*Benitez awafunga mdomo wapinzani wake
*Mapinduzi ya Liverpool yawalipua Wigan
Mzunguko wa 28 wa Ligi Kuu ya England (EPL) umeanza kwa msisimko wa aina yake, vinara Manchester United wakipaa zaidi kileleni.
Ilikuwa pia siku ya faraja kwa Harry Redknap aliyesherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa zawadi ya timu yake, Queen Park Rangers (QPR) kupata ushindi wa tatu EPL msimu huu.
United walionesha dhamira ya kuibuka mabingwa msimu huu, walipowashindilia Norwich City mabao 4-0 katika dimba la Old Trafford.
Shinji Kagawa alionekana kuwa fiti isivyo kawaida, akafunga mabao matatu ya kwanza na Wayne Rooney kuhitimisha dakika ya 90.
Kwa ushindi huo Man U wamefikisha pointi 71, wakifuatiwa na jirani zao hasimu, Manchester City wenye pointi 56, lakini wanacheza mzunguko huu Jumatatu, watakapowakabili Aston Villa jijini Birmingham.
Hizo zinaweza kuwa salamu kwa Real Madrid wanaoingia Old Trafford Jumanne hii, kwa mechi ya marudiano dhidi ya United, zote zikiwa na bao moja lililopatikana mechi ya mwanzo Bernabeu, Hispania.
Kocha wa muda wa Chelsea, Rafa Benitez amekata ngebe za wapinzani wake waliomwotea kufungwa na kufukuzwa kazi, baada ya kuwachapa West Bromwich Albion bao 1-0.
Benitez alifyatuka wiki hii kwa kuwashambulia washabiki wanaomzomea na kumwandikia mabango ya kumkataa, akaichana Bodi ya Chelsea kwa kumwita kocha wa muda, na kuapa atakaa hadi muda wake uishe, Mei.
Hata hivyo, Chelsea walipoteza karibu nafasi 19 za kufunga na kupata moja kupitia kwa mchezaji wa Senegal, Demba Ba.
Chelea wamerejea nafasi ya tatu waliyokuwa wameiachia kwa Tottenham Hotspurs, lakini kubaki hapo kutategemea matokeo ya mechi ya Jumapili hii kati ya Spurs na Arsenal.
Liverpool wanaojaribu kuondoka kwenye nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi chini ya kocha Brendan Rodgers, walifanikiwa kupata pointi tatu na karamu ya mabao dhidi ya Wigan.
Mshambuliaji tegemeo Luis Suarez alifunga mabao matatu dakika ya 18, ya 34 na ya 49, akisakafia kazi nzuri ya Jordan Henderson aliyefungua kitabu cha mabao dakika ya pili tu.
Nao QPR walio mkiani katika msimamo wa ligi, walimpa moyo kocha wao, Redknapp katika mechi ya ugenini, kwa kuwafunga Southampton mabao 2-1.
Jay Bothroyd aliwahakikishia QPR pointi tatu muhimu, alipowafungia dakika ya 77, na wenzake wakashirikiana kulinda ushindi huo, baada ya kuwa sare katika muda mwingi wa mchezo.
Walikuwa QPR walioanza kupata bao dakika ya 14, lakini matumaini yao yalikatishwa na Gaston Ramirez aliyesawazisha muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.
Hii ilikuwa pia mara ya kwanza kwa Redknapp kurudi Southampton tangu 2005 alipokuwa kocha wao, aliposhuhudia wakishushwa daraja baada ya kufungwa na Manchester United.
Katika mechi nyingine, Everton walipumua baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Reading, baada ya kufungwa mechi ya awali uwanjani Madjeski.
Reading wamerejea kwenye eneo la kushuka daraja, ambapo mabao ya Everton wanaofudishwa na David Moyes yalifungwa na Marouane Fellaini, Steven Pienaar na Kevin Mirallas.
Reading walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Hal Robson-Kanu, na sasa itabidi wajipange vyema kwa mechi 11 zilizobaki.
Swansea waliotwaa Kombe la Ligi Jumapili iliyopita, wameendeleza sherehe katika uwanja wa Liberty jijini Swansea, baada ya kuwapiga bao 1-0 Newcastle United.
Hata hivyo walilazimika kutoka jasho, ambapo ilishadhaniwa mechi ingemalizika kwa suluhu, hadi
Luke Moore aliyeingia kipindi cha pili alipoandika bao dakika tano kabla ya mpira kumalizika.
Swansea wamefikisha pointi 40 na kujikita nafasi ya nane kwenye msimamo, huku wakiwasukuma Newcastle katika nafasi ya 15, wakiwa na pointi 10 nyuma ya vijana hao wa Wales.
Kocha Sam Allardyce wa West Ham alifarijika kwa ushindi wa kwanza ugenini tangu Novemba mwaka jana, pale vijana wake walipowafunga Stoke 1-0.
Jack Collison alinasa pasi ya Ricardo Vaz Te kabla ya kumtazama kumpeleka sokoni golikipa Asmir Begovic na kuzisalimu nyavu.
Sunderland walipigana kufa na kupona kukomboa mabao mawili na kwenda sare ya idadi hiyo na Fulham.
Ilikuwa furaha kwao, maana sare hiyo imesitisha mfululizo wa kushindwa mechi tatu. Fulham walipata mabao yao kupitia kwa Dimitar Berbatov kwa penati na Sascha Riether aliyefunga kwa shambulizi la kushitukiza kipindi cha kwanza.
Craig Gardner alifunga penati waliyopewa dakika ya 37 kabla ya Stephane Sessegnon kusawazisha, muda mfupi baada ya Berbatov kukosa bao akiwa na kipa Simon Mignolet.
Comments
Loading…