in , , ,

Man City, Everton wateleza

Real Madrid wawapiga Barca Copa Del Rey

NIA za Manchester City kutwaa ubingwa na Everton kupata nafasi ya nne zimepata mapigo makubwa, baada ya City kwenda sare huku Everton kufungwa, wote wakicheza na timu dhaifu.
Man City ambao walikuwa wakipigiwa chapuo la ubingwa kwa muda mrefu kutokana na uwezo wao mkubwa wa kufunga mabao na mechi walizokuwa nazo mkononi walianza kupoteza mwelekeo walipochapwa na Liverpool hivi karibuni.
Kwa kupoteza mechi hiyo, walijiweka katika nafasi mbaya, kwani hata wangeshinda mechi zote zilizobakia, watategemea kuteleza kwa Liverpool. Kana kwamba hiyo haitoshi, usiku wa Jumatano hii wamekwenda sare ya 2-2 na Sunderland wanaoshika mkia na kuelekea kushuka daraja.
Wakicheza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Etihad ambako ni kawaida kutoa kichapo kikubwa, Man City walikabwa vilivyo, licha ya kuanza kuongoza dakika ya pili tu kupitia kwa Fernandinho. Bao hilo lilisawazishwa dakika ya 73 na Connor Wickham na kasha akapachika tena la pili na la kuongoza dakika 10 baadaye.
Hata hivyo, vijana hao wa Manuel Pellegrini walijitahidi na Samir Nasri akachomoa dakika mbili kabla ya mechi kumalizika na kuondosha aibu ya City kufungwa nyumbani.
Kwa matokeo hayo, City wamefikisha pointi 71 wakati Liverpool wanazo 77, Chelsea 75. Licha ya kuwa na mechi moja mkononi, City wanaweza kuishia nafasi ya tatu iwapo Liver na Chelsea watafanya vyema kuliko wao. Sunderland wanabaki mkiani hata hivyo.

DUA LA ARSENAL LAWAPATA EVERTON
Katika mechi nyingine muhimu, Everton waliduwazwa na Crystal Palace baada ya kufungwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Goodison Park kwa 3-2 na kusitishwa mfululizo wao wa kushinda mechi saba.
Everton waliojijenga na kujiamini sana chini ya Kocha Roberto Martinez walijikuta wakipelekeshwa tangu mwanzo, kwani walifungwa bao la kwanza katika dakika ya 23 kupitia kwa Jason Puncheon kabla ya Scott Dann kuwaadhibu tena dakika nne tu baada ya kuanza kipindi cha pili.
Everton waliongeza jitihada na kufanikiwa kufunga bao dakika ya 61 kupitia kwa Steven Naismith lakini Palace wanaofundishwa na Tony Pulis walirejea kwenye nyavu za The Toffees dakika ya 73 kwa bao la Cameron Jerome. Everton walipunguza maumivu kwa Kevin Mirallas kufunga katika dakika ya 86.
Matokeo hayo maana yakie ni kwamba Everton na Arsenal wana mechi sawa, na Everton wapo nyuma ya wenzao kwa pointi moja na wikiendi hii wanawakaribisha Manchester United wanaofundishwa na kocha wao wa zamani, David Moyes.
Palace kwa ushindi huo wamejintyanyua hadi nafasi ya 11 baada ya kufikisha pointi 40 na kujiweka salama katika nafasi ya kubaki ligi kuu.

REAL MADRID WAWAADHIRI BARCA, MABINGWA COPA DEL REY
Nchini Hispania, Real Madrid wamewaadhiri wapinzani wao wakubwa, Barcelona kwenye fainali ya Kombe la Mfalme kwa mabao 2-1.
Alikuwa ni gareth Bale aliyefunga bao la ushindi la aina yake dakika tano kabla ya kipenga cha mwisho akimtoka beki Marc Bartra katikati ya uwanja jijini Valencia kabla ya kumzidi maarifa kipa Jose Manuel Pinto.
Real waliocheza bila nyota wao, Cristiano Ronaldo walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa winga Angel Di Maria lakini Barca wakaswazisha kwa kichwa kwa beki huyo kusawazisha makosa yake kipindi cha pili.
Bale aliyesajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 85 kutoka Tottenham Hotspur alionesha thamani yake halisi uwanjani hapo, alipofanya kazi alivyotakiwa. Kocha carlo Ancelotti alibebwa juu juu na wachezaji wake huku akiwa amenyanyua kombe hilo la mfalme.
Kwenye Ligi Kuu, Madrid wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 79, Atletico Madrid wakiongoza kwa pointi 82 huku Barcelona wakishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 78.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arsenal wawatega Everton

Yaya Toure: Weusi unaniponza