in , , , ,

Mwelekeo mpya wa Simba utimize hasira hizi

Tamasha la Simba Day lilikuja na hotuba kali amabzo hazikuzoeleka. Miaka mingi klabu ya Simba ambayo ndiyo mbunifu wa tamasha la soka nchini na ambalo linaigwa na timu nyingi kama vile Yanga, Mbeya City, Singida Black Stars na nyinginezo. Tamasha la Simba Day mwaka huu licha ya kutawaliwa na shangwe, viongozi walikuja na kauli ambayo inaonesha mwelekeo mpya wa Simba katika mchezo wa soka. TANZANIASPORTS inachambua maudhui mazima ya klabu ya Simba na tamasha lao la Simba Day.

Kauli ya Mo Dewji

Akizungumza kwenye Simba Day, Rais wa heshima wa klabu ya Simba, bilionea Mohammed Dewji alifichua shauku ya uongozi ya Simba. Mo Dewji siku ya Simba Day alifuchua kuwa kikosi chao kimejipanga kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali nchini na Kimataifa. Maneno ya Dewji yaliikwenda mbali na kusema kuwa mpango wao ni kuhakikisha wanaleta kombe la Afrika hapa nchini. Ingawaje Dewji hakutaja kombe gani kati ya mawili yanayoshindaniwa Afrika, yaani Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho. Maelezo ya Mohammed Dewji yanayonesha kuwa shauku ya Simba ni kuunda kikosi chenye ushindani na uwezo wa kupambana na timu kali barani Afrika.

Timu ya Afrika SI Ligi Kuu

Katika hali nyingine, hotuba ya Simba ilikuwa na msimamo wa dhati ambao umewekwa bayana mbele ya mashabiki. Uongozi wa Simba umebainisha wazi kuwa malengo yao ni kuhakikisha wanaunda timu ya Afrika. Kwamba katika kikosi chao wameunda kwa kulenga mashindano ya Afrika ambayo bila shaka ni Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika. Mara nyingi Simba wamekuwa wakitupwa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya robo fainali. Kwa miaka kadhaa ilionekana Simba wangetwaa taji la Ligi ya Mabingwa lakini safari zao zilikuwa zinaishia kwenye hatua ya robo fainali. 

Kuonesha Simba wamepania kupiga hatua Kimataifa, wanao ushahidi wa kulikosa kombe la Shirikisho msimu uliopita baada ya kutoka sare 1-1 na RS Berkane kwenye dimba la Amaan Zanzibar. Mchezo huo ulikuwa wa pili baada ya ule wa kwanza Simba kukubali kipigo cha mabao matatu. Kwenye tamasha la Simba Day uongozi umetamka na umeweka ajenda yao kuuu; kutwaa Kombe la Afrika. Uthubutu wa kuwaambia mashabiki kauli hiyo unatokana nan a kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho. Ushiriki wa Simba ulivyokuwa ni ushahidi kuwa walikuwa na uwezo mkubwa wa kutwaa taji hilo, lakini matokeo yalikuja kikatili na kuwanyima fursa ya kuwa klabu ya kwanza Tanzania kutwaa taji kubwa la CAF. 

Mwitiko wa benchi la ufundi

Fadlu Davids ana kila sababu ya kutimiza ndoto za uongozi wa klabu ya Simba. Katika msimu wake wa kwanza ametinga fainali ya Kombe la Shirikisho, ikiwa maana kuwa ana kitu kikubwa cha kuwafanyia mashabiki wa Simba endapo uongozi utamwezesha kuwa na rasilimali muhimu kwenye mashindano. Fadlu Davids katika msimu wake wa kwanza alikuwa na kauli mbiu ya kujenga timu kwa ajili ya ushindani, na akafanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho. Lakini sasa anatakiwa kuvuka zaidi ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho. Kibarua alichonacho sasa ni kutumia wachezaji waliosajiliwa ili kufanya vizuri kwenye mashindano ya Ligi ya mabingwa. Ni dhahiri msimu huu atakuwa amelenga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa kwani waajiri wake wameshasema kuwa wanataka kombe moja la Afrika. Kwa maana nyingine benchi la ufundi la Simba limaefiki malengo ya klabu na wanalo jukumu la kuhakikisha taji linawasili Tanzania. 

Wachezaji kumalizia mkia 

Kazi kubwa ya wachezaji wa klabu ya Simba sasa ni kuhakikisha wanalitwaa taji lolote kati ya mawili ya Afrika ili kutekeleza maagizo ya viongozi wao. Hilo lina maana wachezaji wa Simba watapewa kila aina ya nyenzo ya kuhakikisha anapigania nembo ya klabu ya Simba na kuleta furaha mitaa ya Msimbazi. Wachezaji waliosajiliwa ni katika maeneo ya safu ya ushambuliaji, ulinzi na kiungo wa ushambuliaji. Usajili huo ni kuimarisha kikosi chao na kuwapa nguvu wachezaji ili waweze kutetea jezi za klabu hiyo. 

Mashabiki wana deni

Ingawa viongozi wameweka msimamo wao wa kusaka mataji ya Afrika, kwa upande  wao mashabiki wanalo deni la kuishangilia na kuunga mkono timu kwa hali na mali kuhakikisha wapinzani wao wanateseka kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Kazi ya mashabiki itakuwa kuhamasisha na kujazana kwenye dimba la Benjamin Mkapa ili kuwaongezea nguvu wachezaji wao. Kama shabiki huendi uwanjani kuimba kidedea, utakaa ndani kuangalia Televisheni hadi lini. Nao mashabiki waamke, waujaze uwanja wa Benjamin Mkapa kila inapokabiliana na wapinzani wa kigeni.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Fadlu apasua Kichwa kwa Yanga

Tanzania Sports

Nani kucheka, nani kununa Simba au Yanga