in

Simba kutangaza ufalme wa soka Afrika?

SIMBA SC

Nimetazama mara kwa nyingine mechi tatu za Simba dhidi ya AlAhly kwenye uwanja wa Mkapa, AS Vita jijini Kinshasa na Al Ahly jijini Cairo, nimeona ujumbe mzito wanaotuma mabingwa wa Ligi kuu Tanzania Bara kwa vigogo,wadau, na mashabiki wa soka kwa ujumla wake.

Kwenye mechi dhidi ya El Merreikh ilitarajiwa Simba wangeibuka na ushindi mnono jijini Dar es salaam. Lakini kwenye mechi dhidi ya AS Vita jijini Kinshasa ambako Simba walishinda 1-0 yalikuwa matokeo ya kushangaza. Kwenye mchezo wao wa pili dhidi ya A Ahly jijini Dar es salaam ambako walishinda bao 1-0 kila kitu kipo wazi kuwa Simba wanacheza mpira mzuri kuliko wapinzani wake.

Baada ya kichapo walichopata Al Ahly jijini Dar es salaam nilisoma mahali maoni ya mkongwe wa klabu hiyo na nahodha wao Wael Gomaa akilalamikia uwezo wa kocha Pitso Mosimane. Gomaa nimemtaza wakati akiwa mchezaji wa Al Ahly na timu ya taifa, lakini alichozungumza kilikuwa kitu tofauti na nyakati tofauti.

Kwanza, uamuzi wa Al Ahly kumchukua Pitso Mosimane ni wazi ulitokana na kuona mabadiliko ya kandanda na uwezo wa kocha huyo. Pitso amekuwa kocha mwenye uwezo wa kufundisha kandanda safi, lakini Wael Gomaa na wenzake wanaofanana nao mawazo wanataka tuamini kuwa timu za kiarabu zitaendelea na mchezo wao wa kasi pasipo kuwa na uwezo mkubwa wa kutawala mchezo.

Al Ahly ya  Pitso Mosimane inalazimishwa kuchezea mpira kama wanavyofanya Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini. Huko ndiko alikotokea Pitson Mosimane.

Pili, Gomaa hakuzingatia ukweli kuwa Simba walicheza mpira mzuri na waliwashinda Al Ahly kimbinu na hata namna ya kucheza kitimu. Pia Simba walicheza mchezo huo wakiwa na moto baada ya kuwashinda AS Vita.

Tatu, Simba walikuwa nyumbani ni kama motisha kwao. Ni kama ambavyo Al Ahly walivyokuwa jijini Cairo dhidi ya Simba lakini nao wakaibuka na ushindi wa bao 1-0 kama ule wa Simba.

Hapo ndipo utaona mdomo na fkra za Wael Gomaa zilitakiwa kunyamaza. Lilikuwa suala la uwezo wa Simba katika kandanda, wanacheza vizuri, wachezaji wana uzoefu, wanahimili presha na wana kikosi kinachotoa ufundi tofauti.

kwa mantiki hiyo utaona Simba ni timu inayojijenga na kuwa tayari kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa. Swali moja linalobaki ni je Simba wapo tayari kutawala soka la Afrika kwa muda mrefu? Hili majibu watayatoa Simba katika michezo ijayo ya robo fainali.

Hadi sasa takwimu za Shirikisho la soka barani Afrika CAF zimeonesha kuwa Simba inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 13 kati ya vilabu 16 vilivyoshiriki mashindano ya kimataifa msimu huu. Timu zote 16 zimetoka kwenye makundi zikiwa zimecheza mechi 6.

Simba wamejikusanyia pointi 13 kutoka Kundi A walimopangwa na Al Ahly, AS Vita na El Merreikh, huku mchezo wao wa mwisho dhidi ya washindi wa pili wa kundi hilo na mabingwa watetezi wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ulifanyika hivi karibuni.

Licha ya kufungwa bao 1-0 bado Simba haikuwa na sababu ya kuyumbishwa na kama mazoezi ya kujiandaa na mshindani wa robo fainali basi wameshafanya, huku wakiwa na mechi kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Turudi kwenye suala la kutawala soka. Shirikisho la Soka Afrika linatarajiwa kupanga mechi za mtoano ifikapo Aprili 30 mwaka huu. Timu 8 zilizotinga hatua ya robo fainali ni hizi; Simba (Tanzania),Al Ahly (Misri), Mamelodi Sundowns (Afrika kusini), Belouizad (Algeria), Wydad Casbalanca (Morocco), Kaizer Chiefs (Afrika kusini), Esperance (Tunisia) na MC Alger(Algeria).

Aprili 30 mwaka huu hapo ndipo Simba watajua wanakabiliana na mpinzani yupi kati ya hizi tatu kwenye hatua ya robo fainali; Belouizdad (Algeria),Kaizer Chiefs(Afrika kusini),MC Alger(Algeria).

MC Alger wametoka kundi D wakiwa na pointi 9 na kushika nafasi ya pili, ambako kinara wao ni Esperance wenye pointi 13 sawa na Simba. Kwa vinara wa makundi hawapangwi kukutana, hivyo Simba itakuwa na uwezekano wa kuchuana na MC Alger.

Kaize Chiefs imetoka kundi C wakiwa na pointi 9 kati ya mechi 6 na kushika nafasi ya pili, huku kinara wao akiwa ni Wydad Casablanca ya Morocco. Hii ina maana Wazulu hawa wanayo nafasi ya kupangwa kuchuana na Simba katika robo fainali.

Belouizad ya Algeria imetoka kundi B ikiwa na pointi 9 kutokana na mechi 6, huku kinara wao akiwa ni Mamelodi Sundwons waliokusanya pointi 13. Hii ina maana upo uwezekano Simba kukutana na mshindi wa pili wa kundi B.

Timu zote zinazofuzu hatua hiyo zina uwezo mzuri na zina tofauti zake katika kandanda. Timu zilizoongoza makundi ni kali zaidi, mfano Mamelodi Sundwons, Esperance,Wydad Casbalanca na Simba.

Uzito wa timu hizo unatofautiana, lakini ukweli wa kiwango cha Simba msimu huu kinaoenaka wazi kuwatisha wapinzani wake. Bingwa mtetezi Al Ahly alipigwa Dar es salaam. AS Vita alitandikwa Dar es salaam,El Merreikh alipigwa nyingi Dar es salaam.

Hata kwenye hatua ya awali ya mchujo timu ya FC Plateaus ya Nigeria ilishindwa kutamba Dar es salaam baada ya kukubali kipigo nyumbani kwao.  Vilevile FC Platinum ya Zimbabwe ilifia Dar es salaam.

Kote walikopita Simba wanatuma ujumbe kuwa wamekuja kuwashika katika soka. Simba hawa si kwamba wanacheza soka la kutisha lakini wana msimu mzuri, wachezaji wazuri na benchi la ufundi limekuwa na wakati mzuri. Kwahiyo ikiwa Simba watavuka hatua ya robo fainali ni wazi watakuwa wametuma ujumbe mzito kwenye kandanda “wanataka kutawala soka Afrika

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
TP Mazembe

Nini kimewatokea TP Mazembe?

VAR ikitumika kwenye mechi ya Simba, Yanga

VAR ikitumika nini kitatokea Ligi Kuu Tanzania?