Miongoni mwa nyota wapya walioingia EPL ni James Rodriguez. Ni mara yake ya kwanza kucheza Ligi hiyo. Tangu alipoanza kandanda amecheza Ligi za kwao Colombia kisha akaelekea Benfica nchini Ureno na baadaye Monaco ya Ufaransa.
Real Madrid ilimsajili akiwa Monaco. Ni staa ambaye anafuatiliwa kwa ukaribu. Jina lake ni kubwa kuanzia mashindano ya ngazi ya klabu na timu za taifa. James ni nyota ambaye aling’ara kwenye fainali za Kombe la dunia mwaka 2014 na baadaye kujiunga na vibopa wa Ulaya, Real Madrid. Msimu huu wa 2020-2021 amesajiliwa na E verton. James amejiunga na kocha Carlo Ancelotti ambaye alifanya kazi naye Real Madrid.
TOFAUTI IKO HAPA
James Rodriguez anaonekana kuwa mchezaji tofauti tangu ajiunge Everton msimu huu. Mcolombia huyo anajiamini,anatafuta mpira,anachangamka, anatengeneza nafasi na tishio kwa tiu pinzani ambazo zinatakiwa kumwekea ulinzi maalumu kila dakika ya mchezo.
Chini ya Ancelotti, kikosi cha Everton msimu huu kimeanza vema, huku James akiwa mchezaji wa kutumainiwa tofauti na alipokuwa chini ya Zinedine Zidane kule Real Madrid.
Uhusiano mbovu,kukosekana ukaribu kati ya James Rodriguez na Zidane unajulikana kwenye kolido za uwanja wa Santiago Bernabeu. Hii ni miongoni mwa sababu iliyochangia James Rodriguez kupelekwa Bayern Munich kucheza kwa mkopo, na hata aliporejea hakupata nafasi ya kutosha kucheza klabuni hapo.
Sasa chini ya kocha wa zamani za Real Madrid na Bayern Munich, bosi Ancelotti, kiungo huyo amekuwa chachu ya ushindi wa Everton. Safu ya ushambuliaji ya Everton yenye kuongozwa na Richarlison, James na Calvert imekuwa tishio tangu kuanza kwa msimu huu.
Jose Mourinho akiwa na kikosi chake cha Tottenham Hotspurs walicharazwa mabao 3-0 wakiwa nyumbani. Everton wamechangamka na kumfanya James aonekane kuwa mchezaji muhimu.
James amekuwa akicheza nyuma ya washambuliaji wawili; Richaelison na Calvert. Ni grisi iliyoanza kulainisha ‘vyuma’ na kuipa ufanisi kazi ya Ancelotti. Je tofauti ya makocha Ancelotti na Zidane ni ipi katika kutumia kipaji cha James Rodriguez?
1. IMANI
Kati ya vitu vyote muhimu kwa mchezaji na kocha ni kuwa na imani baina yao. kocha anatakiwa kumwamini mchezaji na mchezaji nae anatakiwa kuwa na imani na kocha wake. Ancelotti anamwamini James Rodriguez, wakati Zidane hakuwa akimwamini staa huyo kwenye kikosi chake.
Ushahidi wa hilo upo katika mifumo ya uchezaji, mbinu na mahusiano binafsi. Kimbinu Ancelotti anaamini James anaweza kuifanya kazi ya ufungaji Everton kuwa rahisi zaidi kutokana na umahiri wake,kipaji na maarifa aliyonayo kuelekea lango la adui. Yote yameonekana Everton.
2. NAFASI
Zidane alipendelea kumtumia James kama winga akiwa Real Madrid, hali ambayo ilimtenga nyota huyo kwenye ‘move’ nyingi zilizokuwa zikisukwa kwenye mchezo. Kumweka nafasi ya winga ilikuwa kumfanya achangie maarifa yake badala ya kuwa sehemu kamili ya uzalishaji kama ambavyo Ancelotti anamtumia kwa kuwa kiunganishi cha safu ya ushambuliaji.
Chini ya Ancelotti pale Eveton tunamwona James akichza kwa uhuru zaidi, timu inamzunguka yeye na ndiye anapanga mipango ya kutengeneza mabao. James hashughuliki na suala la ulinzi, kazi yake ni kushambulia tu kwa mechi nzima.
3. KUUNGWA MKONO
Ancelotti amekuwa akimuunga mkono James kila wakati, iwe ndani ya uwanja au nje ya uwanja. Hilo halikuwepo kati ya Zidane na James walipokuwa Real Madrid. Zidane hakuwa akimsapoti nyota huyo, hata pale
alipompanga hakutoa nafasi ya kumsifu kwa uwezo mzuri anaojaribu kuonesha.
4. HADHI
Ndani ya kikosi cha Real Madrid, James alionekana kuwa mchezaji wa kutoa mchango katika Ligi Kuu pekee, lakini lilipofika suala la mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hakupewa nafasi. Jambo hilo lilisababisha sintofahamu, kwani hakuelewa kwanini anawekwa kando kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa ilhali anacheza vizuri kwenye La Liga.
Kwenye mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2017, James aliwekwa nje ya kikosi cha Real Madrid dhidi ya Juventus. Hakuwa kwenye benchi, badala yake alituowa jukwaani hali ambayo ilimuumiza mchezaji huyo.
5. MALENGO
Takwimu zinaonesha kuwa hii ni mara ya tatu kwa kocha Carlo Ancelotti kumsjaili James Rodriguez akiwa katika timu tatu tofauti. Kwanza alimsajili James akiwa kocha wa Real Madrid mwaka 2014. Pili alipokuwa kocha wa Bayern Munich alimsajili James kwa mkopo wa misimu miwili. Tatu, sasa ni kocha wa Everton amemsajili James kwa mara nyingine tena.
Wakati akiinoa Napoli, alifanya jaribio la kumsajili James ingawa hakufanikiwa. Kwa upande wa Zidane hakuwa na malengo ya kumbakiza James kikosini mwake. Hii ina maana makocha hao wana malengo tofauti linapokuja jina la James Rodriguez.
Bila shaka sasa tutamshuhudia James akiwa kwenye kiwango bora na kuthibitisha kuwa alipokuwa Real Madrid hakupewa nafasi ya kutosha, lakini sasa yuko Everton na amepewa nafasi anayopenda kucheza, bila shaka watanufaika naye. Ni muda tu utaongea iwapo Ancelotti, James na Zidane nani alikuwa sahihi kufanya maamuzi.
Comments
Loading…