Manchester United na Real Madrid wameingia vitani kusaka huduma ya
mchezaji nyota wa Ufaransa, Paul Pogba.
Habari zilizokuwapo ni kwamba tayari mchezaji huyo alishaafikiana na
Man United lakini nyingine zinasema kwamba bado mchezaji huyo mwenye
umri wa miaka 23 hajafikia hatua ya kuhamia Old Trafford.
Kiungo huyu wa Juventus amekuwa na wakati mzuri kwenye michuano ya
Euro 2016 nchini mwake Ufaransa na Jumapili hii atamalizia kwa fainali
dhidi ya Ureno.
Madrid wanaonolewa na Zinedine Zidane wanamtaka Pogba ili kujiimarisha
lakini pia ni aina ya klabu wanaopenda kuingia dili kubwa na
wachezaji, ambapo hadi sasa ndio wanashikilia rekodi ya kununua
mchezaji ghali zaidi duniani katika Gareth Bale kutoka Tottenham
Hotspur.
Walifanya hivyo kwa Cristiano Ronaldo kutoka Manchester United kabla
yake. Hata hivyo, taarifa za ndani kutoka Hispania zinasema kwamba
kuna kila dalili za Pogba kuhamia United atakakokuwa chini ya kocha
Jose Mourinho.
Mabingwa wa England, Leicester, wanazidi kutikiswa ambapo sasa klabu
ya Shanghai SIPG ya China imeingia kwenye mkakati wa kumsajili N’Golo
Kante.
Wachina hao wanaonolewa na bosi wa zamani wa Timu ya Taifa ya England,
Sven Goran Eriksson, wapo tayari kuweka mezani pauni milioni 35kwa
mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25.
Manchester City wanataka kupambana ili kumsajili Leroy Sane, 20,
kutoka Schalke, siku chache baada ya kutolewa kwenye Euro 2016 akiwa
na Wajerumani wenzake.
Arsenal wamefanya mazungumzo juu ya uwezekano wa kumsajili
mshambuliaji wa Lyon ya Ufaransa, Alexandre Lacazette (25), lakini
wanaiona bei yake ya pauni milioni 42 kuwa ni kubwa mno.
Ni juzi tu Washika Bunduki wa London walikataa ofa ya pauni milioni 30
kutoka Juventus ambao wanamtaka mshambuliaji wa Arsenal, Alexis
Sanchez.
West Ham wameachana na fursa ya kumsajili Robin van Persie kutoka
Fenerbahce, japokuwa mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal na Manchester
United mwenye umri wa miaka 32 yupo tayari kupunguziwa mshahara kwa
kiasi kikubwa ili arudi England.
Badala yake, Wagonga Nyundo hao wa London wametoa ofa ya pauni milioni
25.7 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Colombia, Carlos Bacca,
29, kutoka AC Milan nchini Italia.
Southampton wapo kwenye mazungumzo kwa ajili ya mauzo ya Mtaliano
Graziano Pelle kwa pauni milioni 13 kwenda klabu ya Shandong Luneng ya
China.
Kocha wa Chelsea, Antonio Conte yupo tayari kutumia pauni milioni 34
kwa ajili ya kuimarisha ukuta wa timu yake kwa kumsajili beki wa kati
wa Napoli, Kalidou Koulibaly, 25.
Everton wapo katika nafasi nzuri ya kumsajili kiungo wa Manchester
United, Juan Mata, 28, kwani Barcelona wameachana na kumfukuzia.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania ana wakati mgumu, kwani kocha
Mourinho aliyemkataa Chelsea na kumuuza Man United sasa ametua Old
Trafford na kuna kila dalili kwamba hatampa nafasi ya kutosha kucheza.
Mshambuliaji wa West Bromwich Albion, Saido Berahino, 22, amepewa ofa
ya mkataba mpya wenye thamani ya pauni 65,000 kwa mwezi ili asiondoke
kwenda Stoke wanaomtaka.