in , , , ,

Tuweke mikakati TOC mpya

*Ukame wa medali kwa miaka 22 ufike mwisho

*Uchaguzi uwe fursa kwa waliosomea michezo

Mchakato umeanza kwa ajili ya kupata safu mpya ya viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).
Uchaguzi mkuu wa chombo hiki muhimu umepangwa kufanyika Desemba 8 mwaka huu katika makao makuu ya nchi – Dodoma.
Uchaguzi huu unakuja wakati wadau wengi wa michezo wakiwa bado na kumbukumbu mbichi za jinsi taifa lilivyofanya vibaya kwenye Michezo ya 30 ya Olimpiki iliyoanza jijini London Julai hadi Agosti.
Nimeonelea ni muhimu kuandika, ili kukumbushana mapema kabla muda wa kuchukua fomu za kugombea haujaisha, kwamba hili ni jambo kubwa.
Ukame wa medali kwa miaka 22 sasa ni dhihirisho la changamoto kubwa na nyingi zinazoikabili TOC, hivyo kuna haja ya wadau kufikiria mara mbili mbili kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika.
Ndiyo kusema kwamba matokeo ya London, ambapo wanamichezo wetu na ujumbe wa viongozi wengi walikuwa katika utendaji wa kimazoea, bila ubunifu wala mawazo mapya ya kuling’arisha taifa.
Kwa hiyo, Rais wa TOC,  Ghulam Rashid alipotangaza jijini Dar es Salaam kwamba mchakato wa uchaguzi unaanza chini ya Kamisheni ya Uchaguzi inayoongozwa na mwanasheria Lloyd Nchunga, nilisubiri kuona makubwa.
Ni bahati mbaya kwamba bado sijayaona, naendelea kusubiri kama wengine, lakini siku zinakatika na imebaki pungufu ya wiki moja mwisho wa uchukuaji fomu ufike.
Je, utafiti unaofaa umefanyika ili kujua kiini cha kufanya vibaya miaka yote au tunaendelea tu na ratiba za uchaguzi, watu waingie madarakani, mashindano yaje, wasafiri na kupata posho, wakose medali na maisha yaendelee kama kawaida?
Palikuwa na haja kabla ya viongozi wa sasa kuondoka madarakani wawekwe kitimoto na wenye chama chao, ikiwa ni pamoja na serikali ambayo ni kama mlezi.
Wanaomaliza muda wangeeleza walifanya nini, yepi mafanikio yao, walikwama wapi, nani kikwazo na walichukua hatua gani kujikwamua?
Haitatosha kusimama siku ya uchaguzi kabla au baada ya viongozi wapya au wa sasa kuchaguliwa tena, kuchomoa karatasi yenye hotuba ndefu, kuisoma na kisha kuifutika mkobani na kupigiwa makofi.
Hiyo si TOC tunayoitaka, si kazi tuliyowatuma watu hawa kuifanya na kama ni uvumilivu, miaka 22 ni mingi mno, hivyo ikiwa waliopita hawakuulizwa, kisiwe kigezo cha hawa kuachwa wakapita.
Kama kweli tuna uchungu na jinsi jina la nchi yetu linavyopotea kwa kutotangazwa, lazima sasa watokee watu waseme basi, na watu hao wapo, hivyo waingie kuinusuru TOC.
Hii ni kwa sababu chama hiki kimebaki tu jina, lakini utendaji haupo, maana ungekuwapo ungedhihirika kwenye vitendo mashindanoni.
Jirani zetu wa Kenya na Uganda wanajitahidi na wameanza kutuchukulia sifa zetu kidogo kidogo kama ilivyokuwa London walikopata medali.
Imefika mahali mpaka Wazungu wakiuliza ikiwa Kenya ndiko kuna mlima Kilimanjaro, na wanajibiwa ndio! Wakitaka kuupanda mlima huo wanatoka makwao na kutua kwanza Nairobi, wanaipatia Kenya mapato na sifa nyingi.
TOC ingeweza kuwa kipaza sauti cha maliasili na maeneo makubwa ya urithi wa kitaifa yaliyopo Tanzania kwa wachezaji kupeperusha vyema bendera ya nchi yetu.
Uchaguzi huu wa TOC unatakiwa kutuzindua, kutufikirisha sana, kwa sababu wenzetu wanatumia michezo kukuza uchumi wao. Uingereza ni moja ya nchi hizo, ina kile wachumi wanachoita ‘service economy’, ambapo michezo inajenga uchumi kwa njia mbalimbali.
Kwa mfano, majuzi tu imetangazwa kwamba Uingereza imeondoka tayari kwenye mdororo wa uchmi kwa sababu ya mapato yaliyotokana na Michezo ya 30 ya Olimpiki.
Kumbe walio ndani ya TOC, serikalini na kwenye vyama mbalimbali wanatakiwa kuelewa kwamba siku hizi michezo ni uchumi, si burudani tu za kuitazama na kucheka.
Kamisheni ya Uchaguzi ambayo licha ya Wakili Nchunga ina Abdallah Juma, Harrison Chaulo na Hamis Ali Mzee, inatakiwa iwe tayari na mambo haya kichwani mwao.
Wakae vikao vizito na wajenge mazingira ya kupata viongozi wa kweli; ikishindikana kuona dalili za kupata viongozi bora, afadhali kuashauriana kuahirisha uchaguzi kuliko kuendelea na kazi kwa mazoea (business as usual).
Tunataka kupata wanamichezo na viongozi wa kweli kweli katika nafasi za Rais, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi.
Hatutaki kabisa watu legelege huko, wala kwenye nafasi za Mweka Hazina, Mweka Hazina Msaidizi na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ambapo nafasi tano ni za Tanzania Bara na tano za Zanzibar na yule mjumbe kutoka Kamisheni ya Wachezaji (KAWATA).
Kamisheni ya Uchaguzi itajua aina ya wanaowania kugombea kwa kupitia fomu zao, lakini pia kuchungua na kupata taarifa za ziada kuwahusu.
Wawania uongozi wakishatoa ada za fomu za kugombea ambazo ni Sh 200,000 kwa nafasi ya Rais hadi Mweka Hazina Msaidizi na Sh 150,000 kwa ujumbe wa Kamati ya Utendaji, mchujo uwe mkali.
Usaili wa Dar es Salaam Novemba 20 na Zanzibar Novemba 24 uwe kweli kitimoto cha kuipitisha dhahabu na ghafi yake kwenye moto ili kupata dhahabu safi.
Lakini, Kamisheni ya Uchaguzi ambayo hatuna budi kuweka imani kwayo, haitaweza kuchuja na kupitisha viongozi bora ikiwa mwito wa kuwania hautapokewa na wadau wa michezo.
Hima watu wajitokeze kwa wingi, maana hili ni eneo korofi linalohitaji mtu makini wa kulinyoosha, na kama ni ugonjwa, basi daktari bingwa anatakiwa kujongea kuifanya kazi.
TOC ni chombo nyeti kwa nchi na maendeleo ya michezo, lakini hali inavyokwenda bado haujaonekana msisimko na mwamko wa kweli kwa watu kuwa na nia ya kukirejeshea heshima chombo hiki.
Tutakaa pembeni hali lini baadala ya kuwania kugombea ili tuongoze? Tusiwe watu wa kulalamika tu, kukosoa au kuchekelea mafanikio bila kuwa sehemu yake.
Leodeger Tenga alililiwa sana kuingia kwenye uongozi wa soka, akawa akikataa kwa sababu ya shughuli zake, lakini alifika mahali akaitika mwito, akaingia kwenye uongozi.
Hebu wakereketwa wa michezo wajitokeze katika siku hizi chache zilizobaki wachukue fomu ili wagombee uongozi, tuijenge tena Tanzania yetu kimichezo.
Tunajua kwamba TOC inaiwakilisha Tanzania katika Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC). Wanachama wakuu wa TOC ni vyama vya taifa vya michezo inayochezwa Olimpiki na Jumuiya ya Madola.
Kwa msingi huu, kama ni wadau wenye uwezo wa kuongoza, wapo wengi na ni kiasi cha wao kujitokeza, ili Kamisheni ya Uchaguzi iwapitishe kwa sifa walizo nazo kugombea mbele ya wanachama ili kukidhi matakwa ya demokrasia.
Iwe marufuku hata hivyo, watu kujitokeza kugombea uongozi ili wakale pesa, kwa vile wanajua kuna fedha nyingi hutolewa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).
Wapo wenye uchu wa kuzitafuna pesa hizo na kupata posho kwenye safari za mikutano, semina na mashindano mbalimbali, ili eti wamalizie nyumba, wanunue magari mengine na kujiendeleza kimaisha binafsi.
Hiyo si shabaha ya kuwataka wadau wajitokeze, bali wanatakiwa watakaotoa ushirikiano wa dhati kwa wadau.
Tunataka watu wenye uwezo wa kuongoza, kuratibu na kushirikiana na vyama vingine vya michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Wizara ya Michezo na serikali na umma kwa ujumla.
Sikatai watu kutetea nafasi zao kwenye uongozi wa sasa unaomaliza muda wake, lakini watetee wakiwa tayari ‘kukaangwa’ kwa rekodi zao, ambapo wanaweza wakepa au wakapepetwa.
Lakini maswali yanabaki juu ya wenye uwezo mkubwa na wanaopendwa na wadau kutojitokeza kwenye nafasi hizi. Je, hawana uzalendo kwa taifa lao na watu wake?
Hebu watu wajitokeze, lakini baada ya tafakari ya kina na kupata majibu au kuwa na nia ya kushirikiana na wenzao kupata majawabu ya tatizo la ukame wa medali kwa miaka 22.
Wasomi kwenye taaluma ya michezo hii ndiyo fursa yao, kwa sababu kisomo chao kinahitajika katika uongozi wala hawakusoma bure ili waje kukaa pembeni.
Wanatakiwa hamasa ya aina yake ili wagombee, na hili linaweza kufanywa na BMT na wizara yenye dhamana ya michezo.
Inatambulika kwamba wakati mwingine watu huwa wazito kugombea, kwa vile kuna wengine wanaowatolea macho kana kwamba wana uchu tu wa vyeo, hivyo hujiweka pembeni.
Napenda kuona mchakato wa uchaguzi ukienda vyema, ukiwa na msisimko na mguso kwa watu wengi ndani na nje ya nchi, badala ya kwenda kama kutimiza ratiba tu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Liverpool wawakatalia Chelsea

CONGO YAWASILI KUIVAA SERENGETI BOYS