Hapa ndipo tatizo linapoanzia kwake yeye mpaka sasa hivi Bernard Morrison anashiriki michuano miwili msimu huu. Mchuano wa kwanza ni ule ambao klabu yake ya Simba SC inashiriki.
Simba SC mpaka sasa hivi inashiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, ligi kuu ya Tanzania bara na kombe la shirikisho. Michuano hii Bernard Morrison anatakiwa kushiriki kama mchezaji wa Simba SC ili aisaidie timu yake.
Kiwango chake kinahitajika sana kwenye michuano hii kwa ajili ya timu yake ya Simba SC kufika mbali. Kwenye michuano hii kinahitajika kipaji cha Bernard Morrison pamoja na utimamu wa akili ya Bernard Morrison.
Kipaji peke yake hakitoshi kwa mchezaji kufanya vyema ndani ya uwanja, kipaji cha mchezaji kinatakiwa kuunganishwa na utimamu wa akili yake ili kipaji kioneshe matokeo chanya.
Utimamu wa akili ya mchezaji yoyote duniani unapatikana kwa mchezaji huyo kuelekeza akili yake ndani ya uwanja tu ( uwanja wa mazoezi na uwanja wa kwenye mechi za mashindano).
Kitu chochote ambacho kinachokuja kutoka nje chenye mwelekeo wa kuharibu utimamu wa akili ya mchezaji kinatakiwa kiondolewe kwanza na mchezaji mwenyewe pili na viongozi wanaomzunguka mchezaji husika.
Bernard Morrison anacheza mashindano mengine ya nje ya uwanja. Mashindano ambayo siyo rafiki kwa kipaji chake. Mashinsano ambayo yana nafasi ya kudidimiza kiwango chake na siyo kukishamirisha kiwango chake.
Tangu aondoke katika klabu ya Yanga , Bernard Morrison amekuwa na ligi na mashabiki wa Yanga. Ligi ambayo inahusisha kurushiana maneno kati ya pande zote mbili yani upande wa Bernard Morrison na upande wa mashabiki wa Yanga.
Ligi hii ilisababisha kwa kiwango kikubwa Bernard Morrison kupunguzwa kasi ya kiwango chake kwa sababu yeye aliwekeza kushindana nje ya uwanja na siyo ndani ya uwanja.
Tatizo ukishindana nje ya uwanja na mashabiki , watu ambao watanufaika ni mashabiki na siyo mchezaji. Shabiki silaha yake ni mdomo na mchezaji silaha yake kubwa ni mguu wake.
Kwa hiyo shabiki atamlazimisha mchezaji atumie mdomo wake na ausahau mguu wake anaoutumia uwanjani. Shabiki hana cha kupoteza, yeye atakuchokoza kwa sababu ni kazi yake na yeye atakufanya usahau kazi yako ili ushindane naye .
Wakati ambao unashindana naye ndiyo wakati ambao majukumu yako ndani ya uwanja unapoyasahau. Hata ukiingia uwanjani kucheza utacheza kwa hasira ya kutamani kuwakomesha mashabiki ambao anashindana nao nje ya uwanja.
Ukicheza kwa nia ya kuwakomesha lazima upanie mechi husika. Kupania kunasababisha mchezaji husika kutokuwa na ufanisi ndani ya uwanja kwenye baadhi ya maamuzi yake ndani ya uwanja.
Hiki ndicho kitu ambacho Bernard Morrison alikuwa nacho kwa muda mrefu tangu atoke Yanga na kwenda Simba. Anashindana sana na mashabiki wa Yanga kuliko kucheza uwanjani.
Mechi ya jana ilikuwa mechi bora kwake tangu atue Simba. Alihusika katika magoli matatu (3) moja (1) akisababisha na mawili(2) akifayangua yeye mwenyewe kwa mguu wake.
Kama Bernard Morrison akitulia ndani ya uwanja na kuachana na mashindano ya nje ya uwanja. Mashindano ambayo hayana faida kwake kwa kiasi kikubwa ataisaidia sana Simba SC kwenye michuano ambayo inashiriki.
Comments
Loading…