Makocha hawa ni Albert Sokaitis na Jocquis L. Sconiers
Kwa niaba ya Shirikisho la mpira wa kikapu nchini (TBF) nina furaha kuwatangazia kuwa Tanzania tumefanikiwa kupata kocha wa taifa wa kikapu kutoka Marekani (atakuwa na msaidizi wake). Makocha hawa watakuwa na majukumu ya kufundisha timu zetu zote za Taifa (wanawake na wanaume) na pia kufundisha makocha wetu wazalendo na pia Kocha huyu mkuu ndio atakuwa mshauri mkuu wa kiufundi kwa TBF.
Makocha hawa ni Albert Sokaitis (Kocha Mkuu) ambaye ni Kocha mwenye uzoefu wa miaka 24 kwa sasa ni Kocha Mkuu wa timu ya Chuo Kikuu cha Post huko huko Marekani katika jimbo la Connecticut. Pia amewahi kufundisha timu na kuendesha mafunzo nchi za Uchina, Lebanon, Ugiriki na Japan.
Kocha Sokaitis atasaidiwa na Kocha Jocquis L. Sconiers ambaye nae ana uzoefu wa miaka mingi na kwa sasa ni Kocha Mkuu Msaidizi wa timu ya Chuo Kikuu cha Post huko Marekani katika jimbo la Connecticut.
Walimu wote hawa wana shahada za juu kutoka vyuo vikuu mbali mbali vya Marekani na wanatarajiwa kuwasili nchini tarehe 21/09/2012 na kuanza mafunzo rasmi kwa timu zetu zote 2 tarehe 22/09/2012.
Pia TBF imewateuwa Makocha wasaidizi wazalendo 4 watakofanya kazi na walimu hawa wa kigeni, makocha wazalendo ni Everist J. Mapunda (kutoka klabu ya Pazi.), Leonard V. Kwale (kutoka klabu ya ABC), Agnella R. Semwaiko (kutoka klabu ya Don Bosco Lioness) na Bahati Mgunda (kutoka klabu ya Vijana). Makocha hawa watatangaza vikosi vya timu za taifa za wanawake na wanaume mapema juma lijalo.
2. Mpango wa Muda wa Kati kuinua Viwango vya mchezo wa Kikapu Tanzania:
TBF imeandaa mpango wa muda wa kati utakaotuwezesha kuinua viwango vya mchezo huu nchini. Mpango huu utajumuisha utoaji wa mafunzo ya kutosha kwa makocha wazalendo nchi nzima na pia kutambua vipaji na kuweka mpango wa kuviendeleza. Mpango huu ambao kwa sehemu kubwa utatekelezwa na makocha wa kigeni kutoka Marekani watakaowasili hivi karibuni ni sehemu ya mkakati wetu wa kuinua mchezo wa kikapu kiufundi ikiwa ni mwanzo wa maandalizi yetu ya mipango yetu ya baadae ya kushiriki michuano mikubwa ya kimkoa (Regional) Afrika na duniani.
Mpango huu maalum wa kuinua kiwango cha mchezo wa kikapu nchini utasimamiwa na TBF lakini utagharamiwa na wadau na wafadhili mbalimbali pamoja na Serikali ya Tanzania. Tunachukua fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya M. Kikwete kwa msaada na mchango wake mkubwa katika kuendeleza michezo kwa ujumla na hususani mchezo wa mpira wa kikapu.
Wakati tunasubiri uamuzi wa Serikali kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Mhe. Rais ya kulipia gharama za walimu wa kigeni sisi TBF tunatoa wito kwa wadau wengine wajitokeze kwa wingi kumuunga mkono Rais wetu kutusaidia katika kufanikisha programme hii ambapo kuna mahitaji mengi ikiwa ni pamoja na gharama za kambi ya timu, vifaa, usafiri wa wachezaji n.k.
Hiyo basi, tunapenda kuwashukuru kwa namna ya pekee ndugu zetu watu wa Marekani kupitia ubalozi wao hapa Tanzania kwa kuwa wa kwanza kuunga mkono juhudi za Rais ambapo wametusaidia kulipia baadhi ya gharama za awali za mpango huu zitakawezesha walimu hao kuja nchini na kuanza mafunzo.
Tunaomba wadau wengine wawaunge mkono.
3. Tanzania kuwa Mwenyeji wa Michuano ya Kanda ya 5 FIBA:
Nachukua nafasi hii kuutangazia umma kuwa baada ya mafaniko mazuri ya kuandaa michuano ya klabu bingwa ya kikapu kanda ya 5 mwaka huu Tanzania tumekubaliwa kuwa wenyeji wa michuano mikubwa ya Kanda ya 5 ya FIBA ya timu za Taifa, michuano hii ni mikubwa sana na inatarajiwa kushirikisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Somalia, Djibouti, Sudan na Sudani ya kusini.
Mashindano haya yanayotarajiwa kufanyika hapa Dar Es Salaam mwezi December, 2012.
Tunaomba wadau wote tuunge mkono kwa hali na mali kufanikisha malengo yetu ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu kwa faida ya vijana wetu na Taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania
PHARES MAGESA MAKAMU WA RAIS-TBF
Comments
Loading…