Hongera sana!
Arsenal kuwapigia saluti jumapili
Manchester United wametwaa taji la ubingwa wa England, baada ya kufikisha pointi 84 zisizoweza kufikiwa na timu nyingine.
Usiku wa Jumatatu hii, bendera za mabingwa zilishaanza kusambazwa na kuuzwa mitaani, ikiwa ni pamoja na nje ya dimba lao la Old Trafford.
Katika mechi waliyokamia kwenye uwanja wao wa Old Trafford dhidi ya Aston Villa, United walianza kwa hasira na kuhakikisha hadi nusu ya kwanza wanaongoza kwa mabao matatu kwa nunge.
Kocha Alex Ferguson alisema tangu awali kwamba hawangedharau tena mechi walizo nazo mkononi, na Jumatatu hii aliingiza kikosi kizito, wakiwamo Robin van Persie, Wayne Rooney, Shinji Kagawa, Rooney akichezeshwa eneo geni la kiungo, akafurukuta.
Aliyeng’aa na kulielekeza kombe la 20 Old Trafford alikuwa mchezaji namba 20, RVP aliyesajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 25 kutoka Arsenal msimu huu.
Ndiye alifunga mabao yote ya kipindi cha kwanza, akimaliza ukame wa mabao kwa muda mrefu, alioanza kuufuta kwa bao la tuta mechi iliyopita.
Uchukuaji wa haraka wa kombe ulianza kujengewa mazingira na mahasimu jirani wao waliokuwa mabingwa watetezi, Manchester City, waliokubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Tottenham Hotspurs Jumapili hii.
Wakati kocha Roberto Mancini akisema mechi hiyo dhidi ya Spurs ilikuwa kioo cha jinsi walivyocheza hovyo msimu huu, Emmmanuel Adebayor alisema kabla kwamba City si wazuri ugenini, na wangeanza kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Kwa hali ilivyo, Manchester City wakiendeleza ulegelege wanaweza wasiipate hata nafasi ya pili, kwa sababu Arsenal, Chelsea na Spurs wanakuja kwa kasi. City wana pointi 68, Arsenal 63, Chelsea 62 na Spurs 61.
Sherehe za ubingwa wa Manchester United zilianza mapema Jumatatu hata kabla mechi haijaanza, na RVP na wenzake wakazikoleza kwa mabao ya haraka, ikiwa ni hat trick ya haraka zaidi katika kipindi cha miaka tisa.
Hata hivyo, kipindi cha pili kilikuwa na ukame, na si RVP, wenzake wala wapinzani wao waliofaulu kutikisa tena nyavu, lakini yote kwa yote, United wameanza sherehe zao.
RVP mwaka jana alikuwa mfungaji bora wa EPL, na mwaka huu anaelekea huko tena, hasa baada ya Luis Suarez kufanya makosa ya kumng’ata mchezaji, hivyo kutarajiwa kukosa mechi kadhaa zijazo.
Manchester United ilianzishwa 1878, lakini wakati huo ilikuwa ikitumia jina la Newton Heath LYR, ikaja kuitwa Manchester United 1902 na kuanza kutumia dimba la Old Trafford.
Licha ya makombe 20 ya EPL waliyofikisha Jumatatu hii, Man U wametwaa Kombe la FA mara 11, Kombe la Ligi mara nne na Ngao ya Jamii mara 19.
United pia wametwaa mara tatu makombe ya Ulaya, moja Kombe la Washindi la UEFA, Super Cup ya UEFA na Kombe la Dunia la Klabu la FIFA.
Msimu wa 1998–99, United walitwaa vikombe vitatu – Trebble – navyo ni vya EPL, FA na katika LIgi ya Mabingwa ya UEFA, ambayo haijapata kutokea kwa klabu ya England.
Mwaka 1958 United walipata ajali ya ndege huko Munich, ambapo wachezaji wanane walipoteza maisha yao. Mwaka 1968, chini ya uongozi wa Matt Busby, Manchester United walikuwa klabu ya kwanza ya England kutwaa kombe la Ulaya.
Kocha wa sasa, Ferguson ametwaa mataji 24 tangu ajiunge nao Novemba 1986.
United ni moja ya klabu tajiri zaidi duniani na zenye washabiki wengi hata katika nchi za pembezoni. Januari mwaka huu ilitokea kuwa klabu ya kwanza duniani kukadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni tatu. Jarida la Forbes linaikadiria klabu hiyo kuwa na thamani ya dola bilioni 3.3.
Mwaka 1991 waliingizwa kwenye Soko la Hisa la London na Mei 2005 dili lilifikiwa la kiasi cha pauni milioni 800, na familia ya Malcolm Glazer ikawanunua Manchester United.
Agosti mwaka jana Manchester United waliingia kwenye Soko la Hisa la New York, Marekani, lakini hawakufanya vizuri.
Kama Aston Villa wangewafunga United, basi Queen Park Rangers (QPR) na Reading wangeshushwa daraja rasmi, lakini kwa vile imeshindikana, atakayefungwa Jumapili timu mbili hizo zinapocheza atashuka daraja. Aston Villa wapo nafasi ya nne kutoka chini, hivyo wanatakiwa kutia jitihada kushinda ili kujiondoa eneo la hatari.
Comments
Loading…