Moja ya kitu ambacho Watanzania wengi huwa tunalilia ni kuwa na wachezaji wengi wa kulipwa. Wachezaji ambao wametoka kwenye ligi au nchi ambazo zimeendelea kwa kiasi kikubwa kwenye mpira wa miguu.
Hatuwahitaji kwa ajili ya kuzisaidia timu zetu ndani ya uwanja peke yake ingawa hili ndilo jambo la msingi na la kwanza. Mchezaji husajiliwa kwa ajili ya kuisaidia timu uwanjani kwanza , ndiyo maana mashabiki huanza kuhoji kipindi ambacho mchezaji husika anaposhindwa kufanya vyema uwanjani kwa sababu hiyo ndiyo kazi yake ya kwanza.
Lakini kuna kazi moja ambayo huwa kama shule kwa wachezaji wetu wazawa. Hawa wachezaji wanaotoka kwenye ligi au nchi ambazo zimeendelea kwenye mpira wa miguu wengi wetu huwa tunatamani wawe darasa kubwa kwa wachezaji wetu wazawa.
Tunaamini kuwa wachezaji wageni ni walimu wazuri wa namna ya kuhakikisha mchezaji anakuwa na nidhamu binafsi ya mazoezi. Namna ambavyo mchezaji anaweza kufanya mazoezi bila kusimamiwa na mtu.
Namna ambavyo mchezaji anaweza kuwa na ratiba binafsi ya mazoezi tofauti na ratiba ya mwalimu wa timu, namna ambavyo mchezaji anavyoheshimu maelekezo na mazoezi ya mwalimu wa timu yake.
Namna ambavyo mchezaji anahakikisha yale ambayo amefundishwa mazoezini anayatimiza kwa nidhamu kubwa uwanjani. Nidhamu ya kuwasilisha maelekezo ya mwalimu kutoka kwenye kiwanja cha mazoezi mpaka kwenye kiwanja cha mechi.
Yeye ni darasa kwa wachezaji wetu hata kwenye ile nidhamu ya kula chakula sahihi kwa kuzingatia muda sahihi wa kula, ile nidhamu ya kupumzika mapema na kutojihusisha na starehe ambazo zinaweza kuharibu kiwango chake.
Wengi wanajifunzia kutoka kwake kwa sababu yeye ni mchezaji wa kulipwa , mchezaji ambaye ana vingi vya kuwafundisha wenzake. Mchezaji wa kulipwa ambaye anajua hata namna ya kuongea na vyombo vya habari bila kuathiri kitu chochote kwa timu yake na yeye mwenyewe.
Hapa ndipo tunapoanzia kumwangazia Bernard Morrison . Kumekuwa na mjadala mkubwa ambao unaendelea kwenye vyombo vya habari pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, mjadala huu kwa kiasi kikubwa unamhusu Bernard Morrison, Yanga na Simba.
Kuna tetesi Simba wanamtaka Bernard Morrison kwa sababu mkataba wake unaisha mwezi ujao wa saba, wakati huo huo Yanga wanadai kuwa Bernard Morrison wana mkataba naye wa miaka miwili unaoisha mwaka 2022.
Bernard Morrison alipokuwa anazungumza na Saleh Ally wa Global TV alidai kuwa mkataba wake na Yanga unaisha mwezi ujao wa saba , ule mkataba wa miaka miwili ambao Yanga wanadai wanao na Bernard Morrison, mkataba huo Bernard Morrison hautambui.
Mimi sina tatizo la hali ya sintofahamu kuhusu mkataba wa Bernard Morrison na Yanga. Kitu ambacho ninakiwaza hapa ni namna ambavyo Bernard Morrison alivyoongea na Global TV kama chombo cha habari.
Nakurejesha huko mwanzo wa makala yangu, nilikuambia hawa wachezaji wageni ambao wametoka kwenye ligi bora kuzidi ligi zetu wanatakiwa kuwa darasa kwa wachezaji wetu wazawa kwenye mambo mbalimbali.
Bernard Morrison katoka kwenye ligi ya Afrika Kusini, ligi bora kuzidi ligi yetu. Pamoja na kuwa darasa ndani ya uwanja, Bernard Morrison anatakiwa kuwa darasa nje ya uwanja. Wakati alipokuwa na Global TV alikuwa nje ya uwanja.
Somo kubwa ambalo alitakiwa kulitoa ni namna ya kuzungumza na vyombo vya habari kwa weredi, darasa ambalo hakulitoa wakati anazungumza na Global TV chini ya kaka yangu Saleh Ally Jembe.
Kwenye mazungumzo yake na Global TV yalinibakizia maswali matano ya muhimu. Kwanza, Bernard Morrison anadai kuwa alicheza michezo miwili ya mwanzo na Yanga bila mkataba. Tujiulize kwa pamoja, Bernard Morrison alikuwa anacheza kama mchezaji as kulipwa au wa hiari?
Swali la pili, kama alicheza michezo miwili bila mkataba, ITC yake ilipatikana kwa njia ipi? swali la tatu, kama Bernard Morrison alicheza bila mkataba alipata wapi leseni ya kucheza, leseni ya kufanya kazi hapa Tanzania na bila mkataba TMS ilikubali usajili wake?
Swali la nne, Je mkataba ambao unatajwa sana na Yanga kupitia GSM kuwa ni wa miaka miwili upo? Kama upo nani mkweli kati yake (Bernard Morrison ) na GSM.
Swali la tano la mwisho, Bernard Morrison ana meneja? Kama ana meneja alimruhusu kwenda kuzungumza na chombo cha habari habari za yeye kufanya kazi bila leseni ya kufanya kazi , bila kibali cha kufanya kazi nchini, bila mkataba wa kazi? Kama anaye, huyo siyo meneja wake ila mshikaji wake na Bernard Morrison anatakiwa kutafuta meneja wake kabla hajafikiria kupata mkataba Simba au Yanga
Comments
Loading…