in , , , ,

Mikono ya Allison inazidi kumuumbua Klopp

Mikono ya Allison inazidi kumuumbua Klopp

Wakati Arkadiusz Milik anapiga shuti kuelekea kwenye lango la Liverpool kila mmoja wetu alijua huo ndiyo ulikuwa mwisho wa Liverpool.

Lilikuwa pigo la mwisho kuondoa uhai wa Liverpool. Wengi tuliona kuwa hakuna ambaye angeweza kuisaidia Liverpool iendelee kupumua tena!.

Mazingira ya ule mpira yalikuwa yanatia mashaka kama Allison angeweza kuokoa ule mpira, moja kwa moja tulijua Liverpool alikuwa anaenda kutoka katika michuano hii ya ligi ya mabingwa.

Mashabiki wa Liverpool walifumba macho wakiamini huo ndiyo ulikuwa mwisho wa safari yao na ikizingatia kuwa zilikuwa dakika za mwisho.

Lakini alitokea binadamu mmoja ambaye aliwapa tumaini jipya, binadamu ambaye aliwapa maisha mapya.

Binadamu ambaye alizua gumzo sana wakati anasajiliwa, wengi walisema sana. Wengi waliongea sana kuona Liverpool ikitoa pesa ya kumnunua mshambuliaji kwa minajili ya kumchukua golikipa.

Na cha kushangaza zaidi kocha ambaye alikuwa anaitoa pesa hiyo alikuwa Jurgen Klopp. Kocha ambaye hakuwa rafiki na matumizi ya pesa nyingi katika soko la wachezaji.

Hakuamini kabisa kipaji cha mpira wa miguu kinaweza kununuliwa kwa bei kubwa. Hakutaka kuamini kabisa binadamu mwenye miguu miwili anaweza kununuliwa kwa pesa ndefu.

Hakutaka kabisa kuanzisha urafiki na aina hii ya upuuzi. Kwake yeye aliona ni upuuzi mkubwa. Alitumia muda mwingi sana kuuongelea usajili wa Paul Pogba kwenda Manchester United.

Hakupendezwa kabisa na kitendo cha timu kutoa pesa ndefu kwa ajili tu ya kumnunua binadamu. Hakuwa anaelewa dunia imefika mbali sana.

Iko sehemu ambayo kumpata mchezaji bora ambaye anaweza kuingia moja kwa moja kwenye kikosi na kuweza kuisaidia timu kwa muda mfupi , timu inatakiwa kugharamika.

Hakuweza kuelewa kabisa kumpata mchezaji wa kiwango cha juu cha dunia inahitajika matumizi ya pesa ndefu, mchezaji ambaye atakuwa na uwezo wa kuamua mechi kipindi ambacho timu haina uwezo wa kufurukuta.

Aina hii ya wachezaji kuwapata ni ngumu kama mkono wako utakuwa wa birika siku zote. Unatakiwa kurefusha mkono ili uwapate waje kukutumikia.

Hakuna huduma bora unayoweza kuipata bila kugharamikia. Na aina hii ya wachezaji wako kwa ajili ya kutoa huduma bora kipindi ambacho wewe umeamua kutoboa mfuko wako haswaaa!.

Ndiyo maana Jurgen Klopp alichelewa kulijua hili, alianza kutoka usingizini kipindi ambacho alipoamua kumchukua Van Djik.

Safu yake ya ulinzi ilikuwa na matatizo sana, ilikuwa inafanya makosa mengi binafsi. Makosa ambayo yalikuwa yanaigharimu timu kwa kiasi kikubwa.

Kuna wakati Liverpool ilikuwa na uwezo wa kufunga magoli 4 lakini inaruhusu magoli 3. Kitu ambacho kilikuwa kinamuumiza sana Jurgen Klopp.

Ndiyo maana aliamua kutoa pesa yake kwa ajili ya kupata huduma bora ya Van Djik. Hapo ndipo akaanza kutoka taratibu kwenye imani ya kutotumia pesa kubwa kwenye biashara ya wachezaji.

Rasmi akaanza kuamini kwenye kutumia pesa nyingi ili kupata huduma bora. Na inawezekana hata kombe la klabu bingwa barani ulaya msimu Jana angechukua.

Lakini makosa binafsi ya golikipa yake yaliwagharimu sana , na hapo ndipo ukawa mwanzo wa yeye kuingia sokoni tena kwa ajili ya kutafuta golikipa.

Ndipo hapo aliushangaza ulimwengu kwa kutumia pesa kubwa kwa ajili tu ya golikipa. Kitu ambacho kilikuwa kigeni kwa Jurgen Klopp.

Leo hii Liverpool inamefuzu kwenda hatua inayofuata kwa sababu ya mikono ya Allison. Inawezekana Salah alifunga goli, lakini ile save ya mwisho ya Allison ndiyo iliokoa maisha ya Liverpool.

Leo hii Liverpool siyo mufu tena kwa sababu tu Allison aliwapa pumzi ya ziada kipindi ambacho walikuwa wanaelekea kufa.

Liverpool wako pale kwa sababu waliamua kutumia pesa ili kupata huduma bora, hawakuwa mabahiri, walikuwa na nia ya kufanya vizuri.

Ni ngumu sana kwa mpira wa sasa kufanya vizuri kama huna msuli kwenye soko la wachezaji, inawezekana Jurgen Klopp alikuwa anapingana nalo hili ila kwa sasa ndiye mhubiri mkubwa wa injili hii ya kutumia fedha nyingi kwenye usajili.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Kwanini Liverpool atashinda dhidi ya Napoli ?

Tanzania Sports

Kurasa za kitabu cha LIVERPOOL zinamsubiri KLOPP