Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kumalizika kwa tamasha la Simba Day, mmoja wa vigogo wa klabu hiyo na mkongwe kwenye kandanda Cresentus Magori alisema ana matumaini kuwa klabu yake itanyakua kombe la kwanza katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi Yanga. Hali kadhalika, upande wa Yanga, akizungumza kwenye kilele cha ‘Wiki ya Mwananchi’, kocha Romaine Folz alibainisha kuwa anatambua kazi aliyonayo na amefika kufanya kwa ajili ya mashabiki waliojazana kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Yanga wamebainisha kuwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo utakaofanyika Septemba 16. TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu katika mchezo huo.
Vita ya ‘Wazulu’
Unapozungumzia kabila la Wazulu moja kwa moja unaitaja nchi ya Afrika kusini. Katika mchezo wa Simba na Yanga wa Ngao ya Jamii unawakutanisha “Wazulu” kwa maana ya wazaliwa wa Afrika kusini. Si lazima wawe wanatoka kabila la wazulu, badala yake ni umaarufu wa kabila hilo mbali yam engine kama Xhosa, Afrikaner, na mengineyo. Katika mchezo Yanga wataingia uwanjani wakiwa na benchi la ufundi kutoka Afrika kusini. Benchi la Yanga linaongoza na Romaine Folz, nyuma yake wamejaa wataalamu kutoka Afrika ambao watahakikisha bosi wao huyo anakuwa na kikosi imara na chenye uwezo wa kuichachafya Simba. Maisha ya Romal Folz kwenye ukocha yamekuwa na uhusiano wa karibu na Afrika kusini, ndiko alikoweka msingi wa kuwa mwalimu wa mchezo wa soka. Wakati Folz akiwa na wataalamu wenzake, upande wa Faldu Davids habari ni hiyo hiyo. Fadlu Davids kwenye benchi lake kuna wataalamu kutoka Afrika kusini ambao watakuwa na kibarua cha kuwanyuka wenzao. Kifupi ni vita vya Wazulu ndani ya mchezo wa Ngao ya Jamii.
Ugeni wa Folz na uzoefu wa Fadlu
Inawezekana Romain Folz anamfahamu vyema Fadlu Davids. Lakini Fadlu Davids pia anamfahamu Romain Folz. Ndiyo kusema mchezo huu utakuwa chini ya makocha wanaofahamiana tangu Afrika kusini, lakini wana tofautiana kidogo tu; Fadlu Davids anazijua kasheshe za mechi ya Kariakoo Derby, huku Romain Folz ikiwa ni mara ya kwanza kuongoza kikosi cha timu kubwa ya Yanga. Fadlu Davids anawajua wachezaji wa Yanga na mbinu zao binafsi, huku Romain Folz akiwa na kibarua cha kutafuta mwarobaini wa kuifunga Simba kwa mara ya kwanza. Makocha hawa wote wanatafuta furaha ya mashabiki wao, wakati Folz akitaka kuweka rekodi, mwenzake Fadlu anataka kuondoa uteja wa Simba kwa Yanga.
Mashabiki Yanga, Simba hawamjui Romain Folz
Tangu alipowasili nchini na kutambulishwa kuwa kocha mpya, Romain Folz hajawahi kucheza mchezo wa rasmi wa ushindani na timu yoyote. Mechi nyingi alizocheza ni za kirafiki ili kuiandaa timu yake. mashabiki wa Yanga wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa wanataka kuangalia ‘uchawi’ wa kocha huyo katika kuipasisha timu yao. kwa shabiki wa Yanga hakuna raha kama kuifunga Simba, hali kadhalika kwa Simba wanajisikia vizuri wanapowafunga Yanga. Kwa maana hiyo katika mchezo huu mashabiki wa pande zote mbili wanatamani kuona mbinu gani zitatumiwa na Folz ili wampime kwa kazi yake.Simba wanatamani kuona namna kocha huyo mwenye sifa za kufundisha soka la burudani atafanya nini mbele ya Fadlu Davids, na pia wanataka kuvunja mwiko wa kufungwa mfululizo na hivyo kufuta kabisa uteja kwa Yanga. Yanga wao wanaelekea kupima kazi ya kocha huyo katika mpambano mkubwa dhidi ya watani wao. Romain Folz ataweza kufanya kazi yake vizuri? Ni suala la kusubiri na kuona.
Uzoefu kuamua mchezo?
TANZANIASPORTS katka tathmini yake inabainisha kuwa mchezo wa Kariakoo Derby huwa hautabiriki na mara nyingi hutokea mambo ya ajabu ya wachezaji binafsi na ufundi wa makocha. Katika mechi walizokutana kwa misimu minne mfulilizo Yanga wanaonekana kuwa wababe mbele ya Simba, lakini ushindi wao umekuja katika namna ya ajabu. Mchezo mmoja ambao Simba wanapenda kufuta akilini mwao ni ule walipochapwa mabao 5-1 na kuwaliza Shomari Kapombe na Mohammed Hussein wakiwa Simba. Katika mchezo wa timu hizi kumekuwa na makocha kadhaa binafsi ambayo yanawasababisha matatizo ya kufungwa. Pia uzoefu unatumika kama njia ya kusaka ushindi, huku ubora binafsi wa wachezaji unakuwa kivutio zaidi ndani ya dimba. Ni uzoefu wa Simba au Yanga ndiyo utakaoibuka na ushindi? Ni jambo la kusubiri na kuona.
Nahodha wa Simba katika jezi za Yanga atacheka au kununa?
Hakuna ubishi Mohammed Hussein anakuwa mchezaji ambaye yupo katikati ya mjadala kuhusiana na mchezo wa Derby. Mohammed Hussein anakuwa mchezaji mwenye mvuto zaidi kuelekea mchezo huu kwani amehama Simba na kujiunga na Yanga. Mohammed Hussein alikuwa nahodha wa Simba ambaye ameacha kitambaa hicho na kuvuka upande wa pili anakokwenda kuwa mchezaji asiye madarakani ndani ya dimba. Yanga wanafahamu kuwa mashabiki wa Simba wamechukizwa na usajili huo lakini hakuna namna nyingine zaidi ya kukubaliana na uamuzi wake.
Katika mchezo huo, Mohammed Hussein atacheka au atanuna wakati mashabiki wa Simba wakimcheka? Hilo linasubiriwa kwa hamu.


Comments
Loading…