in , , ,

Yanga Walifeli Kwenye Usajili au Benchi la Ufundi?

Klabu ya Yanga moja ya vigogo wa soka nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki imekuwa katika mijadala katika vijiwe mbalimbali vya soka hapa Tanzania na kwenye mitandao ya kijamii kutokana na matokeo mfululizo ambayo hayajafikia matarajio ya mashabiki wake. Swali kubwa linalozungumzwa ni kama tatizo lipo kwenye usajili wa wachezaji au benchi la ufundi ambalo lina jukumu la kusimamia na kuboresha kiwango cha timu.

Yanga walifanikiwa kufanya usajili mkubwa msimu huu, wakiongeza wachezaji wenye majina makubwa kutoka ndani na nje ya Afrika. Wachezaji kama Clatous Chama , Jean Baleke , Duke Abuya na Prince Dube walikuwa kati ya wale waliotarajiwa kuongeza ubora wa timu. Pia, klabu ilijipanga kuhakikisha inasalia na nyota wake wa msimu uliopita waliokuwa muhimu kama Aziz Ki, Farid Musa , Bakari Mwamnyeto na Djigui Diarra.

Licha ya juhudi hizi, bado kuna maswali kuhusu ubora wa usajili huu. Baadhi ya wachezaji waliosajiliwa hawajafikia viwango vilivyotarajiwa. Mfano mzuri ni baadhi ya wageni walioonekana kutokuwa na athari kubwa wanapopewa nafasi. Mashabiki wanaamini kwamba fedha nyingi zilitumika bila kufanya tathmini ya kina juu ya mahitaji halisi ya timu. Je, ni suala la usajili wa wachezaji wasioendana na mfumo wa timu, au ni wachezaji wenye uwezo wa kawaida?

Pia, kuna dhana kwamba baadhi ya nafasi muhimu hazikuzingatiwa kikamilifu. Yanga walihitaji kuongeza nguvu zaidi katika safu ya ulinzi na kiungo wa kuzuia, lakini mapungufu yameendelea kuonekana katika maeneo haya.

Kabla ya kutimuliwa aliyekua kocha mkuu wa Yanga, Miguel Ángel Gamondi alikuwa akishutumiwa kwa kushindwa kutumia kikamilifu wachezaji waliopo na kwa kushindwa kubadilika pindi mambo yanapokwenda vibaya. Licha ya kuwa na kikosi chenye vipaji, mwitikio wa mbinu zake katika baadhi ya mechi haujawa wa kuridhisha.

Tatizo la Yanga linaweza kuwa si usajili pekee, bali pia namna benchi la ufundi linavyotumia kikosi. Mashabiki wanalalamika kuwa timu haioneshi mabadiliko mazuri katika uwanja, hasa inapokutana na timu ngumu au pale inapohitaji kurekebisha matokeo. Mfumo wa uchezaji wa Yanga umekuwa ukionekana kutegemea wachezaji wachache badala ya kufanya kazi kama timu nzima.

Tanzania Sports

Aidha, kumekuwa na madai kwamba benchi la ufundi halijawa na mpango thabiti wa muda mrefu wa kuimarisha timu. Kukosekana kwa mkakati wa maendeleo ya wachezaji vijana ndani ya kikosi na utegemezi wa wachezaji wa kigeni kumeongeza changamoto kwa timu hiyo.

Kama klabu, Yanga wanapaswa kutathmini suala la kubadilisha Kocha wakati mgumu kama huu ambao wameenda katika hatua ya makundi ya ligi ya Mabingwa Afrika . Ni dhahiri kwamba changamoto zinazowakumba ni mchanganyiko wa masuala ya usajili na benchi la ufundi pamoja na utawala Kwa ujumla. Wakati wachezaji bora waliosajiliwa wanatarajiwa kuleta mafanikio, wanahitaji pia kufundishwa na kuwekwa kwenye mifumo inayolingana na uwezo wao. Bila usajili mzuri, benchi la ufundi halitakuwa na nyenzo bora za kufanikisha malengo lakini bila mbinu nzuri za ukufunzi hata wachezaji bora hawawezi kufikia viwango vinavyotakiwa.

Kwa Yanga, kujifunza kutokana na makosa ya msimu huu ni hatua ya kwanza. Wanahitaji kuimarisha kitengo cha usajili ili kuhakikisha wanapata wachezaji sahihi wanaolingana na mahitaji ya timu. Vilevile, benchi la ufundi linapaswa kuonyesha uwezo wa kubadili hali dimbani, kuimarisha mifumo ya uchezaji, na kuhakikisha kila mchezaji anatoa mchango wake.

Ikiwa Yanga wataweza kutatua changamoto hizi kwa uwiano mzuri, watarejea kuwa timu yenye ushindani mkubwa si tu katika ligi ya ndani, bali pia katika michuano ya kimataifa. Mashabiki wanahitaji kuona juhudi na mabadiliko haya haraka. Sasa ni wakati wa viongozi wa klabu kujitathmini kwa kina kwani mashabiki wanastahili zaidi ya Kile ambacho wamezoea kukiona wakati wote.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

20 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Jinsi kocha wa Yanga alivyoaibishwa kimbinu

Tanzania Sports

Matano yanayomkabili Kylian Mbappe