in , ,

Kurasa za kitabu cha LIVERPOOL zinamsubiri KLOPP

Kurasa za kitabu cha LIVERPOOL zinamsubiri KLOPP

Makocha tisa wamepita kabla yake, kila kocha alikuwa na kazi moja tu nayo ni kurudisha hadhi ya klabu ya Liverpool katika ligi kuu ya England.

Hii ndiyo klabu ambayo Waingereza walikuwa wanajivunia sana kwa sababu tu ilikuwa na mafanikio makubwa sana ndani ya uwanja kuliko klabu yoyote.

Waliita PROUD OF ENGLAND, hii ni kuonesha ni jinsi gani ambavyo walikuwa wanajivunia kuwa na Liverpool katika ardhi ya England.

Ndiyo maana ni moja ya klabu ambayo ina mashabiki wengi zaidi nchini England. Na hii ni kwa sababu tu waliwahi kuwa tishio kipindi cha nyuma.

Hakuna ambaye aliweza kuwatingisha kwenye utawala wao mpaka pale Sir. Alex Ferguson alipokuja kuvunja utawala wao na kuwake utawala wa Manchester United.

Walitoka tena kwenye kilele cha kuongoza kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya England mara nyingi zaidi. Manchester United wakachukua nafasi yao na wao wakabaki wanawatazama tu Manchester United kwa hasira.

Walikuja makocha tisa awali, kila kocha alitamani kuipa nafasi Liverpool kuchukua tena ligi kuu ya England lakini hakuna aliyefanikiwa.

Inawezekana kama siyo makosa ya nahodha anayeheshimika zaidi kwenye klabu hiyo Steven Gerald basi Brendan Rodgers angeipa ubingwa Liverpool.

Lakini ilikuwa totafuti na matazamio ya wengi, Liverpool alishika na nafasi ya pili baada ya kuonekana muda mrefu kuwa ana uwezo mkubwa wa kuchukua ubingwa.

Maumivu yakawatala tena , wakaamini kupitia kesho yao lakini kesho yao ilikuwa mbovu tena. Wakakosa uwezo tena wa kushindana kwa nguvu tena.

Na hii ilionesha dhahiri kuwa Brendan Rodgers alikuwa anabebwa zaidi na Luiz Suarez, baada ya kuondoka kwake Liverpool ilibaki mpweke tena.

Ikaanza kuhangaika tena , uwezo wa kushindana ukapungua tena kwa kiasi kikubwa. Hali ambayo ilimfanya Brendan Rodgers awe na maisha mafupi ndani ya Liverpool.

Leo hii wanaye Jurgen Klopp, anaaminika ni moja wa makocha bora sana duniani kwa sasa. Ni kocha wa kisasa ambaye anauwezo mkubwa wa kuendana na mbinu za kisasa.

Ni kocha ambaye aliwahi kusimamisha utawala wa Bayern Munichen nchini Ujerumani akiwa na bajeti ndogo sana kwenye mfuko wake.

Alikusanya vipaji, akavifanya vipaji viwe na uwezo wa kuupenda mpira, kupenda mafanikio na kuvifanya vicheze kwa moyo sana.

Ndiyo maana kwa kipindi cha Jurgen Klopp , Borrusia Dortmund iliweza kushindana sana na Bayern hata kwenye ligi ya mabingwa barani ulaya iliweza kushindana na vigogo wa ulaya.

Ikawa moja ya timu tishio, timu ambayo ilikuwa inaogopeka sana duniani. Wengi walikuwa hawatamani kukutana na Borrusia Dortmund ya Jurgen Klopp kwa kipindi hicho.

Taratibu Jurgen Klopp ameanza kujitengenezea U-Borrusia Dortmund kwenye kikosi cha Liverpool kwa sasa. Ameanza kutengeneza timu ambayo ni imara.

Msimu jana alifika fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya, kilichomwangusha ni safu mbovu ya ulinzi ya timu yao.

Leo hii ana safu imara ya ulinzi safu ambayo mpaka sasa hivi ina cleansheets 12 katika michezo 23 waliyocheza katika michuano yote.

Na katika ligi kuu ya England wana Clean sheets 10 na wamefungwa magoli 6 tu na ni timu ambayo imefungwa goli chache kuzidi timu zote.

Taratibu Jurgen Klopp ametengeneza silaha kubwa. Silaha ambayo mara zote huwa ni muhimu sana katika mbio za ubingwa kwa timu yeyote.

Silaha ambayo inaweza kusababisha kitabu cha kumbukumbu cha Liverpool kimwandike kama mtu shujaa na muhimu.

Mtu ambaye ameleta tabasamu lililopotea baada ya miaka 26, miaka 26 hawajashinda ligi kuu ya England. Hiki ndicho kitu ambacho wengi wanakitamani sana.

Na ndicho kitu ambacho kitamletea sifa kubwa sana Jurgen Klopp na Liverpool itakumbuka utawala wake kila uchwao.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Mikono ya Allison inazidi kumuumbua Klopp

Serengeti boys

Tumkumbuke MALINZI na SERENGETI BOYS yake