in , , ,

Man U waangusha moja tena

 

*De Gea amshangaa Van Gaal

 

Manchester United wameendelea kupata ushindi mwembamba wa 1-0 katika mechi ya pili mfululizo, lakini wakijikusanyia pointi zote ambazo zingewezekana.

 

Ijumaa hii waliendeleza rekodi yao ya kutofungwa katika dimba la Villa Park walipowafunga Aston Villa waliokaa vibaya 1-0, bao likitiwa kimiani na kinda anayedhaniwa atatolewa kwa mkopo, Adnan Januzaj.

 

Vijana hao wa Louis van Gaal walianza ligi kuu ya hapa kwa kuwafunga Tottenham Hotspur 1-0 kwenye mchezo ambao hawakuonesha makali sawa na wa Ijumaa hii, na katika ule wa awali walishinda kwa bao la Spurs kujifunga wenyewe.

 

Villa waliomuuza mpachika mabao wao tegemeo, Christian Benteke kwa Liverpool walikuwa dhaifu karibu muda wote wa mchezo, ambapo United wangeweza kupata mabao zaidi iwapo Memphis Depay angetia jitihada za kutosha.

 

Mshambuliaji namba moja wa United, Wayne Rooney aliendelea kuwa doro kama mechi iliyopita, japokuwa amejipangia kufunga mabao walau 20 msimu huu na kocha alisema huenda asinunue mshambuliaji mwingine kwa sababu ya uwapo wa nahodha huyo.

 

Pamoja na Januzaj kufunga bao hilo la ushindi, bado Van Gaal anasema kwamba Mbelgiji huyo anatakiwa kufanya zaidi ya kufunga, bila shaka akimaanisha katika suala zima la uchezeshaji na kupanga mashambulizi.

 

Alipangwa kwa kushangaza kwenye mechi ya jana, kwani katika nafasi yake alitarajiwa awepo Ashley Young. Timu zinazosubiri kwa hamu atolewe kwa mkopo ili zimchukue ni Everton na Sunderland.

 

Kwa mara nyingine, kipa namba moja wa United, David De Gea hakuwapo kwenye kikosi kilichoanza wala kwenye wachezaji wa akiba, badala yake alianza kipa wa Timu ya Taifa ya Argentina aliyesajiliwa Old Trafford kiangazi hiki, Sergio Romero.

 

De Gea ameeleza kushitushwa kwake na taarifa alizotoa Van Gaal kwamba eti alimwambia kocha kwamba hakuwa na hamu ya kucheza katika mechi zote mbili. Mtoa taarifa wake amekanusha habari hizo na kusema hapakuwa na kitu kama hicho, bali alikuwa na hamu ya kurejea langoni.

 

Mhispania huyo anahusishwa na kurudi nyumbani kuchezea Real Madrid, wakati huu ambapo amebakisha mwaka mmoja tu kumaliza mkataba wake, lakini Man U hawataki kumuuza, vinginevyo wanataka Madrid wawape beki wao wa kati, Sergio Ramos.

 

Van Gaal anadai kwamba hakumchezesha kwani licha ya kusema hana hamu ya kucheza, walivyomwona kwenye mazoezi amebadilika, si yule wa zamani na hangeweza kuhimili mikiki ya mechi hizo.

 

Katika hatua nyingine, Van Gaal amemtupa kipa huyo kwenye kufanya mazoezi na timu B na hakuruhusiwa kusafiri na kikosi cha kwanza kwenda Villa Park Ijumaa. United walikataa ofa ya pauni milioni 20 kutoka Madrid, wakitaka mauzo yake yavunje rekodi ya dunia.

 

Mechi za Jumamosi hii ni Southampton dhidi ya Everton, Sunderland wanawakaribisha Norwich wakati Newcastle ni wageni wa Swansea. Spurs wanawasubiri Stoke hapo White Hart Lane , West Bromwich Albion wanasafiri kwenda Watford huku West Ham wakiwa wenyeji wa Leicester.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

‘De Gea hataki kucheza’

Barcelona wachakazwa 4-0