Mabingwa wa England, Manchester City wameendelea kufanya vibaya kwenye mashindano ya kimataifa, baada ya kupigwa 2-1 na CSKA Moscow .
City ambao sasa wanashikilia mkia kwenye kundi lao la kuwania kufuzu hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) walikubali bao katika dakika ya pili tu ya mchezo huo uliofanyika nyumbani Etihad, lakini Yaya Toure alisawazisha dakika sita baadaye.
CSKA waliwazidi nguvu kwa bao la Seydou Doumbia la dakika ya 34, akiwa ndiye mchezaji aliyefunga bao la kwanza pia. Mambo yalikuwa yamemalizika mapema hiyo, kabla hata kipindi cha pili kuanza, na nahodha wa City, Vincent Kompany anaamini bado wanaweza kufanya vizuri.
Kana kwamba kichapo hakitoshi, wachezaji wawili wa City, Toure na Fernandinho walipewa kadi nyekundu, ambapo watakosa mechi ngumu na muhimu dhidi ya Bayern Munich, na kwa namna fulani ni rahisi kusema kwamba wanaelekea kutolewa.
Wamefikisha pointi mbili tu kutokana na mechi nne, wakiwa wamefungwa mbili na kwenda sare mbili, wakati Bayern wana pointi 12 kwa kushinda mechi zao zote. Roma wnashika nafasi ya pili kwa pointi nne sawa na CSKA na kuwaacha City kama yatima.
Katika matokeo mengine, Chelsea walichechemea kwa kwenda sare ya 1-1 na NK Maribor, ambapo kocha Jose Mourinho amekilalamikia kikosi chake kwa kucheza kichovu. Hata hivyo, Chelsea wanaongoza kundi lao kwa point inane, wakifuatiwa na Schalke wenye pointi tano, Sporting nne na Maribor tatu.
Matokeo mengine ni kwamba Ajax walikubali kipigo cha 2-0 kutoka kwa Barcelona, Paris Saint-Germain wakawafunga Apoelic Nic 1-0, Sporting wakalala kwa Schalke 4-2, Athletic Bilbao wakafungwa na Porto 2-0 na Shaktar Donetsk wakawachakaza BATE Bor 5-0.
Comments
Loading…