in , , ,

Neymar hatiani

*Ni kwa kukwepa kodi Brazil, atozwa faini ya mamilioni

*Mahakama ya Hispania nayo yalianzisha Barcelona

Hatiani. Ndilo neno sahihi kutumia na linatumika huko Rio sasa,
likimhusisha nyota wa Barcelona, Neymar na hatia ya kukwepa kodi ya
mamilioni ya dola.

Mahakama nchini Brazil imekamilisha kazi yake na kuamua kwamba
mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Brazil ambaye jina lake kamili ni
Neymar da Silva Santos Júnior, alifanya udanganyifu wa kodi.

Neymar anayeendeleza makali ya ushambuliaji Barcelona katika wale
wanaoitwa mapacha watatu – sambamba na Lionel Messi na Luis Suarez,
anadaiwa kuficha taarifa za mapato yake yanayotokana na mikataba
kadhaa minono.

Kwa makosa aliyotenda, Neymar sasa atatakiwa kulipa reals (sarafu ya
Brazil) milioni 188.8 ambazo ni sawa na dola milioni 51.74,
zikijumuisha faini, riba na kodi za nyuma alizokwepa. Neymar, mzaliwa
wa Brazil aliingia kwenye ulingo wa soka akiwa na kikosi cha vijana
cha Santos humo humo Brazil.

Akiwa na umri wa miaka 14 alianza kutafutwa na klabu kubwa za Ulaya,
lakini alibaki nyumbani akiendelea kuchezea Santos, akaanza soka ya
kulipwa 2009 na ni wakati huo klabu kubwa zikaanza mazungumzo na
Santos, na fedha za siri zikaanza kulipwa lakini Neymar hakuzilipia
kodi.

Hatimaye Neymar mwenye umri wa miaka 24 kwa sasa, alihamia Barcelona
2013, na inadaiwa hata katika mkataba huo kuna fedha zililipwa kwa
kificho, ambapo Santos wamekuwa wakilalamikia hilo.

Mwaka jana Neymar alitangazwa na jarida la Forbes kuwa anashika nafasi
ya 82 miongoni mwa watu maarufu matajiri na wa 23 miongoni mwa
wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani, akielezwa kuvuta dola milioni 14
kama mshahara na nyingine milioni 17 kutokana na kutangaza kampuni
mbalimbali.

Santos wanadai kwamba mjadala wa Neymar kujiunga na Barca ulifanyika
tangu 2011 na kwamba malipo yalilipwa kwa kampuni ya Brazil
inayodhibitiwa na baba yake. Wapelelezi wa Hispania wanaona kwamba
fedha hizo zilitakatishwa na kudaiwa kulipwa kwa ajili ya mambo
mengine ili wakwepe kodi.

Santos, baada ya kuona kwamba walidanganywa, waliamua kufungua kesi
ili kupata ukweli wa kina juu ya kilichofanyika. Neymar na babaye
wakati huo walikana kufanya kosa lolote, wakidai kwamba masuala yoyote
ya kodi yangefanyiwa kazi nchini Brazil.

Na hicho ndicho kilichotokea hasa mwaka jana, baada ya Jaji Carlos
Muta wa Brazil alipomfungulia mashitaka Neymar kwa tuhuma za kuficha
sehemu ya mapato kutoka ng’ambo kuanzia 2011 hadi 2013, Barcelona
wakitajwa kuwa chanzo cha utoaji wa fedha hizo.

Jaji Muta sasa ameagiza kwamba mali za Neymar zenye thamani ya
mamilioni hayo zikamatwe. Muda mfupi baadaye, Neymar na baba yake
wakaamriwa kulipa euro 100,000 (dola 109,374 ) zikiwa ni faini kwa
kosi ambazo hazikulipwa kuanzia 2007 na 2008.

Neymar anadaiwa kukatia rufaa uamuzi wa awali na pia mawakili wake
wanajiandaa kupinga hii ya pili inayohusu miaka ya 2007 na 2008.
Maamuzi haya ya mahakama ambayo ni ya madai ni tofauti na ya jinai
yaliyofunguliwa dhidi ya mwanasoka huyo mwaka jana.

Mahakama iliamua mapema mwaka huu na kuruhusu kwamba kesi hiyo ya
jinai iendelee baada ya hii ya madai kumalizwa. Mahakama ya Hispania
nayo imeona kwamba kuna uelekeo wa kuanzisha kesi kumhusu mchezaji
huyo, kutokana na uhusika wa Barcelona na Santos.

Kwa kuwa Neymar anacheza nchini Hispania, mamlaka za huko zinaamini
kwamba kuna kiasi cha fedha serikali ya huko imeminywa. Japokuwa
Neymar na mzazi wake huyo hawajafunguliwa rasmi mashitaka nchini
Hispania, Barcelona wataingia kizimbani kwa madai ya udanganyifu wa
kodi.

Mkondo huo wa sheria pia unawafuata Rais wa Barcelona, Josep Bartomeu
na rais wa zamani, Alexandre ‘Sandro’ Rosell. Klabu wamekana kufanya
kosa lolote lile. Katika uamuzi wa karibuni zaidi kwenye masuala ya
ukwepaji kodi, mchezaji mwenza wa Neymar, Javier Mascherano, alikiri
makosa mawili aliyotenda akiwa hapo Hispania.

Mascherano alikiri kutolipakodi ya mapato yake ya 2011 na 2012,
akatiwa hatiani na kutakiwa kulipa kodi na adhabu ya jela anayotarajia
kuiepuka hata hivyo. Mchezaji mwenza mwingine wa Neymar –Messi, naye
anakabiliwa na ukwepaji kodi. Wanasheria wa Messi wanatarajia kuiomba
korti isogeze mbele shauri hilo.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SABABU TANO KUWA YANGA WATAWAONDOSHA APR

Tanzania Sports

Man City mdomoni mwa PSG