Liverpool wamezidi kupata pigo baada ya mlinzi wao, Martin Skrtel kupigwa marufuku kucheza mechi tatu.
Skrtel amepoteza rufaa aliyokata mbele ya jopo huru lililosikiliza suala lake la nidhamu akipinga mashitaka kwamba alimrukia na kumkanyaga kwa makusudi golikipa wa Manchester United, David De Gea.
Mchezaji huyo wa Slovakia alitenda kosa hilo Jumapili ya juzi sekunde za mwisho katika mechi baina ya Liverpool na Manchester United.
Mwamuzi Martin Atkinson hakuona kitendo hicho lakini alishuhudia wachezaji wawili hao wakizozana na kuwatenganisha muda mfupi baadaye.
Hili ni pigo la pili kwa Liverpool, kwani nahodha wao, Steven Gerrard alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwenye mechi hiyo kwa kumkanyaga mchezaji wa United, Andre Herrera katika kulipiza kisasi baada ya kuchezewa rafu.
Gerrard alikuwa ameingia sekunde 38 tu akitokea benchi na yeye atakosa mechi tatu katika hatua muhimu inayofuata kwa ajili ya kutafuta nafasi kwa timu hiyo kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu ujao.
Skrtel (30) amedai kwamba hakufanya makusudi kumkanyaga kipa huyo, lakini alionekana akizozana naye lakini mbaya zaidi baada ya kupewa adhabu ameweka vikaragosi vitatu vikicheka kwenye mtandao wake.
Kwa uamuzi huo, ina maana kwamba Skrtel atakosa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Arsenal Aprili 4 April na dhidi ya Newcastle Aprili 13. Kadhalika ataikosa mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Blackburn MAprili 8.
Viongozi wa Liverpool wamekataa kuzungumzia uamuzi huo. Liverpool wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, wakiwania nafasi nne za juu zinazoshikiliwa na Chelsea, Manchester City, Arsenal na Manchester United.
Comments
Loading…