in

TFF haitaki Simba kufundishwa na kocha MZAWA?

Simba

Wiki iliyopita kuna vitu viwili vilifanyika kwenye mpira wetu kiujumla. Baada ya Simba kufanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika , aliyekuwa kocha mkuu wa Simba, Sven Vandbroeck aliachana na Simba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu ya Simba, pande zote mbili. Upande wa Sven Vandbroeck na ule upande wa Simba ulikubaliana makubaliano ya pande mbili kusitisha mkataba.

Kitu cha pili ambacho kilitokea wiki iliyopita ni kutoka kwa orodha ya waamuzi ambao watachezesha katika michuano ya CHAN, michuano inayoanza mwezi huu .

Kwenye vitu vyote viwili nilivyovitaja hapo juu kuna kitu cha kujifikirisha kidogo, kitu chenyewe ni kwamba kwenye vitu vyote viwili hapo juu hakuna neno “MTANZANIA”.

Baada ya Simba kukubaliana kusitisha mkataba na Sven Vandbroeck hakuna “MTANZANIA” anayetajwa kuchukua nafasi ya kuwa kocha mkuu, na inawezekana hata Simba hawatamani kuwa na kocha mkuu ambaye ni “MTANZANIA”.

Kwenye suala la waamuzi watakaochezesha michuano ya CHAN hakuna jina la mwamuzi “MTANZANIA” ambaye atachezesha michuano hiyo ya CHAN.

Tuanzie hapa tafakari yetu. Ligi yetu inaonekana bora kwa sasa ukilinganisha na ligi nyingine za Afrika Mashariki. Pamoja na ligi hii kuonekana bora kuna vitu viwili muhimu ambavyo siyo bora.

Ubora wa ligi yetu ulitakiwa kwenda sambamba na ubora wa makocha wazawa pamoja na waamuzi wazawa, lakini hiki kitu kipo tofauti kabisa kwenye ligi yetu.

Tatizo liko wapi? Tatizo linaanzia wapi? Hapa ndipo mwanzo wa sisi kuanza kutafakari kwa pamoja. Ukiniuliza mimi tatizo liko wapi moja kwa moja nitakupa majibu ambayo yatagusa uongozi wa mpira wetu wa miguu uliokabidhiwa dhamana ya kuendesha mpira wetu.

Kwanini nasema hivo? Nchi hii bado mfumo wa upatikanaji wa waamuzi na makocha una siasa nyingi. Waamuzi wengi wazuri wanaachwa kwa sababu sio watu wetu na mfumo wa upatikanaji makocha bado ni mfumo wa kizamani sana.

Hata wakufunzi wanaotumika kuwafundisha makocha wetu ni wakufunzi wale wale na hawajifunzi kutokana na mabadiliko ya mpira wa kisasa.

Ndo maana Sven vandbroeck ameondoka lakini hakuna mtu hata mmoja anafikiria kuna kocha Mtanzania anaweza kupewa kazi pale Simba.

TFF haifanyi jitihada kubwa ya kushirikiana na mashirikisho mbalimbali ya mpira wa miguu kwenye nchi ambazo zimepiga hatua ili kuleta wakufunzi bora kuja kuwafundisha makocha wetu.

Makocha wetu wazawa nao hawana utamaduni wa kujiongeza kwenda kuongeza maarifa ya mpira wa miguu kwenye sehemu mbalimbali ambazo zimeendelea kisoka.

Marefa wanaopata nafasi ni wale ambao tupo nao kwenye mfumo ambao wanaweza kuchezesha mechi kwa maelekezo yetu na wasioweza kudai kipindi cha malimbikizo ya mishahara yao.

Binafsi sijawahi kusikia wakufunzi wa waamuzi kutoka nje  wamekuja hapa kuwapa mafunzo maalumu ya uamuzi  na kufundishana mabadiliko ya kisasa kwenye soka.

Mfumo wa upatikanaji wa waamuzi na makocha ni mfumo ambao mizizi yake inaanzia kwenye chaguzi za viongozi wa Shirikisho kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa. Inaenda inaunga kwenye namna tunavyopata makocha wetu na waamuzi.

Inaenda mbali kwamba mwamuzi unayejisimamia kwa kutokubali maelekezo hutopata games za kuchezesha.Jiulizie tu kwa muda wa miaka 3 sasa, kuna kocha gani wa Kitanzania ametoka kwenye kufanya mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi?

Waamuzi wetu lini wamepata mafunzo ya darasani toka kwa wataalamu?  Kuna watu nadhani ukiachana na ile mitihani ya mbio hawajawahi kufanya  wala semina tangu wameanza kuchezesha soka.

TFF inachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo mabovu ya makocha wetu na waamuzi wetu wazawa kwa kutokuleta wakufunzi bora kwa ajili ya kuwafundisha waamuzi na makocha wetu.

Leo hii Simba inatafuta kocha wa kuziba nafasi ya Sven Vandbroeck lakini kwa kiasi kikubwa matarajio ya wengi kocha huyo atatoka nje ya nchi. Hatokuwa “MTANZANIA”. Kama TFF wangeleta wakufunzi bora leo hii Simba ingeweza kufundishwa na kocha “MTANZANIA”.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Lionel Messi

Jihadharini na Barcelona ya Lionel Messi

Patrick Aussems

Natamani kocha wa Simba awe PATRICK AUSSEMS