*Spurs nao hoi kwa West Brom
Manchester United bado wamekaa vibaya, kwani wameogeshwa kichapo cha mabao 5-3 na Leicester City.
Vijana wa Louis van Gaal walidhani walishajiweka sawa walipokuwa mbele kwa mabao 3-1, lakini wenyeji hawakukata tamaa na kupambana hadi wakasawazisha na kuongeza mawili ya ziada.
Wakichezesha wachezaji maarufu kama Wayne Rooney, Angel Di Maria, Radamel Falcao, Daley Blind, Ander Herera na wengineo, Mashetani Wekundu walipigishwa kwata na pia kupata pigo dakika ya 82 kwa beki wao Tyler Blackett kupewa kadi nyekundu kwa rafu mbaya ndani ya eneo la penati.
Mabao ya Manchester United yalifungwa na Van Persie, Herera na Di Maria wakati yale ya Leicester yalifungwa na Leonardo Ulloa, David Nugent kwa penati, Esteban Cambiasso akasawazisha mambo kabla ya Jamie Vardy na Ulloa tena kusakafia ushindi, ngome ya Man U ikionekana kubomoka.
Hiki ni kichapo cha pili kwa Man U, baada ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Swansea, wakaenda sare mbili na kushinda moja tu dhidi ya Queens Park Rangers (QPR) wikiendi iliyopita.
Leicester wanakuwa timu ya sita katika historia ya EPL kuweza kuwafunga United mabao matano au zaidi.
SPURS WAANGUKIA PUA
Tottenham Hotspur wamekubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa West Bromwich Albion waliokuwa mkiani mwa ligi kabla ya mechi hiyo.
Bao la West Brom lilifungwa na mchezaji wa kimataifa wa Scotland, James Morrison katika nusu ya pili ya mchezo na huu ni ushindi wa kwanza nyumbani kwa Spurs katika kipindi cha miaka 30.
Ni ushindi ambao ulikuwa dhahiri kwa Baggies ambao wachezaji wao, Saido Berahino na Craig Gardner walicheza vyema na kukaribia kufunga. Spurs walichanganywa na uchezaji maridadi wa beki wa kati, Joleon Lescott na mshambuliaji wao, Roberto Soldado nusura aokoe jahazi lakini shuti lake lilidakwa.
Comments
Loading…