Timu ya Taifa ya Tanzania ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys, imefuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo.
Taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), imethibitisha hilo pasi shaka kwamba Tanzania ndiyo yenye nafasi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Aprili 2, mwaka huu huko Gabon baada ya Madagascar kuenguliwa kutokana na kutoandaa vema fainali hizo.
Taarifa hizo za CAF kutoka Libreville, nchini Gabon zinathibitisha kwamba Kamati ya Utendaji ya CAF imeipa ushindi Tanzania dhidi ya timu ya Jamhuri ya Congo ambayo katika michuano ya kufuzu, ilimchezesha mchezaji Langa Lesse Bercy aliyezidi umri kinyume cha kanuni za kanuni za michuano hiyo.
Serengeti Boys iliyosimamiwa na Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Rais Jamal Malinzi, sera kubwa ilikuwa ni kuangalia kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana, ilikusanywa na kuandaliwa kwa michezo mingi ya kimataifa ambako kwa mwaka moja tu 2016, ilicheza mechi zisizopungua 16 ya kimataifa.
Katika michezo hiyo ya kirafiki na ushindani, Serengeti Boys ilipoteza mchezo wa 16 tu dhidi ya Congo ilihali kulikuwa na rufaa kuhusu mmoja wa wachezaji wa Congo ambaye alionekana kuwa na umri mkubwa. Mchezaji huyo ni Langa Lesse Bercy.
CAF, kwa nyakati tofauti ikiwamo Novemba 10, 2016 na Desemba 15, mwaka jana walitoa agizo kwa Congo Brazzaville kumpeleka kijana huyo Cairo, Misri kwa ajili ya vipimo vya MRI ili kuthibitisha au kupangua madai ya Tanzania. Congo Brazzaville hawakupeleka.
Januari 12, mwaka huu 2017 iliamriwa kwa mara nyingine kijana huyo kupelekwa jijini Libreville, Gabon ili kufanyiwa vipimo vya MRI, lakini hakupelekwa na katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF, kimeamua kumaliza suala hilo na kuipa ushindi Tanzania.
Siku 10 ziliisha Januari 23, mwaka huu lakini tangu hapo kumekuwa na maswali ya kutosha kuhoji nafasi ya Tanzania yakitoka kwa Watanzania kupitia wanahabari, lakini TFF ilisimama kidete kutangaza kuwa tunasubiri uthibitisho wa CAF ambayo leo Februari 3, mwaka huu imetangaza rasmi kuwa Tanzania itacheza fainali hizo.