzi kwenye maeneo mengine.
Story nzuri yenye kueleweka, kaka najifunza mengi kutoka kwako