in , , ,

Barcelona wachakazwa 4-0

 

Ni mafuriko. Mabingwa wa Hispania na Ulaya, Barcelona wameaibishwa kwa kuchakazwa 4-0 na Athletic Bilbao.

 

Wakicheza mechi ya mkondo wa kwanza ya Super Cup la Hispania, Bilbao waliwalambisha mchanga Barca, ambapo Aritz Aduriz alifunga mabao matatu – hat trick kwenye mchezo huo ambao haukuwa wa kawaida.

 

Alikuwa ni Mikel San Jose aliyefungua kitabu cha mabao dakika ya 13tu ya mchezo kwa mkwaju mzuri kutoka kwenye duara la kati na kutinga nyavuni kutokana na makosa ya kipa wa Barca, Marc-Andre Ter Stegen. Jose alifunga mabao manane msimu uliopita licha ya kwamba ni kiungo mkabaji.

 

Ter Stegen alitoka golini kwa ajili ya kuanua mpira, lakini ukaishia kwa Jose ambaye alipiga mpira wa juu na kumzidi maarifa kipa ambaye tayari alikuwa ameliacha lango lake, akabaki akijilaumu sambamba na wachezaji wengine.

 

Barcelona waliruhusu mabao matatu kwenye dakika 45 za kipindi cha pili, wakiachwa na mlima mkubwa wa kupanda kwenye mechi ya mkondo wa pili Jumatatu hii, pengine watamudu kwa sababu watacheza nyumbani Nou Camp.

 

Hii ni mara ya pili katika mechi mbili kwa Barcelona kuridhia kufungwa mabao manne, baada ya kuwafunga Sevilla 5-4 kwenye mechi ya Super Cup la Uefa majuzi. Kocha Luis Enrique atasikitishwa na matokeo haya wakati akipambana kuweka rekodi kama ya msimu uliopita ya kutwaa mataji matatu.

 

Kwa bahati mbaya kwao, mechi yao ya kwanza katika Ligi Kuu ni dhidi ya klabu hii hii, tena kwenye uwanja walikocharazwa wa San Mames.

 

Kocha Enrique alichezesha wachezaji kadhaa wasio na uzoefu, ikiwa ni pamoja na Sergi Roberto na Marc Bartra, lakini pia walikuwamo nyota kama Lionel Messi na Luis Suarez waliocheza dakika zote 90.

 

Akina Andres Iniesta na Gerard Pique walikuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba, hivyo Bartra alishirikiana kwenye kiungo cha kati na nahodha wa zamani wa Arsenal, Thomas Vermaelen, aliyekuwa akicheza mechi ya pili tu kwa klabu hii tangu ajiunge nao, kutokana na kuwa na majeraha tangu misimu miwili iliyopita.

 

Messi hakucheza vyema, pengine kutokana na kucheza na watu ambao hakuwazoea lakini alipiga mpira mmoja mzuri wa adhabu ndogo ambao ilibidi Gorka Iraizoz akiwa langoni afanye kazi ya ziada. Kwenye mechi ya marudio kuna uwezekano wa Enrique kuchezesha kikosi kamili cha kwanza.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Man U waangusha moja tena

NI MENDES ANAYEMUWEKA FALCAO CHELSEA