in ,

Tumkumbuke MALINZI na SERENGETI BOYS yake

Serengeti boys

Inawezekana muda huu amepata marafiki wapya sana. Marafiki ambao wanawaza tofauti kabisa na marafiki ambao alikuwa nao huku.

Kuna utofauti mkubwa sana wa maisha ya sasa na ya zamani. Kwa sasa amezungukwa na jamii ambayo ina waza kitu kimoja tu.

Kila anapogeuka kushoto, akitazama kulia, akatazama mbele na kurudi kutazama nyuma kila uso anaokutana nao unazungumza lugha moja tu.

Hakuna uso ambao una lugha mbili, kila uso una lugha moja tu nayo ni jinsi ya kutoka sehemu ambayo wapo. Sehemu ambayo wengi wanaichukia kuwepo.

Sehemu ambayo haina Uhuru mkubwa tofauti na sehemu ambayo walikuwepo awali. Inawezejana awali walikuwa wanapanga vingi sana kwa Uhuru.

Kuna wakati walipanga namna ambavyo wangeweza kwenda kushuhudia kombe la dunia nchini Russia.

Kuna wakati inawezekana kabisa Jamal Malinzi alikuwa anawaza namna ambavyo angeweza kuifanya nchi yetu iweze kuandaa Afcon.

Hii ni mipango ambayo alikuwa akiipanga nyakati anbazo yuko huru, nyakati ambazo kichwa chake amekipa nafasi ya kuwaza vyema.

Nyakati ambazo alikuwa anaweza kuwaza vyema hata akiwa kwenye gari lake , ofisini kwake au chumbani akiwa na mke wake.

Kwa kifupi alikuwa na nafasi kubwa ya yeye kuwaza vyema nyakati za nyuma kwa sababu tu alikuwa huru tofauti na kipindi hiki.

Kipindi ambacho akili yake inawaza kutoka kwenye matatizo yake binafsi. Nyakati ambazo akili yake inawaza kutoka nyuma ya nondo.

Hana kingine kikubwa zaidi ya hiki. Anawaza ni namna gani aweze kutoka akutane na marafiki, jamaa na familia yake.

Hana tena wakuwaza mipango ya maendeleo ya mpira wetu kama ambavyo alifanya mwanzoni.

Mwanzoni alitumia muda mwingi sana kuwaza namna ambavyo angefanya kitu ambacho kingekuwa alama katika kumbukumbu zetu.

Alitufanikishia timu yetu ya chini ya umri wa miaka 17 ifuzu Afcon nchini Gabon mwaka uliopita huku mkononi mwake akiwa na ticketi ya kuandaa michuano hiyo ya Afcon ya vijana waliochini ya miaka 17 mwakani.

Hakuwaza kuwa na ticketi pekee kama ndicho kitu ambacho kinatosha ili kufanikisha hili. Aliwaza namna ambavyo angeweza kutengeneza timu ambayo ingekuwa na ushindani kwenye michuano ambayo tutaiandaa sisi.

Aliamua kuandaa kikosi kungine bora ambacho kingekuja kuwarithi kina Yohana Nkomola na kina Ramadhan Kabwili.

Aliamua kuchukua vijana wenye umri chini ya miaka 15 na kuwaweka kambini kwa muda mrefu kwenye shule ya Alliance.

Waliweza kupata muda wa kufanya mazoezi kwa pamoja huku wakisoma masomo yao ya kawaida. Aliwaza mbali sana.

Aliona nchi yake itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo ya Afcon ya mwaka 2019 ndiyo maana akaamua kutumia muda mrefu kuandaa vijana ambao walikuwa na uwezo wa kushindana haswaa.

Alifanikiwa kwenye hilo tena kwa kiwango kikubwa kwa sababu jeshi ambalo ameliacha kwa sasa ni jeshi lenye wanajeshi wenye mafunzo mazuri ya kivita.

Wanapambana sana kila aina ya vita, na wamekuwa washindani haswaa na kuna vita ambazo wamekuwa wakishinda kwa ushindi mkubwa.

Leo hii tunajivunia hawa vijana wa Serengeti Boys kwa kiwango ambacho wanakionesha katika michezo mbalimbali ambayo wamecheza.

Pamoja na kwamba tunajivunia sana, lakini tunashindwa kutoa shukurani kwa mtu ambaye aliwaza namna ya kuwatengeneza hawa ili waje kulipa sifa taifa.

Inawezekana muda huu Jamal Malinzi hajabahatika kuwaona hawa vijana na anakomea kuwasikia tu kwa mbali kuhusiana na matokeo mazuri wanayoyapata.

Lakini mwisho wa siku hii timu inabaki kama zawadi pekee kubwa ambayo Jamal Malinzi alituachia ingawa wengi wetu hatutaki kuitambua kama ni zawadi kutoka kwake.

Acha leo hii awaze namna ya kutoka sehemu ambayo yupo, lakini dunia inamkumbuka kwenye hili. Amefanikiwa kuleta zawadi kubwa duniani.

Amefanikiwa kuwaibua kina Kelvin John ambao wengi wanawasifia kwa vipaji vyao. Mikakati yake ndiyo iliyowapa nafasi kubwa kina Kelvin John Leo hii kuwepo sehemu ambayo wapo.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Kurasa za kitabu cha LIVERPOOL zinamsubiri KLOPP

Tanzania Sports

Makocha wanaofaa kuchukua nafasi ya JOSE MOURINHO