in , , ,

MOURINHO ANATESWA NA REKODI YA 2005

Kwenye msimu uliopita wa 2014/15 wa Ligi Kuu ya Uingereza Chelsea walifungwa mabao 32 kwenye michezo yote 38 huku wakishinda taji hilo la ligi. Hayo yalikuwa mabao machache zaidi kuliko timu yoyote kwenye michuano hiyo. Kiuhalisia yanaashiria kuwa Chelsea ina ulinzi mkali zaidi ya timu nyingine yoyote ya Uingereza.

Uwepo wa walinzi wa kati John Terry, Gary Cahill, Kurt Zouma, golikipa mahiri Thibaut Courtois na walinzi wengine kumeuimarisha ulinzi wa Chelsea. Hata hivyo Jose Mourinho anaona safu ya ulinzi ya timu yake haijaimarika vya kutosha. Anaripotiwa kufanya jitihada kumtwaa John Stones kutoka Everton.

Chelsea ilifunga mabao 73 tu kwenye msimu huo uliopita wa ligi. Walikuwa nyuma ya washindi wa pili wa ligi Manchester City ambao walifunga mabao 83.

Inashangaza mno kwa kuwa Liverpool kwenye msimu wa 2013/14 walifunga jumla ya mabao 101 na hawakuweza kushinda taji hilo la ligi. Kushinda ligi wakiwa na mabao 73 tu ya kufunga kunaashiria kuwa Chelsea walibebwa mno na ulinzi wao mkali ila hawakuwa wazuri kwenye safu ya ushambuliaji.

Hata hivyo Mourinho haonekani kuwa na mashaka kabisa na safu ya ushambuliaji ya kikosi chake. Amemsajili kwa mkopo mshambuliaji Radamel Falcao kutoka Monaco aliyechemsha vibaya akiwa na klabu ya Manchester United msimu uliopita. Kwake usajili wa Falcao unatosha na haoni sababu ya kusajili mshambuliaji mwengine.

Mourinho pia haoni tatizo lolote kwenye safu ya kiungo ya timu yake. Haoni sababu ya kuongeza kiungo yeyote kikosini. Siku chache zilizopita amenukuliwa akisema kuwa haoni sababu ya kumsajili Paul Pogba wakati tayari ana Fabregas na Matic kwenye timu yake.

Sehemu ambayo Mourinho anaona inahitaji kuongezewa nguvu ya ziada kwenye timu yake ni safu ya ulinzi. Anamfukuzia kwa nguvu mlinzi wa kati John Stones. Kuna ripoti kuwa Mourinho yupo tayari kutoa dau la paundi milioni 26 kwa ajili ya mlinzi huyo kijana mdogo wa miaka 21.

Ikiwa Stones atasajiliwa na Chelsea kwa dau hilo la paundi milioni 26 atashika nafasi ya tatu kwenye orodha ya walinzi waliowahi kusajiliwa kwa madau makubwa na klabu za Uingereza.

Atakuwa nyuma ya Eliaquim Mangala aliyesajiliwa na Manchester City 2104 akitokea FC Porto kwa paundi milioni 32 na Rio Ferdinand aliyesajiliwa na Manchester United kwa dau la paundi milioni 30 akitokea Leeds United 2002.

Pia ataweka rekodi ya kuwa mchezaji namba tatu kwenye orodha ya wachezaji waliouzwa kwa pesa nyingi zaidi kwenye historia ya klabu ya Everton. Atakuwa nyuma ya Marouane Fellaini na Wayne Rooney tu huku akiyafunika majina makubwa kama Joleon Lescott, Jack Rodwell na wengine.

Mourinho yupo tayari kutoa paundi milioni 26. Nafikiri kuna jambo linamtesa Mourinho. Anataka kuimarisha ulinzi. Ulinzi ambao utaifikia ama kuipita kabisa rekodi yake aliyoweka msimu wa 2004/05 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza pale Chelsea iliporuhusu mabao 15 tu kwenye michezo yote 38 ya ligi.

Hakuna timu iliyowahi kuruhusu mabao machache kiasi hicho kwenye ligi ya Uingereza. Rekodi hiyo ilidhihirisha ubora wa mbinu za kujihami za Jose Mourinho.

Ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na umahiri wa safu ya ulinzi ya Chelsea iliyoundwa na walinzi John Terry, Ricardo Carvalho na kiungo mahiri Claude Makelele kwenye nafasi ya kiungo mkabaji.

Rekodi hiyo inamfanya Mourinho aone kuwa mabao 32 ambayo timu yake imeruhusu kwenye ligi msimu uliopita ni mengi. Rekodi hiyo inamtesa na anaamini John Stones anaweza kuwa na mchango katika kuifikia ama kuivunja kabisa.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Man City: £60m kwa De Bruyne

Man U wamtaka Ronaldo