in , ,

Mourinho huyoo Man United

Siri imevuja, José Mário dos Santos Mourinho Félix, maarufu zaidi kama
Jose Mourinho ndiye anakuwa kocha mpya wa Manchester United, kuchukua
nafasi ya Louis van Gaal – LVG – anayechukuliwa alishindwa kuwapa raha
waliyotaka watu wa Old Trafford.

Baada ya mawimbi na vigingi mbalimbali, hatimaye Mourinho (53)
anaingia Man U – moja ya klabu kubwa duniani, sasa kocha aliyefundisha
Chelsea, Real Madrid, Inter Milan, Porto, Benfica na Uniao de Leiria.

Tangu apoteze kazi yake Chelsea Desemba mwaka jana, kulikuwapo tetesi
kwamba angechukua nafasi ya LVG, mwenyewe akiwa hakanushi wala
kukubali, ila akisema tu kwamba atarudi kwenye moja ya timu kubwa
ndani ya Ligi Kuu ya England (EPL).

Na Jumamosi hii, baada ya ushindi wao dhidi ya Crystal Palace kwenye
fainali ya Kombe la FA, badala ya kuwa sherehe ilionekana kana kwamba
ni aina ya kuagana au hata maziko ya haramia.

Hata LVG alivyokuwa akikatiza kwa ajili ya kuzungumza na wanahabari
uwanjani Wembley, akiwa na kombe, bado uso wake haukuwa na furaha
badala yake kilichokuwa kinajiri ni taarifa na picha za Mourinho akiwa
karibu tu mjini hapo kwenye Ukumbi wa O2 akishuhudia pambano la ngumu
la David Haye.

Alipoulizwa na wanahabari, alidai hakuwa na muda wa kujadili kuondoka
au kubaki kwake, akasema ‘it is over’, ikidhaniwa kwamba alimaanisha
kwamba muda wa kibarua chake umeisha, lakini wengine wakatafsiri
kwamba alimaanisha msimu kwa Man U ulikuwa ndio umefika ukingoni.

Hata hivyo, aliwaeleza wafanyakazi wenzake kwamba hakuwa na uhakika
iwapo angewaona tena, wakati akiwaaga, akielekea hakuwa na uhakika
kama angebaki Old Trafford kwa msimu ujao. Imekuwa misimu miwili
migumu kwake, akijaribu wachezaji tofauti kwenye nafasi mbalimbali na
akilaumiwa kwa mtindo wa uchezeshaji unaochusha.

Habari sasa si LVG tena, bali ni mkataba wa miaka mitatu wa Mourinho
kuwa hapo Old Trafford kwa ajili ya kazi, akiwa ameinyatia nafasi hiyo
tangu wakati Sir Alex Ferguson akistaafu, ambapo alionekana kuwa
karibu naye, lakini Fergie akampendekeza David Moyes, Mskochi
mwenzake, aliyepewa kazi na kufukuzwa kabla ya mwaka kumalizika.

Dili la Mourinho limewezeshwa na wale wanaoitwa ‘super agents’ kisha
vyombo vya habari vikainasa siri hiyo huku wamiliki na viongozi wa Man
U wakikaa kimya, hata bila kuzungumza na LVG wala wasaidizi wake, kitu
kilichowaudhi na kuwaacha katika sintofahamu.

Ni miaka 12 tangu Mourinho alipoonekana kwenye uwanja wa Old Trafford,
magazeti ya hapa yakimrejea kama kocha mdogo, wakati Porto
walipowang’oa Mashetani Wekundu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa
Ulaya (UCL).

Wapo wanaounga mkono uteuzi huo tarajiwa lakini wengine wakiona si
wazo jema, ikizingatiwa kwamba Mourinho alifanya vibaya msimu uliopita
kiasi cha kufutwa kazi Chelsea, akionekana kwamba hakuwa na mbinu mpya
wala mpango ‘B’ au ‘C’ baada ya ule wa ‘A’ kushindwa.

Wengi wataona ni sawa kwake kuingia kama njia ya kujibu mapigo kwa
majirani zao – Manchester City – waliokuja na Pep Guardiola
atakayeanza kazi kiangazi hiki. Hata hivyo, kulikuwa na
kutokukubaliana awali miongoni mwa wakuu waOld Trafford, wakiangalia
zaidi tabia za Mourinho, mtu mwenye tambo ambaye mara kadhaa amejikuta
katika uvunjifu wa sheria na kanuni. Si mtu anayependa kuingiza vijana
kwenye timu ya kwanza kutoka akademia, bali kununua majina makubwa,
hivyo anaelekea atabadili kwa kiasi kikubwa mfumo uliozoeleka Old
Trafford.

Hata hivyo, LVG atajiualumu mwenyewe kwa aina ya utawala aliokuwa nao
Old Trafford, akiwa na uongozi wa kiimla ambao ulikaribia kuwafanya
wachezaji wafanye uasi, ndipo viongozi wakakutana na wachezaji
waandamizi kuwahoji juu ya kocha huyo.

Ndiyo sababu habari za kuondoshwa kwake zilivuja kabla hata suti yake
haijakauka kwa kumwagiwa champagne baada ya kutwaa Kombe la FA, ambapo
aliambiwa asante lakini alichelewa mno hivyo kwamba ushindi na ubingwa
huo haungemsaidia kuepuka kukinywa kikombe alichoandaliwa – kuupoteza
ukocha wake kabla ya muda wa mkataba kukamilika.

Ndiyo maana hata pale Wembley Jumamosi hii kulikuwa na kelele za watu
zikisema; “José Mourinho” wakati aliyekuwa akiwapa kombe hilo alikuwa
ni LVG. Ana haki ya kufikiri kwamba suala lake lingeshughulikiwa kiutu
zaidi, kwa yeye kujulishwa mapema kwamba mkataba ungekatishwa, lakini
hiyo ndiyo soka na adha ya kuwa kwenye klabu kubwa, kama mwenyewe
alivyosema wakati akianza kazi miaka miwili iliyopita – Manchester
United ni klabu kubwa zaidi duniani.

Ilikuwa chini ya LVG, katika msimu wake wa kwanza, United waliweka
historia mbaya zaidi ya kuanza ligi kwa miaka 25, ambapo wachezaji
walilalamikia mipango yake ya ziara na mechi za kabla ya msimu,
akiwapeleka Los Angeles, wakajihisi kana kwamba wapo kwenye ‘gereza
lenye hadhi ya nyota tano’ kutokana na mazoezi magumu yaliyogawanywa
kwenye vipindi viwili kila siku. Mwisho wake umekuja asivyotarajia, na
Kombe la FA na mwanzo wa Mourinho akichekelea.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Manchester United watwaa Kombe la FA

Tanzania Sports

Van Gaal afukuzwa