in , , ,

MIKEL OBI ANAIKATAA HESHIMA

 

Kesho Jumamosi timu ya Taifa ya Nigeria itakipiga dhidi ya Taifa Stars kwenye Uwanja a Taifa jijini Dar-es-salaam. Huu ni mchezo wa Kundi G wa michuano ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017. Jina la John Mikel Obi halimo kwenye kikosi cha wachezaji wa Nigeria walioitwa na kocha Sunday Oliseh kwa ajili ya mchezo huo.

Oliseh amemuacha Obi kwa kuwa kocha huyo alishasema wazi kuwa kwenye timu yake ataita wachezaji wanaopata nafasi ya kutosha ya kucheza kwenye klabu zao na kuonyesha uwezo. Ni wazi kuwa Obi si mmoja wa wachezaji wanaopata nafasi ya kutosha ya kucheza kwenye klabum kwa sasa.

Kocha Jose Mourinho amekuwa akiwatumia Nemanja Matic na Cesc Fabregas kwenye nafasi ya kiungo katika timu ya Chelsea huku Ramires akibakia kuwa chaguo mbadala  iwapo mmoja wa viungo hao anakosekana. Hili ndilo linalomnyima Mikel Obi nafasi ya kucheza mfululizo Chelsea.

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza kuwa ni kwanini Obi hataki kuondoka Chelsea. Miezi kadhaa iliyopita Mikel Obi alikuwa akihusishwa na kuhamia Besiktas, Galatasaray na klabu nyingine kadhaa. Lakini alikanusha kwa kusema kuwa hayupo tayari kuhama kwa kuwa kocha bado anamuhitaji.

Inashangaza kwa kweli. Inashangaza kumsikia Obi akijinadi kuwa eti anahitajika na Jose Mourinho kwa sababu msimu uliopita mchezaji huyo alipata nafasi ya kuanza kwenye michezo minne tu kati ya michezo yote ya Ligi Kuu ya England. Na msimu huu amepata nafasi ya kucheza mchezo mmoja tu kati ya minne ya EPL tena aliingia kwenye dakika ya 84.

Kiuhalisia Mourinho na Chelsea  hawamuhitaji Obi Mikel ila tu ni yeye mwenyewe anayeng’ang’ania kubakia Chelsea wakati timu kadhaa zimekuwa zikihitaji huduma yake.

Ana umri wa miaka 28 hivyo bado ana nafasi ya kung’ara kwenye klabu nyingine za Ulaya na aweze kupata nafasi ya kuchezea timu ya taifa pia ambapo naamini panaweza kumjengea heshima kubwa nyumbani kwao Nigeria kama aliyowahi kuipata Jay Jay Okocha na nyota wengine.

Obi halioni hili. Yupo tayari kuendelea kusugua benchi Chelsea mbaka mkataba wake utakapoisha mwezi Juni 2017. Ameshatwaa karibu kila kombe akiwa na Chelsea. Ametwaa taji la EPL mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja na mengine ya kutosha akiwa Stamford Bridge. Hana chochote kigeni anachoweza kushinda akiwa Stamford Bridge.

Kuing’ang’ania Chelsea kunamfanya apoteze heshima kubwa ambayo alishaonyesha mwanga wa kuipata tangu alipokuwa kijana mdogo wa miaka 18. Akiwa na umri huo Obi aliiongoza Nigeria kufika fainali ya Kombe la Dunia la vijana wenye umri chini ya miaka 20 mwaka 2005.

Walipoteza fainali hiyo dhidi ya Argentina. Obi Mikel akatwaa tuzo ya ‘Mpira wa Fedha’ kama mchezaji bora wa pili wa michuano hiyo nyuma ya Lionel Messi aliyetwaa ‘Mpira wa Dhahabu’ kama mchezaji bora wa michuano hiyo.

Wengi wakamtabiri kuwa angekuja kuwa mrithi wa Jay Jay Okocha na kujijengea heshima kubwa nyumbani kwao Nigeria. Obi akiwa angali kijana mdogo nyota yake iling’aa zaidi pale Chelsea na Manchester United walipokuwa wakigombania kumsajili mbaka kufikia kushitakiana.

Hayo yote yalimfanya atabiriwe kuja kujijengea heshima kubwa Nigeria na Afrika nzima. Heshima hii ingekuja tu kama angepata nafasi ya kuichezea timu yake ya taifa kwa muda mrefu zaidi. Anaikosa nafasi hii kutokana na kung’ang’ania kusugua benchi Chelsea. Mikel Obi anaikataa heshima yeye mwenyewe.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KUFUZU EURO 2016:

Tanzania Sports

England usajili wa tsunami