*Spurs wawashinda Everton
Hali ya hewa bado ni mbaya Manchester United, baada ya Jumapili hii kujikuta wakipambana kufa na kupona na timu inayoshika mkia na kuambulia sare.
Man U walishafungwa 1-0 hadi dakika ya 78 pale mshambuliaji wao Robin van Persie aliposawazisha na dakika mbili baadaye Michael Carrick akafunga la pili.
Kocha David Moyes alishangilia kwa nguvu akidhani wangeibuka na pointi zote mbili, lakini mpachika mabao wa zamani wa Aston Villa, Darren Bent alifunga bao la kusawazisha dakika ya 90, ikiwa ni baada ya lile la kwanza la Steve Sidwell la dakika ya 19.
Pointi hiyo moja ni muhimu kwa vijana wa Rene Meulensteen aliyepata kuwa kwenye benchi la ufundi la Man United enzi za Alex Ferguson.
Man United walifanya mashambulizi muda mwingi wa mchezo, wakimwaga majalo 81, nyingi kuliko timu yoyote ya ligi kuu tangu 2006 lakini walishindwa kuondoka na ushindi Old Trafford. Fulham walipiga mpira golini mara tatu tu.
Fergie alionekana jukwaani kama kawaida yake, akikumbukia enzi ambazo alikuwa akipata ushindi mara kwa mara.
Moyes sasa anatakiwa kuwapanga vijana wake kwa ajili ya mechi ya Jumatano hii dhidi ya Arsenal kwenye dimba la Emirates.
SPURS WAWAPIGA EVERTON
Tottenham Hotspur wamefanikiwa kuibuka na pointi tatu White Hart Lane baada ya kuwafunga Everton 1-0.
Alikuwa Emmanuel Adebayor aliyefunga bao hilo muhimu na kuwaweka Spurs katika mbio za kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, kwani sasa wanashika nafasi ya tano.
Ya kwanzani Chelsea, wakifuatiwa na Arsenal, Manchester City na Liverpool huku Everton wakishika ya sita na Man United ya saba.
Kocha Tim Sherwood alifurahia ushindi huo, akisema kwamba sasa nafasi nne za juu zina ushindani mkubwa.
Fulham wanabaki mkiani wakiwa na pointi 20, moja pungufu ya Cardiff na tatu pungufu ya West Bromwich Albion.
Comments
Loading…