Mazoea ya soka la Bongo ni kuona timu za Simba na Yanga zinashinda kila mechi. Mazoea hayo yapo kwa mashabiki, viongozi na baadhi ya wadau wanaoamini kuwa timu hizo hazipaswi kufungwa katika mfululizo wa mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara.
INGEKUWAJE SIMBA WANGEKUWA AL AHLY?
Hivi karibuni kiongozi mmoja wa klabu ya Simba alizungumza kwenye redio moja maarufu nchini Tanzania akidai kuwa kwa usajili waliofanya mabingwa watetezi Simba hawakutakiwa kufungwa na timu kama Tanzania Prisons na JKT Ruvu.
Kauli hiyo inamaana kuwa Simba haitakiwi kufungwa mchezo wowote, ni sawa na Simba ilivyowahi kuifunga A Ahly ya Misri ambayo ilikuwa na mchezaji mwenye dau kubwa lenye uwezo wa kusajili kikosi chote cha Simba.
Kwa kauli ya kiongozi huyo ana maana hata Simba haikustahili kuwafunga A Ahly kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa vile mabingwa hao wa Misri wamekuwa na usajili wa nguvu.
Hali hiyo si kwa Simba peke yao, hata upande wa Yanga viongozi wao,mashabiki na wadau wao wanaamini kuwa haitakiwi kufungwa na timu kama Mwadui, Biashara au Lipuli kwa vile nao wanakuwa na usajili wa nguvu.
Mara nyingi yamezungumzwa hayo kwenye vijiwe vya kahawa lakini sasa yanaonekana wazi kutamkwa na viongozi kana kwamba timu zingine zinakuwa hazijasajili wala kujiandaa kwa ushindani wa Ligi.
VIPI SIMBA NA YANGA WANGEKUWA BARCELONA?
Msimu uliopita dunia ilishuhudia mchezaji bora wa dunia na wa kipekee aliyeshinda tuzo sita za ugwiji wa soka, Lionel Messi alikuwa sehemu ya kikosi cha Barcelona kilichochakazwa kwa mabao 8-2 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Barcelona walipokea kipigo hicho kutoka kwa Bayern Munich ambao walifanikiwa kutwaa taji hilo. Barcelona wanakumbuka kutandikwa mabao 4-0 ndani ya dimba la Anfield na Liverpool ambao walikua kuwa mabingwa wa Ulaya.
Barca walifungwa mabao hayo licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3- 0 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nyumbani kwao Camp Nou. Barca licha ya kuwa na mchezaji bora dunia, lakini Messi hakuzuia kipigo cha timu yake na wala hatukusikia kuwa hawakustahili kufungwa nao.
Kwamba Barcelona waliona kipigo hicho ni ujumhe wa kawaida kwenye mchezo wa soka ambapo kila timu inakuwa imejiandaa na hivyo walizidiwa maarifa pamoja na kutakiwa kujipanga upya.
Kwenye mchezo wa El Clasico Barcelona wakiwa nyumbani walipigwa mabao 3-1 wakiwa na Lionel Messi. Kwenye Ligi Kuu Hispania si jambo la ajabu kuona Barcelona wakipokea vichapo kutoka kwa wengine.
KAMA SIMBA NA YANGA ZINGEKUWA REAL MADRID
Klabu ya Cadiz ni ndogo mno katika historia ya soka Hispania. Lakini msimu huu imewashangaza maelfu ya washabiki wa soka baada ya kuikung’kuta Real Madrid bao 1-0.
Bajeti za Real Madrid na Cadiz ni mbingu na radhi, hazifanani hata kidogo. Lakini hilo halikuzuia Real Madrid kuzabwa kwenye La Liga. Kwenye historia ya soka Real Madrid iliwahi kuzabwa mabao 6-2 na Barcelona na maisha yakaendelea.
Vipigo vya aina yake vimetokea mara nyingi kwenye uwanja wa nyumbani wa Real Madrid wa Santiago Bernabeu. Hilo limekuwa sehemu ya mchezo kwani wachezaji wote wana miguu miwili na tofauti zao za kiuchumi na uwezo bado haziwezi kuandaa matokeo ya mchezo.
YANGA,SIMBA WANGEKUWA ARSENAL?
Kipigo cha mabao 8-2 kimewahi kuwakumba Arsenal kutoka kwa Manchester United. Kilikuwa kipigo cha aina yake kwenye EPL miaka kadhaa iliyopita, lakini Arsenal walifahamu ni sehemu ya mchezo, na wanalazimika kukubali kujirekebusha pale wanapokuwa wamezidiwa maarifa au uwezo wa timu hizo. Vipi Yanga wangekuwa Arsenal waliozabwa mabao 8-2? Ingekuwaje Simba ndio waliofungwa 8-2?
Je viongozi wa soka wa Yanga na Simba wanataka kutudhihirishia kuwa wachezaji wa timu zao wana miguu mitatu? Kwa,mba wanatakiwa kushinda karibu kila mechi wala hawana nafasi ya kufikiri kuwa kuna kuzidiwa kwenye mchezo wa kandanda?
Viongozi wetu wawe chachu ya maarifa kwa mashabiki ili wajifunze mpira katika hali halisi na ambayo itrapunguza presha na kudhani kuwa Simba na Yanga ni timu pekee duniani ambazo zinatakiwa kushinda kila mchezo.
Na zaidi wachezaji wao hawana miguu mitatu na kwamba watafanya maajabu kuliko wengine duniani. Kina Cristiano Ronaldo, Messi wana miguu miwili iliyotamba duniani kwa miaka 15 mfululizo lakini wameshuhudia vipigo katika timu zao.
Pep Guardiola pamoja na sifa lukuki alizonazo amewahi kutandikwa mabao 5 katika mchezo mmoja. Ni jambo la kawaida, kwa vile wachezaji wake wana miguu miwili tu. Hivyo basi wachezaji wa Simba au Yanga ni binadamu kama wengine.
Comments
Loading…