in , , ,

Nigeria, Burkina Faso zafuzu AFCON, EPL……

*Liverpool wawavuta shati Man City

*Villas-Boas ashinda, Defoe aumia

NIGERIA na Burkina Faso zimekata tiketi kucheza nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Nigeria waliwaduwaza Ivory Coast waliokuwa wakipewa nafasi ya kuwa mabingwa wapya, na kuacha kikosi cha kushangilia kilichokodiwa na serikali kikichacha.

Super Eagles waliwafunga Tembo mabao 2-1, wakitangulia kwa bao la Emmanuel Emenike kwa mkwaju wa mbali muda mfupi tu kabla ya mapumziko.

Ivory Coast walijibu mapigo kwa kiungo wake, Cheick Tiote kusawazisha mara baada ya kuanza nusu ya pili ya mchezo.

Hata hivyo, ndoto za nahodha Didier Drogba kunyanyua kombe la Afrika zilizimwa na Sunday Mba aliyepachika bao la pili lisilo na ubishi na kuwaingiza Nigeria nusu fainali kwa mara ya tano.

Katika robo fainali nyingine, Burkina Faso waliwazidi nguvu Togo kwa bao 1-0 lililopatikana katika kipindi cha kwanza cha dakika 30 za ziada.

Nahodha wa Togo, Emmanuel Adebayor alihangaika muda wote wa mchezo kupata bao, lakini hakuonekana kusaidiwa na wenzake vya kutosha.

Nusura aiweke mbele timu yake, pale alipopiga mpira wa kichwa, ukampita kipa lakini ukaokolewa na beki wa Burkina Faso kabla haujavuka mstari.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Tottenham Hotspurs alilalamika kwamba mpira ulishakatisha mstari, hivyo labda teknolojia ya mstari wa goli inatakiwa kuharakishwa.

Hadi dakika 90 zinamalizika, timu zilikuwa suluhu, ndipo dakika 30 za ziada zikaanza. Alikuwa mpachika mabao mahiri wa Rennes ya Ufaransa, Jonathan Pitroipa aliyewanyanyua viti washabiki wa Burkina Faso.

Alifunga bao safi la kichwa kutokana na kona, ambapo alikaa mbele ya wachezaji wote, na hakuna aliyemkaba, na hata golikipa alishitukia mpira ukitinga wavuni.

Katika nusu fainali, Burkina Faso watakabiliana na Ghana wakati Nigeria wataoneshana kazi na Mali.

Mzunguko wa 25 Ligi Kuu England

DSC02401

Katika Ligi Kuu ya England (EPL), Liverpool walioanza kuimarika waliwavuta shati mabingwa Manchester City kwa kwenda nao sare ya mabao 2-2.

Licha ya kucheza nyumbani Etihad mbele ya maelfu ya washabiki wake, City walidhibitiwa vilivyo na vijana wa Brendan Rodgers, ambao Jumatano iliyopita walitoa sare kama hiyo Emirates na Arsenal.

Wenyeji ndio walioanza kupata bao kupitia kwa Edin Dzeko kufuatia majalo ya James Milner, kisha fataki ya Daniel Sturridge ikaisawazishia Liverpool.

Wakati Roberto Mancini akiwapanga vijana wake ili kupata ushindi, nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard aliachia fataki kama ya Sturridge iliyojaa wavuni, na kuwa bao la pili kwa kipa Joe Hart wa City kufungwa mwaka huu.

Makosa ya golikipa wa Liverpool, Pepe Reina kutoka golini kumfuata Sergio Aguero kwenye wingi liliwagharimu Liverpool, kwani Aguero alimimina majalo iliyozama moja kwa moja golini.

Kwa sare hiyo, Manchester City wamefikisha pointi 52, zikiwa ni tisa nyuma ya vinara Manchester United, wakati Liverpool wamefikisha pointi 36 na wanashika nafasi ya saba.

Katika mechi nyingine, Tottenham Hotspurs waliwashinda kwa tabu West Bromwich Albion kwa bao 1-0 lililofungwa na Gareth Bale, na kujiimarisha kwenye nafasi ya nne.

Albion waliwanaba Spur kipindi cha kwanza, lakini dakika mbili baada ya kipindi cha pili mambo yalibadilika, baada ya mlinzi wao, Goran Popov kupewa kadi nyekundu kwa kumtemea mate Kyle Walker wa Spurs baada ya kugombea mpira.

Baada ya hapo Spurs walitawala na Albion wakaanza kucheza kwa kujihami, ndipo Bale akatumia mwanya huo kupachika bao pekee katika dakika ya 67.

Pamoja na ushindi, kocha Andre Villas-Boas alipata pigo, kwa kuumia mshambuliaji pekee anayetambulika, Jermain Defoe.

Washabiki walisikika wakimpigia kelele kocha huyo, wakimwambia alikosea kwa kutosajili mpachika mabao kwenye dirisha dogo la Januari lililofungwa wiki iliypita.

Albion nao walicheza bila mpachika mabao wao, Peter Odemwingie aliyeachwa nje ya kikosi kilichosafiri, baada ya utata wake wa kulazimisha kujiunga Queen Park Rangers (QPR) siku ya mwisho ya usajili na kushindwa.

Albion wamebaki nafasi ya tisa baada ya kujikusanyia pointi 34.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

KUNA UMUHIMU WA KUWA NA SHINETA BADALA YA CHANETA

Kashfa upangaji matokeo soka ya Ulaya