in , ,

KWANINI SPURS WALIIFUNGA MANCHESTER UNITED?

Usiku wa kuamkia leo Manchester United walienda katika uwanja wa
Wembley kama wageni wa Tottenham Hotspurs.

Uwanja ambao walikuwa hawajawahi kufungwa tangu mwaka 2011 ambapo
walifungwa na Barcelona 3-1 katika fainali ya ligi ya mabingwa.

Baada ya hapa walishinda mechi 6 huku kila mechi wakifunga goli mbili,
walikuwa na rekodi ya kuvutia kwenye uwanja wa Wembley lakini Jose
Mourinho alikuwa na rekodi mbaya dhidi ya Mauricio Pochettinho.
Mauricio Pochettinho kabla ya mechi ya jana alikuwa hajafungwa mechi
tatu alizocheza nyumbani dhidi ya Jose Mourinho.

Kipi kikubwa kilichompa nguvu jana Mauricio Pochettinho?

Timu yake kucheza kwa ushirikiano ndicho kilikuwa kitu kikubwa kwa
Tottenham Hotspurs.

Timu zote zilikuwa zinacheza mfumo wa 4-2-3-1 , mfumo huu ulionekana
kuwa na faida kwa Hotspurs kwa kiasi kikubwa kuliko kwa Manchester
United, kwa sababu Tottenham Hotspurs walikuwa na viungo wawili ambao
kiasi ni wazuri sana kukaba, Eric Dier na Dembele, kumweka Dembele
kwenye hii mechi kilikuwa na faida kubwa sana kwa sababu alikuwa na
uwezo wa kushuka chini kuchukua mipira na kupanda nayo juu.

Kitu ambacho Paul Pogba hakufanikiwa kukifanya, mara nyingi alishindwa
kumsaidia Nemanja Matic katika majukumu yake ya kukaba hivo kumfanya
Nemanja Matic kuwa peke yake na kuelemewa kwa kiasi kikubwa. Tofauti
na kwa upande wa Eric Dier ambako alikuwa na usaidizi mkubwa wa
Dembele.

Pili, wachezaji watatu wa Tottenham Hotspurs ambao walikuwa wanacheza
nyuma ya Harry Kane ambao ni Son, Delle Ali pamoja na Erricksen
walikuwa wanashuka katikati mwa uwanja kuongeza idadi ya viungo
katikati ya uwanja.

Kuna wakati Manchester United ilipokuwa na mpira eneo la katikati mwa
uwanja lilikuwa na idadi isiyokuwa na uwiano sawa kati ya wachezaji wa
Tottenham Hotspurs. Mfano mara nyingi ilikuwa 2 v 4 au 3 v 5 yani
wachezaji wawili wa Manchester United dhidi ya wachezaji wanne wa
Spurs , au wachezaji watatu wa Mnachester United dhidi ya wachezaji
watano wa spurs.

Hiki kitu hakikuleta uwiano mzuri eneo la katikati mwa uwanja hivo
kuonekana Manchester United kuzidiwa kwa kiasi kikubwa eneo lile.

Ni kweli Manchester United bila Pogba huyumba?

Hapana shaka hili swali lina ukweli mkubwa ndani yake, kwa sababu Paul
Pogba hupenda kukaa na mpira pamoja na kutengeneza nafasi. Jana
Manchester United ilikuwa timu ambayo haikutengeneza nafasi kwa sababu
Paul Pogba hakucheza vizuri.

Luke Shaw au Ashley Young?

Luke shaw

Baada ya goli la kwanza kufungwa, Manchester United walijaribu kutumia
upande wa kushoto kushambulia. Young alijaribu kupiga krosi, lakini
kila kina Trippier walipokuwa wanashambulia kupitia kushoto Young
hakuwa dhabiti kwenye jukumu la kujilinda.

Kuna haja ya Luke Shaw kuanza , na kama Luke Shaw haaminiki, kwenye
dirisha la majira ya joto la usajili lijalo mkataɓa wa Luke Shaw
unamalizika , hivo ni wakati mzuri wa Manchester United kuamua kubaki
naye au hapana.

Hata kama wakibaki naye, kuna haja kubwa ya kusajili beki mwingine wa
kushoto ambaye atasaidizana na Shaw kwa sababu Shaw hukubwa na
majeraha ya mara kwa mara.

Kuna haja ya kuendelea kumwamini Jesse Lingard kama namba kumi wa
Manchester United?

Hapana, Manchester United ni timu kubwa ambayo inahitaji wachezaji
wengi wa kiwango kikubwa ndani ya kikosi ili kushindania makombe
makubwa.

Moja ya sehemu ambayo Manchester United wanatakiwa kufanya marekebisho
kwenye usajili ujao ni wao kusajili namba kumi bora ndani ya kikosi.
Henrink ameshaondoka, Mesut Ozil kasaini mkataba mpya jana na Arsenal
hivo tumaini kubwa lililobaki kwao ni kwa Paolo Dyabala wa Juventus.

Mwisho: Jana Tottenham Hotspurs ƙkilistahili kushinda kwa sababu
walitawala mchezo , goli la kwanza lilionesha kuwachanganya mapema
Manchester United kwa sababu hawakutegemea kukutana na mazingira kama
yale.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Pierre- Emerick Aubameyang: alikaribia kutua Newcastle Utd

Tanzania Sports

UCHAMBUZI WA USAJILI WA MWEZI JANUARY