in ,

Ubingwa bila mashabiki uwanjani unanogaje?

Mashabiki Uwanjani

REAL MADRID wametangaza kutumia uwanja wao wa Alfredo Di Stefano kucheza mechi zilizobakia za La Liga. Huo ni uwanja ambao umetumika mara kadhaa kwenye mechi za maandalizi au mazoezi. Ni uwanja uliopewa jina la shujaa wa klabu hiyo, Alfredo Di Stefano.

La Liga imerejea wikiendi hii kumalizia mechi zilizobaki. Klabu mbili  za Real Madrid na Barcelona zenye ushindani mkubwa zikitoana jasho kutaka kuibuka na ubingwa msimu huu.

Kwangu hakuna chaguo jingine zaidi ya kuona Real Madrid ikitwaa ubingwa wa La Liga. Litakuwa jambo muhimu kwa kocha Zinedine Zidane pamoja na bosi wake Florentino Perez ambao wapo kwenye mtihani wa kuhakikisha wanaondokana na jinamizi lililowakuta msimu uliopita.

Msimu mbaya wenye matokeo mabaya kiasi kwamba Perez alilazimika kumpigia simu Zinedine Zidane alirudi kwenye benchi la ufundi. Na Zidane alishatamka, anautaka sana ubingwa wa La Liga.

Pili, kabla ya kusimamishwa Ligi Kuu England, Liverpool walikuwa wanaongoza kwa pengo kubwa la pointi dhidi ya washindani wao Manchester City.

Liverpool wamepania kukata kiu ya taji hilo baada ya kulikosa kwa takribani miaka 30. Ni miaka mingi. Mashabiki wameishi kwa matumaini, wengine wamepoteza maisha. Wengine siku zao za kuishi zilishatimia. Wengine walikuwa vijana, na sasa wamezeeka huku kiu yao ya kitwaa taji hilo ikiota mbawa kila msimu.

Jurgen Klopp amewaonesha Liverpool namna ya kuamini katika nguvu zao. Amewapindua kutoka kwenye shimo la kukata tamaa hadi kwenye kuamini wanaweza kutwaa taji hilo.

Endapo mlupiko wa ugonjwa wa Korona usingekuwepo hadi leo Liverpool wangekuwa wanasherekea ubingwa wa EPL. Hakukuwa na namna yoyote kuona Liverpool wangekubali kushindwa dakika za mwisho. Ni vigumu kutokea hilo hata wakati ambao EPL inarejea tena viwanjani.

Ni mwaka wa Liverpool. Wana mabeki wakali wa kati. Kiongozi wao ni Virgil van Diyk. Mimi hupendelea kumwita Vivi au V.V. Ni bonge la mkoba. Laiti angelikuwepo kwenye safu moja na mwamba kama Sergio Ramos pale Real Madrid hakika mambo yangelikuwa matamu zaidi ya uwepo wa Raphael Varane au alivyokuwa Pepe Lima.

V.V ni silaha ya tatu ya Liverpool katika mafanikio yake. Silaha yao ya kwanza ni Jurgen Klopp, ya pili ni golikipa wao Allison Becker. Mo Salah, Mane na Firmino ni matokeo ya kusuka timu imara. Ufundi wa Firmino ndio chachu ya mafanikio ya Salah na Mane.

Nchini Ujerumani nako Bundesliga ilirejea mapema kuliko zingine. Mitanange mbalimbali imekuwa ikichezwa huko kwenye viwanja vitupu. Wachezaji wanacheza lakini kiwango cha makabiliano sio kama kile cha awali. Mashabiki wamejikunyata kwenye masofa nyumbani mwao kuhofia ugonjwa wa Korona.

Nchini Ufaransa bingwa wa Ligi Kuu yao maarufu kama Ligue 1 ni PSG. Chama cha soka nchini humo kiliamua kwa pamoja kuipa ubingwa PSG. Ubingwa huo ulitolewa bila mashabiki kuwepo. Ni mtihani kweli kweli.

Nchini Italia nayo itakuwa kwenye mchuano mkali wa kuwania ubingwa wa Serie A. Inter Milan na Juventus ni miongoni mwa timu zenye kuchagiza mvuto mara kwa mara.

Inter Milan imerejea kwa kishindo msimu huu ikiwa na kocha Antonio Conte ambaye amewahi kufungiwa virago katika klabu ya Chelsea. Nako ligi itachezwa bila mashabiki kuwepo uwanjani.

Ligi Kuu Tanzania Bara nako imerejea huku masharti yaliyotolewa na serikali ni yaleyale timu kucheza bila mashabiki. Ingawaje waliruhusiwa mashabiki 10 wa kila upande, lakini ilionekana uamuzi huo haukuwa sahihi.

Uwezekano wa mashabiki kutinga uwanjani upo, lakini vipi hatari ya ugonjwa Korona ambao ulisababisha ligi karibu zote duniani kusimamishwa? Hili ni muhimu kuchukua tahadhari na ikiwezekana kuwazuia mashabiki wasiovaa barakoa kuingia viwanjani.

BILA MASHABIKI NI UKIWA

Iwe kwenye chandimu. Iwe kwenye ndondo. Iwe kwenye ligi daraja la kwanza, pili, tatu au Ligi Kuu, kukabidhiwa ubingwa bila kuwepo mashabiki hakunogi. Wachezaji wanakuwa wamekosa kitu fulani.

Pengo la mashabiki haliwezibwa kwa kuwaruhusu watano au 10. Utamu wa soka ni pale mashabiki wanapojazana kwenye uwanja wa Anfield wakishuhudia kocha wao akirusha ngumi hewani na kuwapongeza kwa kuishangilia timu yao.

Kelele za mashabiki ndani ya Santiago Bernabeu zina raha zake. Wakiimba jina la Sergio Ramos, watageukia la Federico Valverde, kisha watamwimba kocha wao Zinedine Zidane. Hawajasahau kuwaimba Marcelo, Carvajal,Benzema,Rodrygo, Toni Kroos, Modric na wengine. Ni kocha gani hapendi kelele za mashabiki wake? Hakuna kabisa.

Kwenye uwanja wa San Siro kila shabiki angependa kuona Inrer Milan pengine itwae ubingwa kisha kelele zao zitande ndani humo. Hata kama ikiwa kwa Juventus nako hivyo hivyo. Mashabiki kwenye viwanja vya Borussia Dortmund, Bayern Munich na nyinginezo zingependa mashamsham ya mashabiki wao.

Uhondo wa mashabiki ni pale wachezaji wanapopachika mabao na kukimbilia kwenye viti vyao kushangilia pamoja. Uhondo wa mashabiki ni pale wanapoimba majina ya wachezaji wao.

Amsha amsha ya mashabiki ni kitu kimoja kizuri kwenye viwanja vya soka. Kuimba bila kuchoka. Kucheza bila kuchoka. Kuwahamasiha wachezaji wao bila kuchoka. Ikibidi kuwazomea pia wanaposhindwa. Kuwachochea ari zaidi pale wanapochoka.

Kimsingi kelele za mashabiki zinakuwa tamu. Utamu wake unajulikana kwa mashabiki wenyewe na wachezaji. Mabenchi ya ufundi yanafahamu uhondo wa mashabiki wao. Kutoruhusu mashabiki maana yake timu zinacheza mpira zikiwa na ukiwa.

Bila mashabiki timu inapopewa ubingwa inakuwa na ukiwa. Pengo la mashabiki hata kwa timu iliyoshindwa msimu ni kubwa. Wachezaji wakishindwa kutwaa ubingwa wanahitaji sapoti ya mashabiki.

Wachezaji wanapookoa timu yao kwenye mstari wa kushuka daraja wanahitaji kupongezwa na mashabiki. Wachezaji wanapofungwa wanahitaji mashabiki kwa vile wanajua watafanya vizuri mechi zingine au msimu mwingine. Bila mashabiki ubingwa hainogi.

Utanogaje wakati amsha amsha, kelele, mbwembwe na ngebe zinakosekana? Yaani mashabiki washangilie ubingwa wa mezani (bila kutokwa jasho uwanjani wakishangilia timu zao)? Hakika ni mtihani mkubwa.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Tanzania: Mkazo zaidi michezoni unatakiwa..

Shahanga

Gidamis Shahanga: shujaa wa riadha Tanzania