in

Takwimu za Simba zinatisha

SIMBA SC

MABINGWA wa soka nchini Tanzania wamedhihirisha kuwa wamepania kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, au hata kucheza kwa mafanikio makubwa zaidi katika mashindano ya ngazi za vilabu barani Afrika. 

Ushindi wao mabao 4-1 dhidi ya AS Vita ya DR Congo waliopata wikiendi hii umeonesha namna Simba walivyo na njaa ya ushindi, huku wakiwa klabu kutoka Tanzania inayojiandikia rekodi ya kipekee kwenye mashindano ya soka ngazi ya klabu barani Afrika.

Ushindi wa Simba dhidi ya AS Vita ulikuja katika wakati mtamu zaidi baada ya kushuhudia soka maridadi kutoka kwa vijana hao wa mitaa ya Msimbazi jijini Dar es salaam, hali ambayo iliwalazimu mashabiki wake kusukuma gari la mwekezaji wa timu hiyo Mohammed Dewji wakati akiondoka kwenye milango ya uwanja wa Benjamin Mkapa. 

Tanzania Sports
Heka heka uwanjani

Simba waliwatawala AS Vita kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za wageni hao. Simba walipata kona 3, wakati AS Vita walipata kona 3. Simba walifanya madhambi mara 24, wakati AS Vita walifanya hivyo mara 17. Simba waliotea mara 2 kwenye lango la wageni wao wakati AS Vita waliotea mara 1.

Simba walipiga mashuti 18 ambayo kati yake 7 yalilenga lango. AS Viya walipiga mashuti 11 kuelekea lango la Simba lakini yale yaliyolenga lango ni mashuti matatu. Kwa hakika ulikuwa mchezo maridadi na wenye kila aina ya ufundi.

Takwimu za Shirikisho la soka barani Afrika CAF zimeonesha kuwa Simba inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 13 kati ya vilabu 16 vilivyoshiriki mashindano ya kimataifa msimu huu. Timu zote 16 zimetoka kwenye makundi zikiwa zimecheza mechi tano. 

Simba wamejikusanyia pointi 13 kutoka Kundi A walimopangwa na Al Ahly,AS Vita na El Merreikh. Simba wamebakiwa na mchezo mmoja mkononi ambao watacheza nchini Misri dhidi ya washindi wa pili wa kundi hilo na mabingwa watetezi wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly. 

Katika kundi A mechi zilizobakia ni kati ya bingwa mtetezi Al Ahly dhidi ya Simba na wenyeji AS Vita watawakaribisha El Merreikh ya Sudan. Katika mchezowa mwisho Simba na Al Ahly haitakuwa mechi ya kuamua kinara wa kundi A kwa sababu hakuna timu nyingine yenye uwezo wa kuzifikia pointi za Simba. Hata Al Ahly ikifanikiwa kumchapa Simba itaishia kuwa na pointi 10 pekee na kuendelea kushika nafasi ya pili.

Vinara wa ubora katika msimamo wa CAF kwa timu 16 ni Mamelodi Sundowsn ya Afrika kusini. Mamelodi wana pointi sawa na Simba, wakiwa wamecheza mechi 5, wameshinda mechi 4, kutoka sare mchezo mmoja na hawajafungwa. Pia wamepachika mabao 10 katika mechi hizo tano na kufungwa mabao mawili. 

Simba wamecheza mechi tano, wameshinda mechi 4, wametoka sare mechi moja dhidi ya El Merreikh, hawajafungwa mchezo wowote na wamepachika wavuni mabao 9. Mchezo wa kwanza dhidi ya AS Vita nchini DR Congo walishinda 1-0. Mchezo wa pili dhidi ya Al Ahly walishinda bao 1-0. Mchezo wa tatu walitoka suluhu 0-0 dhidi ya El Merreikh. Mchezo wan ne waliizaba El Merreikh mabao 3-0 kabla ya kuwazaba AS Vita mabao 4-1.

Katika mechi tano walizocheza Simba wameruhusu nyavu zao kutikiswa mara moja tu dhidi ya AS Vita. Ni kwamba AS Vita ndiyo timu ya kwanza kuziona nyavu za Simba katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. Hiyo ni rekodi ya aina yake.

Wakicheza kwa masharti ya CAF kuingia na mashabiki wachache Simba walionesha kwanini wanastahili kuongoza kundi A, na kwmaba kwanini walimchapa bingwa mtetezi Al Ahly. 

Tanzania Sports
Simba wakishangilia goli..

Takwimu za CAF zinaonesha kuwa timu ya tatu ni Waydad Casablanca na kufutiwa na zingine Esperance,A Ahly, Horoya,MC Alger,Kaizer Chiefs, CR Belouizdad,Zamalek,Teugheth,A Hilal,AS Vita,TP Mazembe,Al Merreikh na Petro De Luanda. 

Matokeo ya Simba kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kunawezesha Tanzania kuwa na wawakilishi wanne kwenye mashindano ya ngazi za Klabu kuanzia msimu ujao 2021/2022. Faida ya mafanikio ya Simba na Namungo kutinga hatua ya makundi zimeongeza pointi ya ushiriki wa timu za Tanzania.

Aidha, Simba wameonesha namna usajili wao wa wachezaji wa kimataifa unayolipa. Vipaji vya kigeni Lus Miquissone (Msumbiji), Cletous Chama (Zambia), Larry Bwalya (Zambia), Joash Onyango (Kenya),Pascal Wawa (Ivory Coast), Taddro Lwanga(Uganda), Meddie Kagere (Rwanda),Chriss Mugalu (DR Congo) na Francis Kahata(Kenya) wakiwa wamekipiga vema katika mechi dhidi ya AS Vita. 

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Taifa Stars

Soka Afrika Mashariki limerudi gizani

Rashid Juma

MWELEKEO WA RASHID JUMA NI UPI?