*Spurs, Hull, Villa washinda
Tambo za ushindi mnono kwenye mechi zote za kujiandaa na msimu zimeishia Old Trafford, baada ya Manchester United kuvunja rekodi kwa kupoteza mechi ya kwanza ya msimu wa ligi nyumbani, ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1972.
Zama za kocha mpya, Lous van Gaal kwenye ngome yao zimeanza vibaya, baada ya vijana wake kukubali kichapo cha 1-2 kutoka kwa Swansea, kitu ambacho mashabiki wengi kati ya 75,339 waliohudhuria hawakutarajia.
Kadhalika rekodi nyingine iliyowekwa ni kwa Swansea kushinda mechi ya kwanza ya ligi kwenye dimba hilo tangu 1931, ambapo siku ilianza kwa kocha huyo Mdachi kupokewa kwa nderemo na vifijo.
Washabiki wengi wa United walimtarajia awasahaulishe haraka zama za David Moyes aliyeharibu msimu uliopita kwa kuwafanya United kumaliza katika nafasi ya saba, hivyo kukosa michuano yote ya soka la kimataifa msimu huu.
Mashetani Wekundu hawakuweza kufurukuta mbele ya vijana wa Garry Monk, ambapo wenyeji walionekana kutocheza kama timu, ambapo Van Gaal aliwaanzisha wachezaji wawili kutoka akademia yao -Tyler Blackett na Jesse Lingard. Kiungo Ander Herrera ndiye mchezaji pekee mpya aliyecheza, na alionesha mchezo mzuri.
Ki Sung-yueng alianza kuwatia matumbo joto United kwa kupachika bao la kwanza dakika ya 28 baada ya ngome ya United kuyumba, lakini nahodha mpya wa Man U, Wayne Rooney alisawazisha baada ya kuhaha kwa muda kutimiza kazi hiyo.
Hata hivyo, maji yalizidi tena unga baada ya Gylfi Sigurdsson, raia wa Iceland kupachika bao la pili dakika ya 72 na hapakuwapo na lolote la maana kutoka United kuweza kufanyika ili walau waambulie sare, licha ya Van Gaal na msaidizi wake, Ryan Giggs kuteta na kujaribu kubadili mchezo.
Matokeo hayo yanawakumbusha United machungu ya kufungwa na Swansea msimu uliopita kwenye uwanja huo huo na kufurushwa kwenye michuano ya Kombe la FA ambalo hatimaye lilitwaliwa na Arsenal.
Ni wachache walitarajia Swansea kufanya kweli, hasa baada ya kuuza walinzi wao, Chico Flores na Ben Davies, huku Michu akipelekwa kwa mkopo Napoli. Van Gaal alitumia mfumo aupendao wa 3-4-1-2 lakini mambo yakachacha.
MATOKEO MENGINE
Katika mechi nyingine zilizochezwa Jumamosi hii, Leicester walichomoa dakika za mwisho na kwenda sare ya 2-2 na Everton wakati Queen Park Rangers (QPR) walilala 0-1 nyumbani kwao walipocheza na Hull.
Aston Villa waliwapelekesha wenyeji wao, Stoke kwa kuwafunga 1-0 wakati West Bromwich Albion waliowakaribisha Sunderland walitoshana kwa sare ya 2-2 huku West Ham wakicheza nyumbani walilala kwa Tottenham Hotspur kwa 1-0.
Kadi nyekundu ya kwanza msimu huu ilikwenda kwa Kyle Naughton wa Spurs dakika ya 28 baada ya kushika mpira kwenye eneo la hatari. Mwamuzi Chris Foy ameanza msimu kwa zawadi ya kadi nyekundu, kwani katika dakika ya 62 alimlima James Collins wa West Ham kwa mchezo mbaya dhidi ya Emmanuel Adebayor. West Ham watajilaumu kwa kukosa penati iliyopigwa hovyo na Mark Noble.
Comments
Loading…