in

Nazikumbuka amsha amsha za Teddy Mapunda Taifa Stars

Teddy Mapunda

Nilikuwa mbali na mifumo ya vyombo vya habari wakati kifo cha galacha wa sekta ya michezo nchini Teddy Mapunda kilipotangazwa. Nilikokuwepo nilitegemea huduma ya ujumbe mfupi wa simu za mikononi kuliko kupatikana kwa mtandao wa intaneti.

Hapo ndipo simu yangu iliashiria kupokea ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa mmoja wa marafiki zangu akinijulisha juu ya kuaga dunia kwa mdau mkubwa wa sekta ya michezo,habari, masoko na maendeleo ya jamii nchini Tanzania, Teddy Mapunda.

Ndiyo, jina lake ni Teddy Mapunda, ambaye alikuwa mke wa Nestory Mapunda. Kutajwa jina la Teddy Mapunda kufariki dunia nilipatwa na mshangao hasa mazingira ya kifo chenyewe. Kwamba aliugua ghafla au kujisikia vibaya wakati akiwa kwenye dhifa katika hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.

Baadaye nilijulishwa kuwa kuugua kwake ghafla kulitokana na sukari kuzidi. Mimi si tabibu lakini nafahamu matukio  ya binadamu kufariki dunia ghafla huacha simanzi kama vilivyo vifo vingine.

Kwangu mimi jina la Teddy Mapunda lina mvuto mkubwa katika sekta ya michezo na burudani kama lilivyo jina la Sauda Kilumanga. Wawili hawa walikuwa maarufu katika michezo na burudani, na walivutia mashabiki wengi katika maeneo mawili.

Kwa Teddy, nakumbuka wakati wa kocha wa timu ya taifa Taifa Stars, Marcio Maximo alikuwa mmoja wa wadau wenye sauti kubwa na ushawishi nchini. Teddy alikuwa mwanamke ambaye aliwavutia wanahabari na kila mmoja kwenye idara za michezo na burudani alitamani kwenda kwenye mikutano yake.

Kwanza alikuwa anashawishi mashabiki, alitumia lugha ya kuhamasisha na kuitangaza vilivyo kampuni ya SBL alikokuwa akifanyia kazi. Ikumbukwe SBL walikuwa wadhamini wa timu za Taifa za mchezo wa soka. wakati ambao soka lilipata neema kutoka kwa Rais Kikwete.

Uongozi wa Kikwete ulimlipa kocha mkuu wa Taifa Stars na benchi lake, Marcio Maximo raia wa Brazil. Mapenzi ya Kikwete katika michezo na burudani ndiyo yanatuletea jina la Teddy Mapunda. Si soka pekee lilinufaika na Kikwete bali hata mpira wa kikapu,pete na riadha. Mvuto wa Kikwete kwenye michezo uliwavutia wadhamini wengi na kila mmoja alipendelea kujihusisha nayo ili kujipatia faida.

Mwanadada Teddy alijua kunogesha mikutano yake kwa kuhamasisha wengi, uvaaji wa jezi za timu za taifa, matamanio ya kuona mastaa wa Taifa Stars, alichagiza hamasa ya Marcio Maaximo ambaye kila wakati alisisitiza washabiki kujazana viwanjani.

Watanzania wakihamasishwa huwa wanahamasika si kidogo na wanaipenda nchi yao kwa dhati. Kuna wakati mtu angeweza kudhani Teddy Mapunda alikuwa msemaji au mhasishaji kutoka Shirikisho la soka nchini TFF. Wala hakuwa msemaji wa TFF bali ofisa uhusiano na masoko aliyeiwakilisha kampuni ya SBL kupitia bia yake ya Serengeti.  

Akiwa amevalia jezi ya Taifa Stars na yenye nembo ya wadhamini wake huku kichwani akiwa amevali kofia maarufu kama kapelo na hereni kubwa masikinio mwake, alikuwa kivutio haswa na alijua kuzungumza kwa staha.

Ukimtazama macho yake mlegezo yalikuwa yanaashiria furaha,uchangamfu na mapenzi makubwa kwa mchezo wa soka. akiwa kwenye mikutano na wanahabari wa michezo pamoja na viongozi wa TFF wengi walisubiri pale kipaza sauti kitakapofika kwa Teddy.

Zamu ya Teddy ilikuwa inasisimua namna alivyopanga maneno huku akiwa amevaa tabasamu la kuuza kampuni yake na kuzua amsha amsha kwa wapenzi wa soka ili kuziunga mkono timu za taifa.

Ilikuwa kawaida kushuhudia mashabiki wakiwa wamejazana kwenye mazoezi yua Taifa Stars au Kilimanjaro Stars ndani ya uwanja wa Uhuru. Lilikuwa jambo la kawaida kwa mwandishi wa makala haya kutorioma vipindi Chuoni na kwenda kushuhudia mazoezi ya Maximo na Taifa Stars.

Halafu, baadaye unasubiri kumsikia Teddy Mapunda akiliamsha dude la hamasa kwa mashabiki. Mojawapo ya mchezo wa kusisimua ulikuwa kati ya Tanzania na Sudan. Pale uwanja wa taifa palikuwa na nyomi si kidogo. Mashabiki walijazana, wakasubiri kasi ya Mrisho Ngassa ambayo Wasudan hawakuijua, kisha mlinda mlango Akrama akawa mchezaji aliyeonja joto la jiwe la kikosi cha Marcio Maaximo.

Nazikumbusha amsha amsha za kufuzu fainali za AFCON, CHAN na Kombe la dunia, pamoja na mashindano ya Chalenji Afrika mashariki na Kati. Zilikuwa nyakati ambazo jina la Teddy Mapunda lilikuwa limo midomoni mwa mashabiki na wadau wengine wa soka. yeye alikuwa ‘icon’ kwenye michezo na burudani.

Uongozi wa TFF ya Tenga ulikuwa na tabasamu kama alivyokuwa Teddy. Ni kipindi ambacho rais alikuwa Jakaya Kikwete. Amsha masha za Teddy zilikuwa kivutio kikubwa kwa wadau wa michezo. Na zaidi katika maisha yake ametumikia sekta ya michezo na burudani akiwa mtu mwenye jina kubwa katika eneo hilo.

Nimalize kwa kusema kuwa Teddy Hollo Mapunda alikuwa mke wa Nestory Mapunda. Kifo chake kilitokea tarehe 4 mwezi Mei mwaka 2021 katika hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam. Mazishi yake  yanatarajiwa kufanyika tarehe 10 mwezi wa tano mwaka 2021 katika makaburi ya Kondo, Bahari Beach. Teddy ameacha mume na watoto wawili Al Tevin Mapunda na Nigel Mapunda.

Kabla ya kifo chake Teddy alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Montage Events Limited, na mkazi wa kitongoji cha Kilongawima huko Mbezi Beach barabara ya Usalama na Mtakuja jijini Dar es salaam. Nyakati zake za amsha amsha zimetuachia somo na kuishi na watu kwa tija.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Benjamin Mkapa Stadium Dar

FIFA ‘imekazia’ msimamo wa El Hadji Diouf

Simba vs Yanga

Maswali magumu kuahirishwa mechi Simba vs Yanga