Ligi Kuu ya England (EPL) imerejea baada ya kupisha michuano ya kimataifa, huku vigogo wakifanya vyema, lakini Jurgen Klopp akianza Liverpool kwa suluhu dhidi ya Tottenham Hotspur.
Manchester City ndio walioonekana kutakata zaidi na kujitanua kileleni, kwani wakicheza nyumbani waliwacharaza Bournemouth 5-1, huku ingizo lao jipya kutoka Liverpool, Raheem Sterling akifunga mabao matatu, mawili yakifungwa na Wilfried Bonny huku lile la wageni likitiwa kimiani na Glenn Murray.
Arsenal waliwafyatua Watford 3-0 ugenini, kwa mabao ya kipindi cha pili yaliyotiwa kimiani na Alexis Sanchez, Aaron Ramsey na Olivier Giroud aliyeingia akitoka benchi, baada ya Theo Walcott kushindwa kuonesha makeke kwa saa nzima aliyokuwa uwanjani.
Kwa ushindi huo Arsenal wanashika nafasi ya pili kwa pointi 19 dhidi ya 21 za City. Manchester United nao walifanya mauaji sawa na Arsenal, wakiwafunga Everton kwa mabao ya Morgan Schneiderlin, Andre Herrera na Wayne Rooney ambaye hakuwaonea aibu Everton, timu yake iliyomng’arisha kabla hajajiunga United.
United wanafungana pointi na Arsenal, lakini Arsenal wana uwiano mzuri zaidi wa mabao. Kocha Louis van Gaal amesema wataweza kuwa washindani wa kweli wa ubingwa iwapo watafanikiwa kuwafunga Man City kwenye mechi ya wikiendi ijayo.
Shinikizo juu ya shingo la Jose Mourinho lilipungua Jumamosi hii, kwani walifanikiwa kuwafunga Aston Villa 2-0 baada ya kurejea kwa Diego Costa aliyekuwa nje kwa utovu wa nidhamu uwanjani. Alifunga bao moja na jingine wakajifunga Villa.
Matokeo hayo yanawaweka Chelsea katika nafasi ya 11 sawa na idadi ya pointi zao, lakini yanamwacha kocha wa Villa, Mwingereza Tim Sherwood katika wakati mgumu, ambapo inadaiwa wamiliki wanataka kuingiza kocha mpya, na David Moyes anasema anaweza kufikiria ofa yao.
Villa sasa wamebaki nafasi ya 18, mbili kutoka mkiani kabisa. Katika matokeo mengine, Crystal Palace walipigwa 3-1 wakiwa nyumbani dhidi ya West Ham. Southampton walikwenda sare 2-2 na Leicester wakati Sunderland wakiendelea kukaangika kwa kufungwa 1-0 na West Bromwich Albion.
Sunderland wanashika nafasi ya 19, ambapo wamepata kocha mpya majuzi, Sam Allerdyce, aliyepata kuwafundisha West Ham kabla ya kuamua kupumzika mwishoni mwa mkataba wake kiangazi hiki kilichomalizika. West Ham wanashika nafasi ya nne wakati Newcastle wanashika mkia.