in , ,

RAIS TENGA ATOA MIPIRA YA DOLA 30,000

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa
mipira zaidi ya 1,200 yenye thamani ya dola 30,000 za Marekani kwa vyama
vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na vituo 21 vilivyo hai vya
kuendeleza vijana (academies).

* *

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) lilimpa Rais Tenga fedha
hizo ikiwa ni shukrani kwake kwa kushughulikia mgogoro wa uongozi wa mpira
wa miguu nchini Kenya uliodumu kwa miaka miwili; ambapo nchi hiyo kutokana
na mgogoro huo ilikuwa na vyama viwili (KFF na FKL).

* *

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mipira hiyo kwenye ofisi za TFF, Dar
es Salaam leo (Aprili 22 mwaka huu), Rais Tenga amesema amefanya hivyo kwa
vile anaamini kuwa mipira ndiyo kitu muhimu katika kuinua mchezo huo mahali
popote.

* *

“Dhamira yangi si kushukuru kwa hafla hii, bali kutoa sababu kwa nini
nimefanya hivi. Ninaamini kwa kuanzia mipira ndiyo muhimu, pili kwa kufanya
hivi itaonekana kweli mipira imegawiwa,” amesema Rais Tenga.

Amesema  mpira wa miguu kwa Tanzania unahitaji sana watu wa
kujitolea, na yeye amefanya hivyo kwa kujitolea kutokana na ukweli shughuli
anazotumwa na FIFA ni za kujitolea.

* *

Rais Tenga ambaye pia alitumwa na FIFA kutatua matatizo ya uongozi wa mpira
wa miguu katika nchi za Uganda, Zambia na Sudan Kusini amesema anaamini
anapata fursa hizo kutokana na kuwa kiongozi wa TFF, na kwa kuwakumbuka
waliomchagua ndiyo maana hakusita kupeleka fedha hizo kwenye mipira.

Amesema moja ya ndoto zake wakati anaingia kuongoza TFF mwaka 2004
ameshindwa kutimiza ni kusaidia mipira, kwani uwezo wa kununua mipira kwa
wanaocheza katika ngazi ya chini hasa watoto haupo.

“Hizi kelele zote za maendeleo ya mpira wa miguu ni kwa sababu shuleni
hakuna vifaa. Nia yangu ilikuwa shule zote zipate mipira, lakini hiyo ni
moja ya ndoto nilizoshindwa kutekeleza. Vipaji haziwezi kupatikana kama
watoto hawachezi.

“Tunashukuru sana kwa Serikali kurejesha mpira shuleni. Hata nitakapoondoka
madarakani nikipata nafasi nitaendelea kuomba mipira kwa ajili ya shule,”
amesema Rais Tenga.

Vyama vya mikoa ambavyo jumla ni 32 (Tanzania Bara na Zanzibar) kila kimoja
kimekabidhiwa mipira 25 (kumi saizi namba tano, 15 saizi namba nne kwa
ajili ya vijana). Kwa academies ambazo ni 21 kila moja imepewa mipira 25
(minane saizi namba tano, na 15 saizi namba nne).

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Almasi Kasongo, Katibu wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) Nassib Mabrouk na Katibu wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Riziki Majala.

Kwa upande wa shule alikuwa Kanali mstaafu Idd Kipingu ambaye ni mmiliki wa
shule ya Lord Baden ya Bagamoyo mkoani Pwani.

* *

*COASTAL, AZAM KUCHEZA SIKU YA MUUNGANO*

Timu za Coastal Union ya Tanga na Azam zitapambana Aprili 26 mwaka huu
katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) itakayofanyika kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.

Awali mechi hiyo namba 168 ilikuwa ichezwe Aprili 27 mwaka huu, lakini
imerudishwa nyuma kwa siku moja ili kuipa fursa Azam kujiandaa kwa mechi ya
marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya
Morocco.

Mechi hiyo itachezeshwa na Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani akisaidiwa na
Abdallah Mkomwa (Pwani), Vicent Mlabu (Morogoro) wakati mwamuzi wa mezani
atakuwa Mohamed Mkono wa Tanga. Charles Komba wa Dodoma ndiye atakayekuwa
Kamishna wa mechi hiyo ya raundi ya 24.

Baada ya mechi ya Tanga, Azam itarejea Dar es Salaam siku inayofuata tayari
kwa safari ya kwenda Rabat itakayofanyika Aprili 28 mwaka huu. Mechi hiyo
itachezwa wikiendi ya Mei 3, 4 au 5 mwaka huu.

Keshokutwa (Aprili 24 mwaka huu) kutakuwa na mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom
kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Dar
es Salaam.

Iwapo Azam itafanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho
kutakuwa na marekebisho ya ratiba ya VPL. Hiyo ni kutokana na raundi
inayofuata ya Kombe la Shrikisho kuchezwa wikiendi ya Mei 17, 18 na 19
mwaka huu ambapo bado haijajulikana Azam itaanzia wapi (nyumbani au
ugenini) iwapo itavuka.

Mechi nyingine za VPL mwezi ni Aprili 25 (Ruvu Shooting vs Simba- Uwanja wa
Taifa), na Aprili 28 (Simba vs Polisi Morogoro- Uwanja wa Taifa).

*MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI*

Kocha Mkuu wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim
Poulsen atakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (Aprili 23 mwaka
huu).

Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

*WAMOROCCO WA AZAM WAINGIZA MIL 50/-*

Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na AS
FAR Rabat ya Morocco iliyochezwa juzi (Aprili 20 mwaka huu) imeingiza sh.
50,850,000.

Fedha hizo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na
kumalizika kwa timu hizo kutoka suluhu zimetokana na watazamaji 8,268
waliokata tiketi.

Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh.
20,000 na sh. 30,000 ambacho kilikuwa kiingilio cha juu kwa jukwaa la VIP
A. Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo
walikuwa 7,354.

* *

Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; gharama za tiketi sh. 5,575,500, asilimia 15
ya uwanja sh. 6,791,175, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 4,527,450
na asilimia 75 iliyokwenda kwa klabu ya Azam ni sh. 33,955,875.

Mechi iliyopita ya Azam katika michuano hiyo dhidi ya Barrack Young
Controllers II ya Liberia iliingiza sh. 44,229,000 kutokana na watazamaji
17,128 waliokata tiketi. Viingilio vilikuwa sh. 2,000, sh. 5,000, sh.
10,000 na sh. 20,000 ambacho kilikuwa kiingilio cha juu kwa jukwaa la VIP
A.

*MECHI YA JKT RUVU, YANGA YAINGIZA MIL 66/-*

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya JKT Ruvu na Yanga iliyochezwa jana
(Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh.
66,568,000 kutokana na watazamaji 11,864.**

Viingilio katika mechi hiyo namba 106 iliyomalizika kwa Yanga kutoa dozi ya
3-0 kwa wenyeji wao vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000
huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 15,702,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,154,440.68.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,984,450.40,
tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,790,670.24, Kamati ya Ligi sh.
4,790,670.24, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,395,335.12,
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 931,519.21 na Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 931,519.21.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Spurs wawapopoa Man City

Manchester United mabingwa