in

Namungo FC kuwatikisa Raja Casablanca?

Namungo FC

Kwa jina la utani wanaitwa Southern Killers, yaani wauaji kutoka kusini. Ni vijana ambao wanaongozwa na mshambuliaji wake Stephe Sey. Majonjo ya vijana hao wakifunga bao basi wote huchomekea jezi zao na kupunga mikono hewani kama ishara ya ‘ringa ringa’ au ‘ng’ara ng’ara’. Ni mtindo wa kipekee ambao unazidi kuchukua sura mpya kwani umewavutia wapenzi wengi wa kandanda nchini Tanzania.

Hao ndiyo Namungo FC ambao wametinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kuwachakaza vigogo CD De Agosto Angola kwa jumla ya mabao 7-5.

Mechi zote za Namungo na Agosto zimechezwa katika uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam kutokana na uamuzi uliofanywa na CAF baada ya kushuhudia vitimbi vya serikali ya Angola dhidi ya Namungo kwa kile kilichoitwa kupambana na virusi vya corona.

Namungo wakiwa chini ya kocha Hemed Morocco wamecheza mechi katika uwanja wa Azam Complex kama wageni na wenyeji kwenye mashindano ya CAF. Awali walicheza dhidi ya Al Hilal mechi mbili kisha CD Agosto nao wamelazimishwa kutumia uwanja wa Tanzania kutokana na figisu za kwao.

Tanzania Sports
Raja Casablanca

Kutinga hatua ya makundi ina maana Namungo watakabidhiwa kitika cha shilingi milioni 600 kama sehemu ya maandalizi na motisha wanayotoa CAF kwa timu zinazofuzu hatua ya makundi.

Kundi D ambalo imepangwa Namungo kwenye kombe la shirikisho ndilo linalovutia zaidi. kwenye kundi hilo, Namungo imepangwa na Raja Casablanca ya Morocco, Nkana Rangers ya Zambia na Pyramid ya Misri. Vigogo wa Morocco na Misri ndiyo tishio kwa Namungo kutokana na kucheza kwa mafanikio kwa miaka ya karibuni.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Machi 10 mwaka huu, huku kocha wao Hemed Morocco akiwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha vijana wake wanacheza kwa mafanikio zaidi bila kujali ukubwa wa timu watakazokabiliana nazo.

Raja Casablanca inafahamika nchini kwa sababu imewahi kuja kucheza na mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga. Hii ndiyo timu ambayo bila shaka ni tishio kwa Namungo.

Morocco imekuwa na vilabu vyenye mafanikio, ambapo Raja Casablanca ndiye bingwa mtetezi wa kombe la Shirikisho la Afrika, CAF.

Msimu uliopita vilabu vinne vya soka Morocco vilifika hatua ya nusu fainali na fainali kwenye mashindano ya CAF msimu uliopita. Klabu hizo ni Wydad Casablanca na Raja Casablanca zilifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Vilevile klabu ya HUS Agadir yenyewe ilitinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ambako bingwa alikuwa RS Berkane. Kiwango walichonacho kinatokana  na kuundwa na wachezaji waliocheza kwa ushindani katika ngazi za juu.

Unapozungumzia soka la Afrika kwa ngazi za vilabu jina la Raja Casablanca ni miongoni mwake. Daraja la Raja Casablanca ni lile la Al Ahly ya Misri, Esperance ya Tunisia, Club Africain ya Tunisia, Enyimba ya Nigeria,Etoile Du Sahel ya Tunisia, Orlando Pirates,Mamelodi Sundowns za Afrika kusini au TP Mazembe ya DR Congo.

Hatua waliyofikia Namungo kwa sasa ni kubwa kutokana na historia yao. Namungo bado ni timu change ambayo haina historia kubwa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini imeonesha kiu ya mafanikio na kutinga hatua ya makundi itabaki kuwa historia kubwa kwa kandanda Tanzania.

Miaka ya nyuma imewahi kuibuka timu ya Tanzania Stars ambayo iliundwa na wachezaji wengi waliostaafu soka, wakashinda taji la TFF hivyo wakafanikiwa kuwakilisha kimataifa. Licha ya kutofanya vizuri lakini ulikuwa ujumbe kuwa lolote linawezekana kwa timu ikiwa dhamira ya kiufanikiwa ikiwa imechukua hatua zaidi.

Namungo F.C imecheza mechi zote kwenye uwanja wa Azam Complex huku ikihudhuriwa na mashabiki wachache wa soka. Kutokana na kuvuka na kutinga hatua ya makundi bila shaka mashabiki watavutika zaidi kuona kandanda la vijana hao. 

Kwa sasa mvuto wa Namungo umeongezeka zaidi, na imekuwa timu ambayo ina kila sababu ya kujivunia mafanikio waliyonayo kwa sasa. Kwa misimu ya karibuni hakuna timu ya Tanzania iliyotinga hatua ya makundi kwenye Kombe la Shirikisho.

Ili Namungo waweze kusonga mbele wanatakiwa kujiandaa vilivyo kuelekea mechi za mashindano hayo. Wanakabiliana na timu nzuri ambazo zimefuzu kutokana na viwango vyao.

Pia Namungo wanakwenda kukabiliana na timu zenye uzoefu mkubwa kwenye mashindano ya Kimataifa, hivyo ni fursa kwao kuhakikisha wanafanya vizuri kwneye uwanja wao wa nyumbani, pamoja na kutafuta pointi kwenye viwanja vya ugenini. Si rahisi kushinda mbele ya waarabu kama Raja Casablanca lakini hakuna lisilowezekana kwenye kandanda.

Ni wakati wa kuamini kwenye soka la kisasa kwamba kila timu inayo nafasi ya kushinda bila kujali ugenini au nyumbani. Naamini Namungo imeyaona makosa ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa misimu iliyopita ambako walikuwa wanakula vichapo kwenye mechi za ugenini.

Msimu huu Simba wamerekebisha makosa ambako mchezo wao wa kwanza ulikuwa ugenini na walifanikiwa kushinda dhidi ya AS Vita. Kwahiyo linapofika suala la kujifunza kwa wengine, Namungo wanao mfano wa karibu kabisa ambao ni klabu ya Simba.

Kila la lenye heri kwa wawakilishi wetu hawa. Nina matumaini maelfu ya watanzania wanaiombea timu hii ifanye vizuri kimataifa na kuhakikisha msimu ujao tunakuwa na timu nyingi kwenye mashindano ya CAF. Ni wakati wetu.

Ni wakati wa Namungo sasa ambao wameibuka ghafla kuliko hata Azam FC iliyotegemewa kuwa itafanya vema kwenye medani ya kimataifa. Kila la heri Southern Killers.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Ferland Mendy celebrates his strike

Refa ameharibu ushindi wa Real Madrid

man city

Ni ipi siri ya mafanikio ya Manchester City?