in , , ,

Real Madrid watwaa Super Cup

*Rooney nahodha mpya Manchester United
*Tata kocha mpya Argentina, Hoddle QPR

Cristiano Ronaldo amewaongoza Real Madrid kutwaa taji la Super Cup kwenye Uwanja wa Cardiff City, Wales.
Ronaldo alifunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya klabu wenzao wanaocheza La Liga nchini Hispania ya Sevilla, ambapo ilikuwa kurejea na kucheza nyumbani kwa mara ya kwanza kwa Gareth Bale.

Ronaldo ambaye pia ni mchezaji bora wa dunia, aling’ara sambamba na wachezaji wapya wa timu hiyo, James Rodriguez na Toni Kroos. Bale ndiye alimimina majalo iliyopokewa vyema na CR7 na kutikisa nyavu.

Mreno huyo alipachika bao la pili na la mwisho baada ya kufyatulia nyavuni mpira kutoka upande wa kushoto aliokuwa amechezeshwa na Mfaransa, Karim Benzema. Hili ni moja ya makombe sita ambayo Real Madrid wanashindania msimu huu.

Wanatetea ubingwa wa Ulaya walioupata kwa kuwafunga mabingwa wa Hispania, Atletico Madrid Mei mwaka huu, lakini pia wanataka kurejesha heshima nyumbani kwa kutwaa ubingwa wa La Liga, Copa del Rey, Kombe la Klabu la Fifa na Supercopa de Espana kwa msimu wa 2014-15.
 
ROONEY NAHOIDHA MPYA MAN UNITED

image

Manchester United wamemtangaza Wayne Rooney kuwa nahodha wao mpya, na kumaliza mvutano uliokuwapo baina ya Mwingereza huyo na Robin van Persie aliyekuwa anatarajia angepewa nafasi hiyo.

Rooney (28) anachukua nafasi ya Nemanja Vidic aliyehamia Inter Milan ya Italia baada ya mkataba wake kumalizika Old Trafford. Nahodha msaidizi anakuwa Darren Fletcher anayechukua nafasi ya Patrice Evra aliyekatisha mkataba mpya wa mwaka mmoja kwa kujiunga na Juventus pia ya Italia.

Rooney alishasema tangu awali alikuwa anataka nafasi hiyo, na jana alisema kwamba ni heshima kubwa kwake kupewa jukumu hilo, na anaona fahari na kumshukuru kocha kwa kumwamini.

Ametangazwa kuwa nahodha siku mbili tu baada ya Arsenal kumtangaza Mikel Arteta kuwa nahodha wao kuchukua nafasi ya Thomas Vermaelen aliyekwenda Barcelona huku Per Metersacker akiwa nahodha msaidizi kuchukua nafasi ya Arteta aliyepandishwa.
 
TATA KOCHA MPYA ARGENTINA

Katika tukio jingine, Gerardo Martino ‘Tata’ aliyeachia ngazi Barcelona majuzi, ameteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Argentina.

Tata anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Alejandro Sabella aliyeamua kuachia ngazi licha ya timu kufanya vizuri hadi kufika fainali ya Kombe la Dunia, ambapo walifungwa 1-0 na Ujerumani baada ya kutoana jasho kwa dakika 120.

Martino (51) ni chaguo tata kwa sababu chini yake Barca walikosa hata taji moja, ikiwa ni mara ya kwanza tangu msimu wa 2007/8. Tata amepata kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya Paraguay kati ya 2006 na 2011 akawafikisha robo fainali katika fainali za Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini.

Tata alichukua nafasi ya hayati Tito Vilanova wa Barcelona Julai mwaka jana, baada ya Vilanova kufariki dunia kwa maradhi ya saratani. Alikuwa na mkataba wa miaka miwili, lakini aliachia ngazi baada ya msimu mkavu wa vikombe.

Aliwasimamia Barca katika ushindi wa mechi 40 kati ya 59 walizocheza lakini akashindwa kuwapa kombe. Walitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya robo fainali walipofungwa na Atletico Madrid. Pia walifungwa na Real Madrid kwenye fainali ya Copa del Rey. Nafasi yake Barca imechukuliwa na kiungo wao wa zamani, Luis Enrique.
 
GLEN HODDLE ATUA QPR KUFUNDISHA

Katika hatua nyingine, Kocha wa zamani wa Timu ya Taifa ya England, Glen Hoddle ameteuliwa kuwa mwalimu wa timu ya kwanza ya Queen Park Rangers (QPR) iliyo chini ya Meneja Harry Redknapp.

Hoddle (56) ni Mwingereza ambaye amekuwa mchambuzi wa soka kwenye televisheni na pia amepata kuzifundisha timu za Swindon, Chelsea, Tottenham Hotspur na Southampton. Aliifundisha England kati ya 1996 na1999, na mara ya mwisho kufanya ukocha alikuwa Wolves, alikoondoka 2006.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arteta nahodha Arsenal

Man U na ‘mechi ya watoto’