Dirisha dogo la usajili lilifungwa tarehe 31 mwezi uliopita na
kushuhudia timu mbalimbali zikinunua na kuuza baadhi ya wachezaji.
Hawa ni baadhi ya wachezaji bora kusajiliwa na timu mbalimbali, na
jinsi ambavyo watazisaidia timu zao katika mifumo tofauti.
Alexis Sanchez, ametoka Arsenal na kujiunga katika timu ya Manchester United.
Msimu wa mwaka 2014/2015 alihusika kwenye 1/3 ya magoli ya Arsenal
akifunga magoli 30 na kutoa pasi za mwisho za magoli 15 kwa msimu
mzima.
Ana miaka mitatu akiwa katika nchi ya England hii ni moja ya faida
kubwa kwa Manchester United. Wamebahatika kuchukua mchezaji ambaye
siyo mgeni wa ligi kuu ya England.
Faida ya pili, Alexis Sanchez kihalisia ni mchezaji wa pembeni na
Manchester United wamekuwa wakikosa mchezaji halisi wa pembeni hivo
kuja kwake itakidhi mahitaji ya timu.
Faida ya tatu, Alexis Sanchez ana uwezo wa kucheza kama false 9, hivo
anaweza kutumika kukidhi mahitaji ya timu kipindi ambacho haina
Lukaku, pia Alexis Sanchez anauwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa
pili( nyuma ya mshambuliaji wa kati).
Swali kubwa na zito ni kama Alexis Sanchez ataweza kuibeba vizuri jezi
namba 7. Jezi yenye historia kubwa na klabu ya Manchester United
ambapo iliwahi kuvaliwa na watu wazito kama Bryan Robson ( “Captain
Marvel”), Eric Cantona, David Beckham , Cristiano Ronaldo. Tangia
Ronaldo mwaka 2019 hakuna mtu ambaye amefanikiwa kufanya makubwa na
jezi hii. Je Sanchez atafanikiwa?
Henrikh Mkhitaryan na Pierre- Emirick Aubameyang kwenda Arsenal.
Wanakutana tena kwa mara nyingine katika timu ya Arsenal baada ya
kuwahi kuwa pamoja katika timu ya Borrusia Dortmund
Swali kubwa kwa mashabiki wengi wa Arsenal namna ambavyo Arsene Wenger
anaweza kuwatumia Laccazate , Ozil, Mkhitaryan na Aubameyang kwa
pamoja.
Wote wanne wanaweza kucheza pamoja katika mifumo ifuatayo.
Mfumo wa kwanza ni mfumo wa 4-2-3-1 ambapo katikati watakaa Wilshere
na Xhaka/Ramsey, mbele yao atakuwepo Mesut Ozil , pembeni kushoto
atakuwepo Mkhitaryan na pembeni kulia atakuwepo Aubameyang na
mshambuliaji wa mwisho atasimama Lacazzate.
Pia hata katika mfumo wa 4-4-2 Diamond pia unaweza ukawafanya wacheze
pamoja huku mbele wakitumia washambuliaji wawili yani Laccazate na
Aubameyang.
Msimu huu Aubameyang amefanikiwa kufunga jumla ya magoli 21 akiwa
Borrusia Dortmund hivo anaenda kucheza na watu wanaojua kutengeneza
nafasi za magoli kama Mkhitaryan na Ozil, hivo uwepo wake utaongeza
nafasi ya ufungaji wa magoli katika timu ya Arsenal.
Lucas Moura kwenda Tottenham Hotspurs , ni usajili ambao haujaongelewa
sana kwenye vyombo vya habari.
Ila ni usajili ambao utakuwa na matokeo makubwa ambayo yatazungumzwa
sana kwenye vyombo vya habari. Lucas Moura anakuja kuongeza kasi
katika eneo la mbele la Spurs, uzoefu wake wa kukaa kwenye timu kama
PSG, kushiriki mara kwa mara kwenye michuano ya ligi ya mabingwa
barani ulaya kutakuwa ni faida kubwa kwa Tottenham Hotspurs.
Theo Walcot kwenda Everton, miaka 15 akiwa katika timu ya Arsenal na
amefanikiwa kufunga magoli 100+ ikiwa ni wastani wa kufunga magoli 10
kwa kila msimu, uzoefu wake wa ligi kuu ya England ndicho kitu ambacho
Everton wanaenda kunufaika nacho, pili ni mshambuliaji ambaye anaweza
kutokea pembeni na akafunga au kutengeneza magoli.
Everton wamekuwa hawana wachezaji ambao wanauwezo wa kufunga wakitokea
pembeni, pia Walcot ana uwezo wa kusimama kama mshambuliaji wa mwisho.
Van Djik kwenda Liverpool. Wamekuwa wakiteseka sana eneo la nyuma.
Wanampata beki Van Djik ambaye anauwezo mzuri wa kukaba, pia anafaida
kubwa hata kwenye kushambulia kwa kuanzisha mashambulizi kwenye timu
na kufunga magoli kwa kutumia mashuti, mipira iliyokufa na mipira ya
kichwa inayotokana na kona.
Giroud kwenda Chelsea. Magoli 105 akiwa Arsenal ndani ya misimu
mitano, wastani wa kufunga magoli 20 ndani ya msimu mmoja, anaweza
akaonekana siyo mtu sahihi kwa Chelsea, ila kwa matumizi ya muda mfupi
Chelsea wamepata kilichokizuri. Katika takwimu za msimu huu Chelsea
ndiyo timu pekee iliyopiga krosi nyingi.Giroud ni moja ya watu
wanaotumia vizuri Krosi kufunga. Anaweza kutumika katika mfumo wa
3-5-2 ambao unaonekana kutumiwa na Conte msimu huu. Ambao Mbele akakaa
yeye na Morata , Morata akacheza kama mshambuliaji wa pili na Giroud
akacheza kama mshambuliaji wa kwanza. Au katika mfumo wa 3-4-3 ambapo
mbele wanakaa Giroud kama mshambuliaji wa kati, Morata na Hazard.
Aymeric Laporte kwenda Manchester City. Usajili mzuri kwa Manchester
City. Ni aina ya mabeki wanaoendana na aina ya uchezaji wa Pep
Guardiola. Anaanzisha mashambulizi vizuri akiwa nyuma, timu zote za
Pep Guardiola huanza kujenga mashambulizi nyuma. Pia kulikuwa na
changamoto ya majeruhi katika eneo la mabeki wa nyuma hivo kumuongeza
Laporte kutakuwa na msaada mkubwa kwa Manchester City katika kuongeza
ukubwa wa kikosi.