Nimemtazama kocha mpya wa Simba, Pablo Franco na kikosi chake cha Simba kikipambana na watandaza soka la burudani Ruvu Shooting. Katika mchezo huo uliochezwa wikiendi, Simba waliibuka na ushindi wa mabao matatu dhidi ya moja la Ruvu Shooting.
Katika makala TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu katika mchezo huo ulikuwa wa kasi na kusisimua wapenzi wa soka kutoka dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mosi, Bernard Efua Morrison anakuwa mchezaji wa kwanza wa Simba kulimwa kadi ya njano chini ya kocha mpya Pablo Franco. Morrison alilimwa kadi hiyo baada ya kumlalamikia mwamuzi Ahmed Araragija kutokana na kumtima penati kwa kile alichodai kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.
Pili, Meddie Kagere amekuwa mchezaji wa kwanza wa Simba kupachika bao chini ya kocha mpya Pablo Franco. Lakini vilevile Meddie Kagere anakuwa mchezaji wa kwanza kupachika mabao mawili chini ya kocha huyo mpya.
Tatu, Erasto Nyoni anakuwa mcheaji wa kwanza wa Simba kukosa penati chini ya kocha mpya. Nyoni alikosa penati hiyo baada ya kupanguliwa na kipa wa Ruvu Shooting, Mohamed Makaka.
Nne, Kibu Dennis anakuwa mchezaji wa kwanza wa Simba chini ya kocha mpya kutengeneza mabao mawili ya timu yake na kufunga moja. Kibu alicheza kwa sehemu kubwa ya mchezo huo ikiwa na maana kocha wake Pablo Martin alikubali uwezo wake na uwajibikaji uwanjani.
Tano, Ruvu Shooting inakuwa timu ya kwanza kumfunga bao kocha mpya kupitia nyota wao Elias Maguli katika dakika 63. Ruvu walifunga bao hilo katika dakika za mwisho za mchezo lakini halikutosha kuwapa pointi tatu licha ya kuwa wenyeji wa mchezo huo kwenye uwanja wa Mwanza. Bao hilo lilifuta rekodi ya nyanda wa Simba, Aishi Manula ya kutofungwa tangu Ligi Kuu ya NBC ilipoanza msimu huu.
Sita, kikosi cha Simba chini ya Pablo Franco Martin kinaonekana kucheza kwa kasi na kutumia pembeni kama sehemu ya kupitisha mashambulizi kuelekea langoni mwa adui. Simba walionesha mchezo mzuri dhidi ya Ruvu Shooting lakini kadiri muwa ulivyokuwa unakwenda walikuwa wamepunguza kiasi kikubwa uwezo wao wa kushambuliaji na kujilinda. Mpangilio wa bao la kufutia machozi la Ruvu Shooting ni kielelezo kuwa Simba wana kazi ya kufanya ili kuzuia madhara zaidi.
Saba, ushindani wa namba ndani ya kikosi cha Simba umeonkana dhahiri, lakini kikwazo kikubwa cha wachezaji wake huenda kikawa ni umri. Baadhi ya wachezaji wakubwa wanaonekana kuwa na umri mkubwa ambao huenda ukawa kikwazo kwa kuendana na kasi ya mbinu za Pablo Franco Martin.
Nane, kocha wa Simba ana mechi mbili za kuisoma Yanga kabla ya kupepetana nayo Desemba 11. Pablo Franco atakuwa ameitazama Yanga iliyocheza dhidi ya Namungo wikiendi hii na kisha ataiona itakapocheza na Mbeya Kwanza jijini Mbeya.
Tisa, kocha wa Simba ana kibarua kizito kuiandaa timu hiyo kucheza Kombe la Shirikisho pamoja na mchezo wao dhidi ya watani wa jadi Yanga. Simba kwa vyovyote vile wanatakiwa kuibuka na ushindi ili kuzima ngebe za Yanga ambao wawaliwafunga watani hao katika mchezo wa Ngao ya Jamii. Na sasa ni wakati wa Simba kulipa kisasi kwa Yanga, na mtu sahihi wa kufanya kazi hiyo sasa ni Pablo Franco Martin.
Kumi, katika mchezo dbidi ya Ruvu Shooting, safu ya ulinzi ya Simba ilionesha dalili za kurejesha makai yao ya kuanzisha mashambulizi. Kwenye mchezo huo Joash Onyango alikuwa beki anayeamuru mashambulizi zaidi kutokana na pasi zake ndefu kuelekea langoni mwa adui. Vile Aishi Manula ameonekana kubadilika na kuanza kuchota ujuzi wa wa golikipa wa Yanga, Djigui Diarra ambaye ni fundi wa kupiga pasi ndefu zinazozaa mabao.
Kwa ujumla hii ni mechi ya kwanza kwa Pablo Franco ambayo tunaweza kusema mambo bado hayajatengamaa kwa sababu hawajakutana na timu yenye ushindani mkubwa kama Yanga au Azam chini yake. katika mechi yenye presha kubwa ndiyo ambayo itafafanua zaidi utulivu na ufanisi wa kocha huyo.
Comments
Loading…