*Chelsea wawakung’uta Aston Villa 8 – 0
*Man United waambulia sare Swansea
Wakicheza kwa tambo zilizokosekana tangu kuanza msimu huu, Chelsea wamepata ushindi wa kihistoria, baada ya kuwabandika Aston Villa mabao 8-0.
Kwa ushindi huo wamepanda hadi nafasi ya tatu, lakini wakiwa umbali wa pointi 12 kuwafikia Manchester United wanaoongoza ligi hiyo.
United wangeweza kutanua pengo la pointi na kuwa sita dhidi ya wanaoshika nafasi ya pili, Manchester City.
Hata hivyo, vijana hao wa Alex Ferguson walibanwa vilivyo huko Wales, walikocheza na Swansea na kuambulia sare ya bao 1-1.
United walitangulia kufunga kupitia beki Patrice Evra kwa kichwa, lakini bao hilo lilirudishwa na mchezaji mwenye makeke, Michu, aliyefunga baada ya kosa kosa nyingi.
Kocha wa muda wa Chelsea, Rafa Benitez amepokea ushindi huo mnono kwa furaha, akitamba ni mafunzo yake yaliyowabadilisha wachezaji.
“Unaona wazi sasa timu imeboreka, kwa jinsi hii tutajaribu kupunguza pengo kadiri itakavyowezekana. Siku zote ushindi ni kitu cha pekee, lakini kubwa ni kuona timu ikisonga mbele na kuwa nzuri.
“Kila siku mazoezini tunarekebisha vitu vidogo vidogo na vinaonekana wazi sasa. Wachezaji wanajituma hasa, wanajifunza, wanaelewa, wanajiamini na wanashinda.
“Iliyopo sasa ni kufanya ushindi huu uwe endelevu, tuendelee kushinda mechi zetu na hapo itakuwa rahisi kwangu kutuma ujumbe kote kote kwamba sisi ni washindani wa kweli,” akasema bosi huyo aliyeanza kazi mwezi uliopita.
Hakuacha kummwagia sifa Mhispania mwenzake, Fernando Torres aliyefunga bao lake la 13 msimu huu, ambaye ndiye alifungua karamu ya mabao leo.
“Kama mshambuliaji, alitakiwa kufunga mabao…timu inafanya vizuri, naye sasa ana nafasi zaidi na anajiamini kwa vile anafunga,” akasema.
Wakicheza nyumbani Stamford Bridge, Chelsea walipata bao dakika ya tatu tu, ambapo hadi mapumziko walishapachika matatu, kupitia kwa David Luiz na Branislav Ivanovic.
Kaimu nahodha, Frank Lampard alipata bao lake la 500 katika ligi kuu, kabla ya Ramires kufunga mawili kisha Oscar na Eden Hazard kumalizia shughuli.
Ushindi huu ulikuwa muhimu kwa Benitez, kwani ni wa kwanza nyumbani tangu alipoanza kazi, ambapo ilikuwa kawaida kuzomewa kila wakifanya vibaya.
Ushindi huu unafanana na waliopata Chelsea dhidi ya Wigan mwaka 2010, ambapo rekodi kubwa hadi sasa inashikiliwa na Manchester United waliowafunga Ipswich Town mabao 9-0 mwaka 1995.
United hao walipoteza nafasi nyingi za kufunga, hata alipoingia super sub, Chicharito, na jitihada za Robin van Persie hazikuzaa matunda yoyote, zaidi ya kuishia kuzozana na wachezaji wa timu pinzani na kuambulia kadi ya njano.
Ferguson anaomba nahodha wa Swansea, Ashley Williams afungiwe kwa muda mrefu, akidai angeweza kumuua RVP, kwa kumpiga na mpira kwa nguvu kichwani alipokuwa amelala chini.
Ferguson amemlalamikia mwamuzi Michael Oliver, huku akisema Swansea wana bahati, kwa sababu waliwapelekesha sana.
Comments
Loading…