in , , ,

STARS v. ALGERIA: TUJITUME DAKIKA TISINI

 

 

Kesho Jumamosi Taifa Stars itakipiga dhidi ya Algeria kwenye mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Urusi 2018. Mchezo huu utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam.

Kwa mujibu wa viwango vya sasa vya ubora vya FIFA vilivyoachiwa tarehe 5 mwezi huu Algeria  ni timu namba mbili kwa ubora Afrika. Timu hiyo iliyowahi kushiriki Kombe la Dunia mara nne ipo kwenye nafasi ya 26 nafasi mbili nyuma ya Ufaransa.

Mabingwa wa Dunia Ujerumani walilazimika kusubiri dakika 30 za nyongeza kuweza kuwaondosha Mashujaa hawa wa Jangwani kwenye mchezo wa hatua za 16 bora huko Brazil uliopigwa Juni 30 mwaka jana. Haya yote yanaonyesha ubora walio nao Algeria.

Tukiachilia mbali nafasi waliopo Algeria kwenye viwango vya ubora vya FIFA na matokeo yao ya michezo ya karibuni, wachezaji wanaounda kikosi cha Algeria wanatosha kabisa kutupa tahadhari wanapolinganishwa na wachezaji waliopo kwenye kikosi cha timu yetu.

Uwepo wa wachezaji kama Yacine Brahimi wa FC Porto ya Ureno, Sofiane Feghouli wa Valencia ya Hispania, Ryad Mahrez wa Leicester City ya England, Islam Slimani wa Sporting Lisbon ya Ureno na wengine kwenye safu ya ushambuliaji unaonyesha kuwa wao ni timu tishio.

Advertisement
Advertisement

Hata unapoitazama safu yao ya kiungo inayoundwa na wachezaji kama Saphir Taider wa Bologna ya Italia, Walid Mesloub wa Lorient ya Ufaransa, Ryad Boudebouz wa Montpellier ya Ufaransa, Nabil Bentaleb wa Tottenham ya England na viungo wengine utangundua kuwa Algeria si timu ya mzaha hata kidogo.

Safu yao ya ulinzi pia si ya mchezo. Hapo unakutana na walinzi kama Aissa Mandi wa Reims ya Ufaransa, Carl Medjani wa Trabzonspor ya Uturuki, Mehdi Zeffane wa Rennes ya Ufaransa na walinzi wengine hodari.

Kikosi chao cha wachezaji 25 ambacho mtandao fulani wa Algeria umedai kuwa ndicho kilichochaguliwa kuja Dar-es-salaam kina takriban wachezaji 20 wanaocheza soka lao kwenye klabu za Ulaya wakiongozwa na Ryad Mahrez ambaye amekuwa gumzo kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu.

Ni dhahiri kuwa kikosi cha timu yetu ta Taifa ambacho hakina hata mchezaji mmoja anayecheza soka barani Ulaya ni kikosi dhaifu kinapolinganishwa na kikosi cha Algeria. Kwenye kikosi cha Stars ni Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngasa pekee wanaocheza soka nje ya Tanzania lakini hakuna kati yao anayecheza barani Ulaya.

Tukiwa tushajua kwamba tunakutana na kikosi bora zaidi ya kikosi cha timu yetu, nini cha kufanya ili tuweze kupata matokeo kwenye mchezo wa kesho? Jibu la swali hili ni rahisi mno.

Kinachotakiwa kufanyika hapo kesho ni kujituma dakika tisini. Tunatakiwa tuutumie vizuri uwanja wetu wa nyumbani na tuibuke na ushindi kwenye mchezo wa kesho ili tujiweke kwenye nafasi nzuri ya kuwaondosha Algeria.

Wachezaji wetu wanatakiwa kuwa tayari kupigana kwa nguvu na akili kwenye dakika zote tisisni za mchezo. Kujituma kwa bidii ndani ya uwanja ndio silaha kubwa zaidi kwenye mchezo wa soka inayoweza kuiwezesha timu dhaifu kuifunga timu bora zaidi.

Kwa vyovote vile kikosi chetu kitahitaji kuelekeza nguvu zaidi kwenye ulinzi ili kuwazuia Algeria wasipate bao lolote hapo kesho na pia tuweze kuzitumia vizuri nafasi za kufunga mabao tutakazozipata. Mwalimu Mkwasa ndiye anayejua zaidi katika hili. Haya yanawezekana iwapo tu wachezaji wetu watajituma.

Kujituma kusiishie tu kwa wachezaji. Washabiki pia tuujaze kwa wingi Uwanja wa Taifa na tujitume dakika zote tisini kwa kushangilia ili kuihamasisha timu yetu na kuitia nguvu. Haya yakifanyika tutaweza kuifunga timu bora hapo kesho.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Blatter alazwa hospitali

Tanzania Sports

FIFA waanza kukata…