*Wigan waendelea kutetea taji
Manchester City wamelipa kisasi kwa kuwafunga Chelsea 2-0 katika mechi ya Kombe la FA na kutinga robo fainali.
Ilikuwa furaha kwa kocha Manuel Pellegrini kwa sababu Chelsea waliwafunga mara mbili kwenye Ligi Kuu ya England lakini sasa Man City wamefanikiwa kuwatupa nje ya michuano hii.
Mabao ya City yalifungwa na Stevan Jovetic dakika ya 16 ya mchezo kabla ya majeruhi aliyerejea dimbani, Samir Nasri kufunga dakika ya 67 na kumfunga mdomo kocha wa Chelsea, Jose Mourinho.
Pellegrini anahifadhi ndoto zake za kutwaa makombe manne msimu huu, kwa kuwa bado timu yake ipo pia kwenye michuano ya Kombe la Ligi, Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya watakakokutana na Barcelona Jumanne ijayo.
Hii ni mara ya pili kwa Pellegrini kumfunga Mourinho katika mechi 10 walizopata kukutana wakiwa na klabu tofauti.
Chelsea hawakucheza vyema, na walianza kuonesha dalili za uchovu kwenye mechi iliyopita dhidi ya West Bromwich Albion ambapo waliambulia sare dakika za mwisho ilhali walikuwa wakiongoza kwa 1-0.
Chelsea walilenga mikwaju mitatu tu golini katika dakika zote 90 kupitia kwa Willian, Cesar Azpilicueta na dakika za lala salama Gary Cahill.
Eden Hazard aliye kwenye kiwango siku hizi hakuwa chochote mbele ya akina James Milner na Pablo Zabaleta ambapo kwa ujumla Chelsea walikosa mbinu za kupenya ngome ya City.
SUNDERLAND, WIGAN MAMBO SAFI
Katika mechi nyingine za Kombe la FA, Sunderland walifanikiwa kuwafunga Southampton 1-0 katika mechi waliyocheza nyumbani kwao.
Bao la mapema kipindi cha pili la Craig Gardner lilitosha kuwazamishia mbali vijana wa Mouricio Pochettino wakati Gus Poyet akifurahia timu yake kusonga, ikiwa pia imeingia fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Man City, mechi itakayochezwa mapema Machi.
Mabingwa watetezi wa kombe hilo, Wigan Athletic waliwatupa nje Cardiff City kutoka Wales kwa jumla ya mabao 2-1.
Mabao ya Wigan ambao pamoja na kutwaa kombe hilo msimu uliopita walishuka daraja, yalifungwa na Chris McCann a Ben Watson wakati lile la Cardiff lilifungwa na mshambuliaji wao machachari, Frazier Campbell.
Mechi baina ya Sheffield Wednesday na Charlton iliahirishwa kutokana na hali mbaya ya hewa.
Jumapili hii kuna mechi kubwa Emirates, ambapo Arsenal wanawakaribisha Liverpool katika FA Cup ambao mara ya mwisho dimbani hapo walionja kichapo cha bao 1-0 lakini Arsenal kule Anfield walikung’utwa 5-1, zote zikiwa mechi za Ligi Kuu.
Comments
Loading…