in

Paralimpiki yadhihirisha uwezo wa walemavu

*Sherehe za ufungaji zafana, hotuba zakuna wadau

Dunia imedhihirisha kwamba wenye ulemavu wakiwezeshwa, wanaweza kufanya makubwa yasiyomithilika.
Wanaodhani kwamba wana miili iliyo kamili na kuwatazama wenye ulemavu kama wa daraja la pili, wamebaini kwamba mawazo yao ni potofu.
Moja ya maeneo ya kudhihirisha hilo, yalikuwa ni katika Michezo ya Paralimpiki iliyofungwa Jumapili usiku, na kuhitimisha rasmi Michezo ya 30 ya Olimpiki.
Kama ilivyokuwa kwa Olimpiki yenyewe, Paralimpiki ilifungwa kwa sherehe kubwa iliyofana, na kuhudhuriwa na watu mashuhuri katika sekta tofauti.
Ni kutokana na umuhimu wa wachezaji wa Paralimpiki, heshima yao na mchango wao kwa jamii na jumuiya ya kimataifa, jumla ya watu milioni 7.7 walitazama sherehe hizo.
Wenye ulemavu wenyewe walihitimisha kwa kuonesha uzalendo na wengine uwezo wa hali ya juu katika kutoa burudani.
Katika lile la uzalendo, aliyeshika hatamu alikuwa shujaa wa vita, Kepteni Luka Sinnot aliyepoteza miguu yake kwenye uwanja wa mapambano.
Huyu, alikuwa jasiri uwanjani Jumapili, kwani katika hali yake, alipanda kwa ukakamavu nguzo maalumu iliyowekwa, na kufanikiwa kupandisha na kupeperusha juu yake bendera ya Uingereza – Union Jack.
Ilikuwa mchanganyiko wa furaha na huzuni, baadhi wakiwa hawajui wacheke au walie, bali ukweli ni kwamba Kepteni Sinnot mwenye umri wa miaka 32 tu alipoteza miguu yake mwaka 2010 huko Helmand.
Alikuwa akitafiti eneo lililodaiwa lilitegwa mabomu ya kuwalipua makomredi wenzake, kwa bahati mbaya yakamlipua yeye na kukata miguu yake!
Jingine kubwa lililovuta hisia lilikuwa tumbuizo kutoka kwa mwimbaji kipofu, Lissa Hermans, aliyeimba kwa ustadi mkubwa Wimbo wa Taifa. Wenye ulemavu na wasio na ulemavu walikuwa sehemu ya maelfu waliojaza kwa kiasi kikubwa uwanja na kufanya hafla iwe kabambe.
Fashifashi zikilitawala anga la London muda mwingi, kiasi kwamba hafla ikapachikwa jina la Tamasha la Moto.
Lilikuwa hitimisho la aina yake kwa michezo ya Paralimpiki iliyochukua siku 11, ambapo sherehe za ufunguzi wake zinasemwa kufuatiliwa na watu wapatao milioni 11.2.
Wasanii waliopamba sherehe hizo hawakuwa wadogo, kwani walikuwapo wanamuziki wa kimataifa, waliovuka bahari kwa ajili hiyo.
Nyota wa muziki wa pop wa Marekani, Rihanna na Jay-Z walinogesha sherehe hizo na kuamsha tabasamu usoni kwa karibu kila mwanamichezo na wadau walioshiriki.
Gwaride la wanamichezo wenyewe lilitia fora, wakipendeza kwa bendera, medali na mavazi ya kuvutia waliyokuwa nayo.
Bendera ya Paralimpiki ilikabidhiwa rasmi kwa jiji la Rio de Janeiro watakaoandaa michezo kama hii miaka minne ijayo.
Akitangaza kufungwa rasmi kwa Michezo ya Paralimpiki, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Paralimpiki (IPC), Sir Philip Craven, aliwatoa watu machozi ya furaha kwa hotuba yake.
“Michezo hii imetubadilisha kabisa, hatutakaa tufikirie tena michezo kwa namna ile ile tuliyokuwa tumezoea, wala hatutauwazia ulemavu kwa aina ile ile ya awali. Paralimpiki imeanua wingu lililokuwa linaweka mpaka,” akasema rais huyo mwenye ulemavu.
Kauli hiyo nzito iliwazamisha watu kwenye mawazo, ndipo baadhi wakaanza kulengwa lengwa na machozi.
Katika mashindano hayo, China ilishika nafasi ya kwanza kwa kutwaa jumla ya medali 231, zikiwamo dhahabu 95, fedha 71 na shaba 65.
Nafasi ya pili ilishikwa na ‘Shirikisho la Urusi’ iliyotwaa medali 36 za dhahabu, 38 za fedha na 28 za shaba.
Wenyeji Uingereza hawakuwa mbali na ushindi mnono, kwani walishika nafasi ya tatu, kwa kutwaa jumla ya medali 120, kati ya hizo 34 zikiwa dhahabu, 43 fedha na 43 nyingine shaba.
Katika 10 bora, kwa mtiririko wa kuanzia nafasi ya nne ni Ukraine, Australia, Marekani, Brazil, Ujerumani, Poland na Uholanzi.
Afrika ilibebwa kwa mbali na Tunisia iliyoshika nafasi ya 14 na Afrika Kusini ya 18.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Olimpiki ya London 2012, Sebastian Coe, katika hotuba yake alisema siku 11 za Paralimpiki zilikuwa za uzoefu wa aina yake na maajabu.
Kwamba walishuhudiwa wanamichezo wa aina mbalimbali waliodhaniwa hawawezi kitu wakionesha vitu visivyo vya kawaida michezoni.
Kwamba katika siku hizo, akili za wengi zimefunguliwa juu ya kile wanadamu wanachoweza kufanya, kile kinachoweza kufanikishwa kwa talanta walizopewa na kujituma kwao.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

TANZANIANS QUALIFY AS FIVB INTERNATIONAL REFEREES

Ferguson: Tuvunje benki tumrejeshe Ronaldo