Jumamosi wiki hii tumeshuhudia mchezo wa kwanza wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini na Pyramids ya Misri. Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Loftus Versfield jijini Pretoria nchini Afrika kusini ulimalizika kwa sare 1-1.
Bao la Pyramids lilipatikana katika dakika za lala salama na kufuta lile la Lucas Ribeiro. Mchezo wa marudiano utachezwa nchini Misri ambako bingwa atakabidhiwa kombe hilo. Katika fainali hii Mamelodi Sundowns ilikuwa mara yao ya tatu kwenye mashindano ya CAF huku Pyramids wakiingia kwa mara ya kwanza. TANZANIASPORTS imeshuhudia mchezo huo na kuibuka na tathmini kuwa mwenyeji wa mchezo Mamelodi Sundowns alishindwa kumaliza mchezo mapema sana kutokana na aina ya uchezaji wake.
Uteuzi wa kikosi wenye utata
Kocha Miguel Cardoso aliingia kwenye mchezo huo akiwa na washambuliaji wawili Sales na Lucas Ribeiro ambao ni Wabrazil, huku akiwaweka benchi Shalulile na Themba Zwane. Kwenye kiungo alianza na Allende na Mathews wakisaidiana na Mokoena. Hata hivyo Mamelodi licha ya kuwa nyumbani walijikuta kikosi chao kidhibitiwa na wageni hao. Ilimchukua dakika 36 tu kocha Miguel Cardoso kubaini kuwa alifanya makosa katika uteuzi wa kikosi chake, kwani alilazimika kumtoa nje kiungo chipukizi Mathews na nafasi yake kuchukuliwa na Adams.
Huu ulikuwa ujumbe kuwa Pyramids walikuwa wamemshika pabaya mno. Safu ya ushambuliaji ilikuwa inamtegemea Lucas Ribeiro ambaye alikuwa akicheza pembeni kulia zaidi huku Sales akitumika pembeni kushoto hivyo kusababisha eneo la mshambuliaji namba 9 kuwa tupu muda mwingi.
Hali hiyo iliwapa mwanya Pyramids kucheza kwa utulivu katika safu yao ya ulinzi kwani hawakukutana na misukosuko yoyote. Ingizo la Shalulile katika kipindi cha pili kulisaidia kuirudisha nyuma Pyaramids ambayo ilikuwa ikicheza kwa ufundi wa hali ya juu bila kupoteza muda wala kumhadaa mwamuzi. Kwahiyo utata wa kocha katika upangaji wa kikosi ulichangia timu yake kuwa dhaifu kwenye eneo la kushambulia.
Matukio machache ya kumaliza mechi
Kama kuna jambo ambalo linawagharimu Mamelodi Sundowns kwa muda mrefu ni kukosekana ile hali ya uchezaji wa kumaliza mechi mapema. Katika uchezaji huo Mamelodi wanakosa ule ukali wa kucheza kwa kasi na kuwa na washambuliaji wenye kuimaliza mechi mapema kwa kufunga mabao. Ufundi huo unategemea sana aina ya wachezaji wanaoandaliwa na kocha wao.
Timu inaingia uwanjani ikiwa na dakika 15 za kwanza za kumaliza mechi kwa maana ya kufunga mabao ya kutosha ili kuwavuruga wapinzani. Mfano unafunga bao moja la haraka huku timu inacheza kwa uchu wa kusaka bao lingine. Ni sababu hii yapo matukio katika timu nyingine kufunga hadi mabao mawili na matatu ndani ya dakika 15 za kwanza ili kuwavuruga zaidi wapinzani wao. Kimsingi mpinzani wake anapokuja kutulia tayari anakuwa nyuma kwa mabao matatu au mawili.
Mamelodi Sundowns hawana hiki kitu na licha ya kubadilisha kocha, wanacheza mtindo uleule ambao unachelewesha kupata ushindi. Ni kama hawawezi kutengeneza matukio mengi ya kuwapatia mabao. Kwa lugha ya kimpira Mamelodi wanacheza ‘Kifaza’ sana, hawalazimishi matukio hali ambayo inawagharimu pale wanapzidiwa maarifa.
Ubora wa Pyramids

Klabu hii inaingia kwa mara ya kwanza kwenye fainali za CAF, lakini wanacheza soka la hali ya juu sana. uchezaji wa Pyramids ni tofauti na klabu nyingi za Kiarabu. Pyramids hawapotezi muda bure, hawamdanganyi mwamuzi katika matukio, badala yake kazi yao inakuwa kutandaza soka tamu ambalo linawavutia wengi.
Uchezaji wao umekuwa kivutio kwa sababu wametengenezewa ufundi mwingi kuliko matukio ya kulazimisha kama ambavyo zinavyofanya timu nyingine za Kiarabu. Licha ya tofauti hii, bado wanakabiliwa na changamoto ya kuwazuia timu inayocheza kwa kasi zaidi yao na yenye uwezo wa kupigiana pasi nyingi eneo la hatari au kuachia mikwaji mikali kwa muda wote wa mchezo.
Kibarua kigumu cha Cardoso
Licha ya kufikisha fainali ya Ligi ya Mbaingwa Afrika kocha wa Mamelodi Miguel Cardoso anakabiliwa na kibarua kigumu ya kulinda kazi yake hasa endapo atafungwa kwenye mchezo wa marudiano. Mamelodi Sundowns imeundwa na kiu ya kutwaa mataji, kwahiyo kama kocha ameshindwqa kuipa taji maana yake amefeli katika msimu wake. kwenye msimu wake wa kwanza, Miguel Cardoso ameipeleka fainali Mamelodi, lakini kwa mashabiki na viongozi wa klabu hiyo kufika hatua ya fainali si habari kubwa kwao kwani wanachotaka ni kombe hilo. Kiu ya kunyakua kombe ndiyo iliyomfukuzisha Rhulani Mokwema klabuni hapo, lakini Cardoso akilikosa kombe naye lazima atafungashiwa virago.
Mfumo anaotumia wa kujihami na kushambulia kwa kushtukiza si kile ambacho kinaundwa na klabu ya Mamelodi ambayo ni maarufu kwa jina la Brazilians. Mfumo wa kujihami na kushambulia kwa kushtukiza unahitaji kuwa na mshambuliaji au washambuliaji angalau wawili au watatu wenye uwezo wa kutumia nafasi chache kumaliza mchezo. Lakini kwenye mchezo wake wa kwanza washambuliaji wake wawili Themba Zwane na Shalulile walikuwa benchi. Hii ina maana licha ya kutaka kushinda, alijikuta akizuia ushindi huo kutokana na mpangilio wa kikosi chake.