in , , ,

SABABU TANO KUWA YANGA WATAWAONDOSHA APR

APR FC kutoka Kigali wameshawasili jijini Dar-es-salaam kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa mzunguko wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga.

Vijana wa Hans van Der Pluijm tayari wako mbele kwa bao moja baada ya kupata ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita jijini Kigali.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa Yanga watawaondosha vijana wa mwalimu Nizar Khanfir na kusonga kwenye raundi ya pili.
Uwezekano huo mkubwa wa Yanga kusonga mbele dhidi ya mabingwa hao wa Rwanda unatokana na sababu tano zifuatazo.

Faida ya mabao ya ugenini

Mabao ya Juma Abdul na Thaban Kamusoko waliyoweka wavuni ndani ya dimba la Amahoro jijini Kigali wiki iliyopita, yanawapa vijana wa Jangwani faida kubwa.

Hii ni kwa kuwa APR wanahitaji kupata magoli mawili au zaidi kwenye mchezo wa kesho vinginevyo watakuwa wameng’olewa kwenye mashindano kutokana na sheria ya goli la ugenini.

Ushindi wa 2-0 au 3-1 au zaidi utawapa APR nafasi ya kusonga mbele. Hata hivyo huo ni mlima mkubwa wa kupanda kwa APR kwa kuwa vijana wa Jangwani wanaonekana kuwa imara.

Ugeni wa mwalimu Nizar Khanfir wa APR

Mwalimu Nizar Khanfir raia wa Tunisia ana wiki mbili pekee tangu alipoteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo mapema mwezi huu.
Kwa vyovyote vile ugeni wake na wachezaji wa kikosi cha APR na benchi zima la ufundi la klabu hiyo ya jijini Kigali kunampa changamoto kubwa kwenye dhamira yake ya kupata matokeo dhidi ya Yanga.

Nafikiri hii ni moja ya sababu iliyosababisha mwalimu huyo kupoteza mchezo wa kwanza dhidi yaa Yanga na hivyo hivyo inaweza kusababisha ashindwe kupata matokeo anayoyahitaji kesho Jumamosi.

Faida ya kucheza nyumbani

Washabiki wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara watakaojaa Uwanja wa Taifa kuiunga mkono timu yao watawapa morali kubwa wachezaji.
Itakumbukwa mabingwa mara nane wa Afrika Al-Ahly walishindwa kuziona nyavu za Yanga walipocheza Uwanja wa Taifa mwaka juzi. Bao pekee la Nadir Haroub liliwazamisha mabingwa hao kwa 1-o Machi 2014.

Hata hivyo APR pia hawatakuwa wapweke kwenye mchezo wa kesho. Watakuwa wakiungwa mkono na washabiki wa Simba SC kama washabiki wa Kiyovu Sports walivyowashangilia Yanga kule Amahoro wiki iliyopita.

Hans van Der Pluijm

Mholanzi huyu aliiongoza Berekum Chelsea ya Ghana kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2012.
Hayo yalikuwa mafanikio makubwa kwa kocha huyo kwa kuwa klabu hiyo changa kutoka jijini Berekum ilikuwa inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza kwenye historia yake.

Kwa vyovyote vile mafanikio hayo yanampa Pluijm utulivu na hali ya kujiamini kuelekea mchezo wa kesho hivyo anaweza kukiongoza vyema kikosi chake kuwaondosha APR na pia kuvuka raundi ya pili na kutinga hatua ya makundi.

Thaban Kamusoko

Nizar Khanfir alikiri baada ya mchezo wa kwanza kuwa makali ya kiungo Mzimbabwe wa Yanga Thaban Kamusoko ndiyo yaliyokipoteza kikosi chake kwenye mchezo huo.
Mzimbabwe huyo aliwapoteza viungo tegemeo wa APR Yannick Mukunzi na Jihadi Bizimana na pia kuchangia bao moja kwenye ushindi wa 2-1.
Kamusoko yuko fiti na anapatikana kwa ajili ya mchezo wa kesho. APR watakuwa kwenye wakati mgumu kupata matokeo endapo kiungo huyo atakuwa kwenye kiwango chake tulichokizoea.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Pep Guardiola ni mbunifu au mvurugaji vipaji?

Tanzania Sports

Neymar hatiani